|
WASIA
WA KUMI NA MOJA-SUBIRI KWA MITIHANI INAYOKUSIBU.
Ndugu yangu katika imani-Allah Taala atupe imani ya kweli
itakayotupa kheri za duniani na akhera-Aamiyn! Tunaendelea kuusiana katika
mapenzi ya Allah, ufahamu na uelewe kwamba miongoni mwa mambo makubwa
yenye kuokoa ni kusubiri kwa mitihani unayotahiniwa na Allah. Subira yako
hii iende sambamba na kuzishukuru neema za Allah alizokuneemesha na kuipa
mgongo dunia imshughulishayo mja kiasi cha kumsahau Allah Mola Muumba
wake. Elewa kuwa subira ni miongoni mwa ibada ngumu lakini zenye fadhila
kubwa kabisa. Subira ni hitajio muhimu la kila muumini katika hali zake
zote na katika kipindi chake chote cha kuishi katika ardhi hii ya Maulana.
Subira ni siri na ufunguo wa fanaka, furaha, amani, salama na mafanikio
yote katika ulimwengu huu wa mpito na ule wa milele. Qur-ani Tukufu
imesheheni aya kathiri zinazotaja fadhila za subira, aya hizi
zinashereheshwa na hadithi adida (nyingi) za Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie. Hebu tuzitafakari kwa pamoja aya zifuatazo tuone namna gani
Allah anavyotuita katika biashara ya subira; biashara isiyododa wala
kukhasirika, tusome: “ENYI MLIOAMINI! JISAIDIENI (katika mambo yenu) KWA
SUBIRA
NA SWALA;
BILA SHAKA ALLAH YU PAMOJA NA WANAOSUBIRI” [2:153]
Haya mpenzi ndugu yangu-Allah atupe fahamu-tunaelewa nini
katika aya hii tukufu? Bila shaka utakubaliana nami ndugu yako kuwa aya
hii inaeleza kuwa muumini ndiye mlengwa na shabaha ya mitihani na
misukosuko kama inavyotuwazikia kupitia aya hii: “NA TUTAKUTIENI KATIKA
MSUKOSUKO WA (baadhi ya mambo haya); KHOFU
NA NJAA
NA UPUNGUFU
WA MALI NA WA WATU NA WA MATUNDA. NA WAPASHE KHABARI NJEMA WANAOSUBIRI”. [2:155]
Tayari
imetuthibitikia kuwa muumini ni lazima ataonjwa na Mola wake kwa kumtahini
kwa mitihani mbalimbali, hana pa kukimbilia. Sasa la msingi la kujiuliza
ni je, akisibiwa na masaibu na mitihani hii ya Mola wake afanye nini? Aya
ikatoa dawa na kuonyesha kuwa tegemeo na kimbilio pekee la muumini wakati
wa masaibu na misukosuko ni SUBIRA na SWALA. Kwa maneno mengine tunaweza
kusema subira na swala ni silaha kali inayompa ushindi mnono muumini
katika vita ngumu ya masaibu na misukosuko ya maisha ya kila siku. Aya
ikamalizia kwa kueleza daraja na cheo cha wanaosubiri na kuswali pindi
waonjwapo na Mola wao kuwa watakuwa pamoja na Allah. Yaani msaada wa Allah
utakuwa pamoja nao katika dhiki na masaibu yote ya leo hapa duniani na ya
kesho kule akhera. Mpenzi ndugu yangu, je unapenda kupendwa na Allah? Kama
unapenda na bila shaka hakuna asiyependa, basi subiri unaposibiwa na
masaibu yatokayo kwa Allah, kwani subira hiyo ndio thamani ya kuyanunulia
mapenzi ya Allah, tusome pamoja na tuamini: “...NA ALLAH ANAWAPENDA
WAFANYAO SUBIRA”. [3:146]
Ndugu
yangu-Allah atuwafikishe kusubiri-tuendelee kutafakari pamoja kwa maslahi
na manufaa ya nafsi zetu wenyewe. Allah Mola Mwenyezi anamkhutubu Mtume
wake-Rehema na Amani zimshukie-kwa kumwambia: “NA SUBIRI NA
KUSUBIRI KWAKO KUSIWE ILA KWA AJILI YA ALLAH TU...”
[16:127]
Sote
tunatambua kuwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alipewa na Mola wake
jukumu gumu na zito la kuufikisha ujumbe wake kwa waja wake. Katika
kulitekeleza jukumu hili Bwana Mtume alikumbwa na misukosuko mikubwa
ambayo ilikuwa ni kikwazo kikubwa katika kufikisha ujumbe wa Allah kwa
waja wa Allah. Ndipo Allah aliyemtuma mja wake kwa waja wake akamuagiza
Mtume wake kusubiri. Kwa kuwa kusubiri tu hakutoshi anamwambia subira yake
yote iwe ni kwa ajili yake yeye tu Allah ambaye ndiye atakayewalipa wote
wanaosubiri: “...NA BILA SHAKA WAFANYAO SUBIRA (wakajizuilia na maasia
na wakaendelea kufanya ya twaa) WATAPEWA UJIRA WAO PASIPO HESABU”.
[39:10]
Bwana
Mtume akanyenyekea na akajisalimisha kwa Mola wake, akasubiri kwa ajili ya
Allah mpaka nusura ya Allah na ushindi ukapatikana na watu wakaingia
katika dini ya Allah makundi kwa makundi. Nasi basi ewe ndugu yangu katika
Uislamu tumuige na kumgeza Mtume wa Allah katika kusubiri kwa ajili ya
Allah ili itufikie nusra na ushindi kutoka kwa Allah.
Ewe
ndugu yangu, nakusihi tukiri kuwa muumini ana haja kubwa kuelekea subira
wakati wa kufikwa na mabalaa mbalimbali yasiyo na hodi wala taarifa.
Asubiri na wala asipapatike anapofikwa na mabalaa hayo, anachotakiwa
kufanya ni kutulia, kunyenyekea, asione dhiki wala uchungu. Asiwashitakie
viumbe mtihani wake huo, bali arejee kwa Allah kwa unyenyekevu na
kujisalimishia kwake amuombe faraja na awe na dhana njema kwa Allah Mola
awaonjaye waja wake. Na ajue
kwa yakini kwamba Allah hakumshushia balaa hilo ila anazo yeye ndani yake
kheri nyingi. Ikiwa ni pamoja na kuinuliwa daraja, kuzidishiwa mema yake
na kufutiwa madhambi kwa ushahidi wa hadithi za Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie. Lakini yote haya hayapatikani ila kwa gharama ya subira,
tena kusubiri kwenyewe kuwe ni kwa ajili ya Allah tu. Muumini anahitajia
sana subira katika kufanya mambo ya twaa; mambo ambayo ndani yake
inapatikana radhi ya Allah, ambayo ndio matakwa na lengo mama la kuazimiwa
na kufikiwa na kila muislamu. Asubiri mja kwa kutokuona uvivu kufanya
mambo ya twaa, ayatekeleze kama alivyoamrishwa na Allah kwa ukamilifu na
unyenyekevu mkubwa. Na ayafanye kwa ajili tu ya Allah (Ikhlaaswi) na waka
asikusudie kuwaonyesha watu cho chote katika mambo ya twaa anayoyafanya.
Ni muhimu kila muislamu akatambua kuwa hali na tabia ya nafsi ni kuona
uzito na uvivu katika kufanya mambo ya twaa. Kwa hali hii basi, inambidi
mja ajitahidi upeo wa jitihada yake kuilazimisha nafsi yake kuzoea kutenda
mambo ya twaa kwa subira njema.
Ndugu
yangu mpenzi-Allah aturehemu-elewa na ufahamu kwamba eneo jingine ambalo
mja anahitajia sana subira ni katika bahari tamu na kipenzi cha nafsi;
bahari maasi. Allah Mola Mtukufu anatufahamisha juu ya tabia ya nafsi:
“...KWA HAKIKA (kila) NAFSI NI YENYE KUAMRISHA SANA MAOVU
ISIPOKUWA ILE AMBAYO MOLA WANGU AMEIREHEMU...” [12:53]
Kwa
hali hii basi, kumempasa na kumuwajibikia mja kuizuilia nafsi yake na
mambo ya maasi na haramu. Hii ni kwa sababu nafsi huyapenda mno na
kuyaonea tamu mambo hayo kwa hivyo humkokota na kumvutia mja katika mambo
hayo. Aizuie kwa subira njema kufanya maasi kwa dhahiri, kuyazungumzia na
kuyaelekea kwa batini.
Naam,
muumini anahitajia subira kubwa katika matamanio yake halali. Haya ni yale
yote ambayo raghba ya nafsi ndani ya matamanio hayo hukomelea katika
kuionea ladha na starehe dunia bila ya kuwa na athari katika maisha yake
ya milele kule akhera. Hii ni kwa sababu kuzama na kujiachia katika
matamanio halali humburuzia mja katika mambo ya shubuha na haramu.
Hukithirisha raghba ya dunia na kumchochea mja kuipupia, jambo ambalo
hupelekea kuyapenda zaidi maisha ya dunia yenye kupita kuliko yale ya
nyumba ya milele (akhera). Mpaka hapa natumai ndugu yangu-Allah
akurehemu-kwa msaada wa Allah utakuwa umejua thamani ya subira na haja ya
muumini kuwa na subira katika hali na maisha yake yote. Basi ninakuusia
bila ya kujisahau mwenyewe tulazimikiane na subira tutafuzu kwa kupata
kheri na mafanikio yote ya dunia na akhera.
|