|
WASIA
WA KUMI-KUWA BAINA YA KHOFU NA MATUMAINI.
Ndugu
mpenzi katika imani-Allah atuwafikishe kupendana kwa ajili yake-ni wajibu
wetu kumuhimidi Allah aliyetuwafikisha
kuusiana mema na kukatazana mabaya. Ni kheri kwetu ikiwa tutafahamu
kwamba miongoni mwa mambo yenye kuokoa ni mja kuwa katika hali ya baina ya
khofu na matumaini. Kuwa katika hali baina ya khofu na matumaini ni katika
jumla ya daraja tukufu zinazopasa kuwaniwa na kila muislamu. Allah Mola
Mtukufu amewasifia mitume wake na wafuasi wao wema kwa sifa mbili hizi
pale aliposema: “...WANATUMAI REHEMA ZAKE NA WANAOGOPA ADHABU YAKE.
HAKIKA ADHABU YA MOLA WAKO NI YA KUOGOPWA”. [17:57]
Allah akasema tena: “...BILA SHAKA WAO WALIKUWA WEPESI WA KUFANYA WEMA, NA
WAKITUOMBA KWA SHAUKU (ya kupata pepo) NA KHOFU (ya moto). NAO
WALIKUWA WAKITUNYENYEKEA”. [21:90]
Allah anazidi kutuambia: “HAKIKA WALE WALIOAMINI NA WALE
WALIOHAJIRI (wakahama kuja Madinah) NA WAKAPIGANIA NJIA YA ALLAH, HAO
NDIO WANAOTUMAI REHEMA YA ALLAH. NA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE
(na) MWINGI WA KUREHEMU”. [2:218]
Allah akasema tena: “NA HAO AMBAO WANATOA (zaka na sadaka katika mali)
WALIYOPEWA, NA HALI NYOYO ZAO ZINAOGOPA KWA KUWA WATAREJEA KWA MOLA
WAO”. [23:60]
Bibi Aysha (mama wa waumini)-Allah amuwiye radhi-alisema: Ewe Mtume wa Allah
[HAO AMBAO WANATOA (zaka na sadaka katika mali) WALIYOPEWA NA HALI NYOYO
ZAO ZINAOGOPA] ni yule ambaye anayeiba, anazini na anakunywa pombe na
ilhali anamuogopa Allah Mtukufu? (Mtume) akasema: “Hapana ewe Bint ya
Abu Bakri, ewe Bint Swidiq, lakini huyo (akusudiwaye na aya) ni yule
ambaye anayeswali, akafunga na akatoa sadaka na ilhali anamuogopa Allah
Mtukufu”. Ahmad, Tirmidhiy & Ibn Abiy Haatim-Allah awarehemu.
Fahamu na ujue ewe ndugu yangu kwamba khofu ni kikatazi na kikemezi
kinachomkataza mwanadamu na kumkemea na maasi. Na matumaini ni kiongozi
anayeshika hatamu za kumuongoza mja kuelekea katika mambo ya twaa. Kwa
mantiki hii basi, mtu ambaye khofu yake haimkatazi maasi na wala matumaini
yake hayamuongozei katika twaa. Khofu na matumaini yake haya ni hadithi ya
moyo isiyopewa uzito wala mazingatio. Kutokupewa uzito huko na kule
kutokuzingatiwa kunatokana na khofu na matumaini hayo kukosa matunda
yaliyokusudiwa na faida itakiwayo. Baadhi ya watu wamekuwa na fahamu
lemavu kuelekea maana/dhana ya kuwa na matumaini kwa Allah. Wakadhania
kwamba maana yake ni kuhalalisha kutenda maasi na kuendelea nayo kwa
kutegemea ukunjufu wa rehema za Allah. Hawa wakaangamia na wataangamia
bila ya kukusudia. Wengi miongoni mwa watu wa tabaka la kawaida
wametumbukia katika utumwa wa fikra lemavu hizi, wakaghurika. Matuamini
yaliyo chini ya mwavuli huu mbovu, haya ni matumaini ya uongo nako ni
kudanganyika na kujidanganya na si vinginevyo. Wala haya sio yale
matumaini mema anayopaswa kuwa nayo kila muumini. Matumaini mema ni yale
yanayomuongoza mja kumtii Mola Muumba wake katika yote; maamrisho na
makatazo yake na kumpitisha njia airidhiayo Allah.
Ewe ndugu yangu-Allah akuhidi-tahadhari kufanya maasi huku ukitarajia
kufunikwa na rehema za Mola wako, hiyo ni ghururi akupandikiziayo shetani
mlaaniwa na ni shari aliyokuletea katika sura na umbo la kheri. Kisha
tahadhari tena tahadhari kweli kujiaminisha na adhabu ya Allah na kukata
tamaa na rehema zake. Hebu na tuizingatie kwa pamoja kauli tukufu ya Allah
Mola Mtukufu: “JE, WAMEAMINISHA KUADHIBIWA NA ALLAH? HAWAAMINISHI ADHABU
YA ALLAH ILA WATU AMBAO (watakuwa) WENYE KHASARA”. [7:99]
Al-Hassan Al-Biswriy-Allah amrehemu-amesema: “Muumini hufanya mambo ya
twaa na ilhali ana khofu na uoga (na adhabu ya Allah). Na faajiri (mtu
muovu) hufanya maasi ilhali akijiaminisha (na adhabu ya Allah)”.
Allah
akasema tena: “AKASEMA: NA NANI ANAYEKATA TAMAA YA REHEMA YA MOLA WAKE
ISIPOKUWA WALE WALIOPOTEA?” [15:56]
Pengine ndugu yangu utataka kuniuliza nini maana ya kujiaminisha na adhabu
ya Allah na kukata tamaa na rehema ya Allah. Ikiwa hivyo ndivyo, haya
naomba unitegee sikio lako nikujuze. Tunaposema kujiaminisha na adhabu ya
Allah tunakusudia kuwa na matumaini matupu yasiyoshehenezwa na amali
njema. Na kutokuwa na khofu ya Allah kabisa kiasi cha kuamini kwamba
hakujuzu kwa Allah kumuadhibu kwa hayo maovu ayatendayo. Ama kukata tamaa
na rehema ya Allah ni kuwa na khofu tupu isiyosuhubiana na amali njema. Na
kutokuwa na matumaini kwa Allah kiasi cha kuamini kwamba hakujuzu kwa
Allah kumrehemu na kumsamehe. Hiyo ndiyo maana sahali ya ibara mbili hizo,
elewa ufahamu.
Kujiaminisha na adhabu ya Allah na kukata tamaa na rehema yake ni miongoni
mwa madhambi makubwa, tahadhari na mawili haya ewe ndugu yangu uiokoe
nafsi yako na hilaki. Kuwa baina ya khofu na matumaini na usighurike kwa
Mola wako na wala usijijasirishe mbele yake kwani: “...HAKIKA MOLA WAKO
NI MWEPESI WA KUADHIBU NA HAKIKA YEYE NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA
KUREHEMU (kwa wale wanaorejea kwake)”. [6:165]
Mpenzi ndugu yangu-Allah atusitiri-hebu na tukamilishe huku kuusiana kwetu
mema na kukatazana maovu, kwa kuzizingatia kauli hizi za Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie:-
ü
“Lau muumini
angelijua adhabu iliyoko kwa Allah asingeliitumai pepo yake ye yote. Na
lau kafiri angeliijua rehema iliyoko kwa Allah asingekata tamaa ya pepo ye
yote”. Ahmad-Allah amrehemu.
ü
“Allah
ameumba rehema mia moja, akaiweka rehema moja (tu) baina ya viumbe wake
warehemeane kwayo. Na tisini na tisa (zilizobaki) ziko kwa Allah”.
Tirmidhiy-Allah amrehemu.
|