|
WASIA
WA TISA-KITHIRISHA KULETA ISTIGHFAARI.
Ndugu
yangu mpenzi katika imani-Allah akuongoze-karibu tena katika jukwaa lako
hili la wasia maridhawa kwa kila muislamu. Ninakuusia bila ya kusahau
kuiusia nafsi yangu kuleta istighfaari. Elewa na ufahamu kwamba, katika
jumla ya mambo muhimu yaliyokokotezwa kwa kila muislamu ni kukithirisha
kuleta istighfaari. Istighfaari ni agizo na amri ya Allah Mola Mkamilifu
kwa waja wake viumbe dhaifu wakosaji. Hii ndio amri ya istighfaari ndani
ya Qur-ani Tukufu, haya na tuamrike: “…NA OMBENI MAGHFIRA (msamaha)
KWA ALLAH; HAKIKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU”.
[73:20]
Allah
Mola Mwenyezi akamwambia Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie: “…NA
OMBA MAGHUFIRA KWA DHAMBI ZAKO NA (dhambi) ZA WAUMINI WANAUME NA WAUMINI
WANAWAKE…” [47:19]
Allah
Mola atoaye msamaha pindi mja anapokiri udhaifu wake na kurejea kwake,
anasema katika kutaja wasifu wa waja wake wema wenye kuswali: “NA
WAKIOMBA MAGHUFIRA NYAKATI ZA KABLA YA ALFAJIRI”. [51:18] Nae
Mfasiri Mkuu wa Qur-ani kwa kauli na amali (vitendo)-Rehama na Amani
zimshukie-anasema kuhusiana na suala zima la istighfari. Haya na tumtegee
sikio la usikivu wa kutii na kufuata: “Ye yote atakayelazimikiana na
istighfari, Allah atampa faraja kwa kila huzuni. Na (atampa)
njia ya kutokea katika kila dhiki na atamruzuku kwa namna
asiyoitazamia”. Abuu Daawoud, Nasaai, Ibn Maajah &
Al-Haakim-Allah awarehemu.
Bwana
Mtume anazidi kutuasa katika uwanja huu wa istighfaari, nasi tusichoke
kumsikiliza kwa faida na maslahi yetu wenyewe: “Furaha iliyoje kwa
yule atakayekuta katika daftari lake la amali istighfaari nyingi”.
Ibn Maajah, Twabaraaniy & Al-Baihaqiy-Allah awarehemu.
Ewe
ndugu yangu-Allah atuwafikishe na istighfaari-ikutoshe katika kujua
fadhila, manufaa na faida za istighfaari, kauli hii ya Allah Mtukufu: “...WALA
ALLAH HAKUWA WA KUWAADHIBU HALI YA KUWA WANAOMBA MSAMAHA (Istighfaari)”.
[8:33]
Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuambia: “Kwa yakini shetani
alisema: Naapa kwa utukufu wako, ewe Mola wangu! Nitaendelea kuwapoteza
waja wako maadam roho zao zimo viwiliwilini mwao (wako hai). Mwenyezi
Mungu akamwambia: Nami naapa kwa enzi na utukufu wangu sitaacha
kuwaghufiria (madhambi yao) maadam wananiomba maghufira”. Ahmad
& Al-Haakim-Allah awarehemu.
Ndugu
yangu hebu na tuipe nafasi Qur-ani Tukufu iliyo muongozo na katiba yetu.
Itusimulie juu ya ahadi hii aliyoichukua Iblisi baada ya kufukuzwa peponi
na kubaidishwa (kutengwa) na rehema za Allah Mwingi wa rehema: “AKASEMA:
MOLA WANGU! KWA SABABU UMENIHUKUMU KUPOTEA, BASI NITAWAPAMBIA (viumbe wako
upotofu) KATIKA ARDHI NA NITAWAPOTEZA WOTE. ISIPOKUWA WALE WAJA WAKO
WALIOSAFIKA KWELI KWELI. (Allah) AKASEMA: HII NJIA YAO YA (kuja) KWANGU
IMENYOOKA (wanaweza kunijia wakati watakao). HAKIKA WAJA WANGU, WEWE
HUTAKUWA NA MAMLAKA JUU YAO, ISIPOKUWA WALE WENYE KUKUFUATA (kwa khiari
zao) KATIKA HAO WAPOTOFU. NA BILA SHAKA JAHANAMU NDIPO MAHALA PAO
WALIPOAHIDIWA WOTE”. [15:39-43]
Ewe
ndugu yangu hiyo ndio ahadi iliyochukuliwa na adui yetu mkuu Iblisi
mlaaniwa mbele ya Allah Mola wake na Mola wetu. Hatutasalimika na shari ya
muovu huyu ila kwa kujifunika mwavuli wa waja wa Allah waliosafika kweli
kweli. Kwani hawa Iblisi anakiri udhaifu wake mbele yao kwamba hana hila
wala ujanja wa kuwapoteza. Hao ndio waja wa Allah ambao Iblisi hana
mamlaka juu yao. Najua bila ya shaka kwamba sasa utakuwa unajiuliza ni
kina nani hao waja wa Allah ambao Iblisi hana ubavu juu yao? Naam, usipate
taabu Qur-ani Tukufu ilijua utauliza swali hilo, kwa hivyo ikakutayarishia
jawabu tosha, haya na tuisikilize: “NA
WAJA WA RAHMAAN (Allah Mola Mwenye rehema, anaowapenda ni wenye sifa
hizi):-
v
NI
WALE WANAOKWENDA (na kurejea) ULIMWENGUNI KWA UNYENYEKEVU, NA WAJINGA
WAKISEMA NAO (maneno mabaya) HUWAJIBU (maneno ya) SALAMA.
v
NA
WALE WANAOPITISHA BAADHI YA SAA ZA USIKU KWA AJILI YA MOLA WAO KWA
KUSUJUDU NA KUSIMAMA.
v
NA
WALE WANAOSEMA: MOLA WETU! TUONDOLEE ADHABU YA JAHANAMU, BILA SHAKA ADHABU
YAKE NI YENYE KUENDELEA. HAKIKA HIYO (Jahanamu) NI KITUO KIBAYA NA MAHALI
(pabaya kabisa) PA KUKAA.
v
NA
WALE AMBAO WANAPOTUMIA HAWATUMII KWA FUJO WALA HAWAFANYI UBAKHILI, BALI
WANAKUWA KATIKATI BAINA YA HAYO.
v
NA
WALE WASIOMUOMBA MUNGU MWINGINE PAMOJA NA ALLAH, WALA HAWAUI NAFSI
ALIYOIHARIMISHA ALLAH ISIPOKUWA KWA HAKI. WALA HAWAZINI, NA ATAKAYEFANYA
HAYO ATAPATA MADHARA (papa hapa ulimwenguni kabla ya Akhera).
v
NA
WALE AMBAO HAWASHUHUDII SHAHADA ZA UWONGO, NA WANAPOPITA PENYE UPUUZI,
HUPITA KWA HISHIMA (yao).
v
NA
WALE AMBAO WANAPOKUMBUSHWA AYA ZA MOLA WAO HAWAZIANGUKII KWA UZIWI NA
UPOFU,
v
NA
WALE WANAOSEMA: MOLA WETU! TUPE KATIKA WAKE ZETU NA WATOTO WETU
YABURUDISHAYO MACHO (yetu, nyoyo zetu) NA UTUJAALIE KUWA WAONGOZI KWA
WAMCHAO (Allah)”.
[25:63-68 & 73-74]
Haya
mpenzi ndugu yangu-Allah akuhidi-tayari Qur-ani imetimiza jukumu lake
kwako, tayari imekutajia sifa za waja wa Allah ambao Iblisi hajasiri
kuwakaribia. Sasa ni zamu yako, jipinde ujivishe sifa hizo ili uwe na
kinga dhidi ya kirusi hatari Iblisi.
Naam,
tulikuwa tukielezea fadhila, manufaa na faida za istighfaari, haya na
tuendelee. Kauli hii ya Allah akitupa khabari za Mtume wake Nuhu-Amani
imshukie-inayaeleza bayana hayo (fadhila, manufaa na faida za
istighfaari), tuisikilize: “NIKAWAAMBIA: OMBENI MAGHUFIRA KWA MOLA
WENU. HAKIKA YEYE NI MWINGI WA MAGHUFIRA (msamaha). ATAKULETEENI MAWINGU
YANYESHAYO MVUA NYINGI. NA ATAKUPENI MALI NA WATOTO, NA ATAKUPENI
MABUSTANI NA ATAKUFANYIENI MITO”. [71:10-12]
Ewe
ndugu yangu-Allah akurehemu-elewa na ufahamu kwamba toba na istighfaari ni
katika jumla ya khazina za kheri. Na ni miongoni mwa milango ya Quruba
(sababu za kuwasogeza waja kwa Allah) na baraka na ni asili ya njia zote
za kufikilia kheri za dunia na akhera. Basi ni wajibu wetu kulazimikiana
na toba na istighfaari nyakati za mchana na usiku. Allah atuwafikishe
kukithirisha kumtaka maghufira kwa madhambi tuyafanyayo usiku na mchana,
kwa siri na kwa dhahiri, kwa makusudi na kwa bahati mbaya-Aaamiyn!
|