|
H/.
TUBIA KWA MOLA WAKO TOBA YA KWELI.
Ewe
mpenzi ndugu yangu-Allah atuwafikishe kupendana kwa ajili yake tu-Aamin.
Ninakuusia kwa mapenzi ya imani ufahamu kwamba kuna mambo mengi yenye
kuokoa ambayo ni wajibu kuupamba moyo wako kwa mambo hayo. Kwa msaada wa
Allah ninakutajia baadhi ya mambo hayo yaliyo muhimu kabisa. Ewe ndugu
yangu, ninakunasihi utambue kwamba mama wa mambo yenye kuokoa ni kutubia
kwa Allah kutokana na madhambi yote. Fahamu kutaka toba ni amri ya
Allah kwa waja wake walio dhaifu na wasioepuka kufanya dhambi. Allah
amewaraghibisha waja wake kufanya toba kutokana na madhambi wayafanyayo na
akawaahidi kuwapokelea toba yao. Akasema Allah Mola Mwenyezi: “...NA
NYOTE TUBIENI KWA ALLAH, ENYI WAUMINI ILI MPATE KUFAULU”. [24:31]
Akasema
tena: “ENYI MLIOAMINI! TUBUNI KWA ALLAH TOBA ILIYO YA KWELI, HUENDA
MOLA WENU AKAKUFUTIENI MAOVU YENU NA KUKUINGIZENI KATIKA PEPO ZIPITAZO
MITO MBELE YAKE...” [66:8] Akasema tena: “...HAKIKA ALLAH HUWAPENDA
WANAOTUBU NA HUWAPENDA WANAOJITAKASA” [2:222]
Akaongeza kusema: “LAKINI MWENYE KUTUBIA BAADA YA DHULMA YAKE
NA AKATENDA WEMA, BASI ALLAH ATAPOKEA TOBA YAKE. HAKIKA ALLAH NI MWINGI
WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU” [5:39] Akazidi kusema: “NAYE
NDIYE ANAYEPOKEA TOBA ZA WAJA WAKE NA ANASAMEHE MAKOSA NA ANAYAJUA YOTE
MNAYOYATENDA” [42:25]
Naye
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema kuhusiana na suala zima la
toba, tumsikilize: “Mwenye kutubia kutokana na dhambi aliyoifanya ni
kama mtu asiye na dhambi”. Ibn Maajah, Twabaraaniy &
Al-Baihaqiy-Allah awarehemu.
Bwana
Mtume akazidi kutuambia: “Hakika Allah huukunjua mkono wake wakati wa
mchana ili apate kutubia mkosa wa usiku. Na huukunjua mkono wake wakati wa
usiku ili apate kutubia mkosa wa
mchana (hufanya hivyo) mpaka litakapochomoza jua kutokea machweo (mazamio)
yake”. Muslim-Allah amrehemu
Na
akasema tena Bwana Mtume: “Enyi watu! Tubieni kwa Mola wenu kabla
hamjafa na harakieni kufanya amali njema kabla hamjashughulishwa. Na
yaungeni mawasiliano yenu na Mola wenu kwa kukithirisha kumkumbuka
kwenu”. Ibn Maajah-Allah amrehemu.
Akaongeza
kusema: “Kwa yakini Allah hukubali toba ya mja (wake) maadam roho
yake haijafika kooni”. Tirmidhiy & Ibn Maajah-Allah awarehemu.
Na
akatuambia: “Allah huipokea toba ya anayetubia”. Ahmad,
Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
SHARTI
ZA TOBA.
Ewe
ndugu yangu-Allah akurehemu-fahamu kuwa kufanya toba ni ibada ambayo
kusihi kwake kunaambatana na sharti kadhaa. Kisha ni vema ukafahamu kwamba
toba kamili; toba ya kweli si maneno matupu ya ulimini. Mtu akasema:
(ASTAGHFIRULLAAH WA ATUUBU ILAYHI) ulimini, bila ya majuto ya moyo wala
kujivua na madhambi. Wanazuoni wetu wema-Allah awarehemu-wametaja sharti
ambazo toba ya mja haitatimia ila kwa kuzileta sharti hizo. Sharti hizo ni
tatu kama zifuatazo:-
- Majuto
ya moyo: Mja
ajute moyoni mwake kutokana na madhambi aliyoyatenda huko nyuma.
- Kujivua
na madhambi: Mja
anapoamua kutubia, basi kumemuwajibikia kujivua na kuyaacha kabisa
madhambi anayoyatakia toba. Haiingii akilini kutaka toba huku
ukiendelea na maasi bila ya kuyaacha, huku ni kumdhihaki Allah.
- Kuazimia
kutorejea madhambini baada ya kutubia: Mja
aamue kwa kutinda kuwa hatarudia tena kumuasi Mola wake kwa kufanya
yale yote aliyoyakataza.
Ndugu
yangu muislamu mja mwenye madhambi kama mimi, hizi ndizo sharti ambazo
toba ya mja haikamiliki wala kusihi ila kwa kupatikana kwake zikiwa
kamili; bila ya mapungufu yo yote. Sharti hizi si maneno matupu tu ya
wanachuoni bali zinatokana na kauli za Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie: “Toba iliyo ya kweli ni kujutia dhambi
inapokupindukia, kisha ukamuomba Allah maghfira halafu usiirejee
tena (dhambi hiyo)”. Ibn Abiy Haatim & Ibn Murdawayhi-Allah
awarehemu.
Ewe
ndugu yangu-Allah akuhidi-fahamu na ujue kwamba sharti tatu hizi ndizo
sharti za kusihi toba ya madhambi baina ya mja na Mola Muumba wake tu.
Madhambi ambayo hamna ndani yake haki ya mwanadamu mithili ya mtu kuacha
swala. Ama madhambi ambayo pamoja na kumuasi Allah ndani yake kuna haki ya
mwanadamu, pamoja na sharti tatu hizi inaongezeka
sharti ya nne. Nayo sharti hii ni kurejesha haki ya watu
aliyoidhulumu kama ni mali au ni haki ya heshima. Akishindwa kurejesha
basi akamtake radhi mwenyewe ambaye atakuwa na khiari ya ama kumsamehe au
kutokumsamehe. Mja akishatubia kwa namna hii tuliyoibainisha,
linaloandamia kwake ni kuwa katika hali baina ya khofu na matarajio.
Akitarajia kukubaliwa toba yake kwa fadhila na ukarimu wa Mola wake. Huku
akikhofu kuwa huenda Mola waku hakuikubali na kuipokea toba yake kwa
sababu hakutubia kama Allah alivyoamrisha na kuelekeza kupitia kwa Mtume
wake.
Ewe
mpenzi ndugu yangu-Allah atuwafikishe kufanya toba ya kweli kweli-nakuusia
uelewe kwamba ni wajibu wa muumini kujiepusha kabisa na madhambi yote.
Muumini wa kweli hujiepusha na madhambi bila ya kuangalia ukubwa au udogo
wake. Anafanya hivyo kwa kutambua na kuukiri kwake ukweli kwamba ndani ya
kutenda dhambi kuna ghadhabu, hasira na machukivu ya Allah Mola Muumba
wake. Allah akurehemu ikiwa utafahamu kwamba madhambi ndiyo sababu kuu ya
majanga na balaa ziwapatazo waja duniani na akhera: “FISADI
(uharibifu) UMEDHIHIRI BARANI NA BAHARINI KWA SABABU YA YALE
ILIYOYAFANYA MIKONO YA WATU, ILI AWAONJESHE (adhabu ya) BAADHI YA
MAMBO WALIYOYAFANYA, HUENDA WAKARUDI (wakatubia kwa Allah)”. [30:41]
Muumini
akiteleza akatenda dhambi, basi kunamuwajibikia kuharakia kufanya toba
bila ya kuendelea nayo dhambi hiyo na wala asiiridhie. Kunampasa muumini
kutubia na kuendelea kuijadidisha toba yake kwa Mola wake kila wakati. Hii
ni kwa sababu madhambi ni mengi mno; madhambi makubwa na madogo, madhambi
ya dhahiri na ya siri. Madhambi ayajuayo mja na yale asiyoyajua. Haya
ndugu yangu na tutubie kabla hatujafikwa na mauti.
|