|
G/.
JIEPUSHE NA GHURURI (kutoka
darsa iliyopita)
Ewe
ndugu yangu Allah-akuongoze katika kuyafuata ayaridhiayo na kuyapenda.
Naam, sasa naomba uniazime fikra, moyo na usikivu wako nikupigie mifano ya
ghururi kwa janibu ya watu
maasi. Kukosea na kufanya madhambi iwe ni kwa bahati mbaya au kwa makusudi
ni sehemu ya maumbile ya mwanadamu, hili halipingiki. Sasa basi mtu
anapoasi kisha akatubu na kumuomba maghfira Mola wake kwa ulimi tu, bila
ya kujua sharti za toba na uhakika wake. Kisha kwa huku kutamka kwake:
“ASTAGHFIRULLAH” kwa ulimi tu, akadhania na kuitakidi kabisa kwamba
amekwishatubia na Allah amemghufiria. Huyu ni maghururi na hicho
akifanyacho ni ghururi tu.
Hii
nayo ni ghururi, mtu kukithirisha kufanya maasi na akaendelea na maovu
hayo huku akizembea kutekeleza wajibu wake katika twaa. Halafu akawa
anajihalalishia uovu wake huo kwa hoja kwamba hiyo ndiyo ‘Qadari’ ya
Allah kwake. Na kwamba yeye hana khiyari ya kutenda ama kutokutenda, kwani
yote ayatendayo au kuacha kuyatenda ameandikiwa na Allah Mola Muumba wake.
Katika aina zote za ghururi hii ndio kubwa yao na mwenye kuifuata ghururi
hii ni mzushi na si vinginevyo.
Kadhalika
miongoni mwa ghururi kwa janibu hii ya watu maasi ni mtu kuwa na matumaini
ya kupata maghfira huku akizembea kutekeleza maamrisho na kujiepusha ma
maharimisho. Baadhi ya watu maasi wasiofanya ibada hupata kusema: (Hakika
Allah hana haja nasi wala amali zetu, madhambi yetu hayamdhuru wala twaa
zetu hazimnufaishi). Maneno yao haya ni haki iliyolengwa batili ambayo
shetani ameitia moyoni mwa huyu maghururi. Kisha akayapitisha ulimini
kwake ili apate kumkata na kumtenga na maghfira na aache kuyahangaikia,
jambo ambalo ni amri ya Mola wake. Hii nayo haipungui kwa cho chote katika
mizani ya ghururi.
Ndugu
yangu katika imani-Allah aithubutishe imani yako-nakusihi uendelee
kunitegea sikio katika mifano hii hai ya ghururi ili uepuke kutumbukia
humo kwa msaada wa Allah. Utawaona baadhi ya watu wakibweteka kufanya
amali njema zitakazowanufaisha mbele ya Allah, wakijinasibisha na
kutegemea wema na uongofu wa baba zao. Wanafanya hivyo bila ya kuwaiga
katika mazuri yao hayo waliyoyafanya, hii ni ghururi mbaya na isitoshe ni
upumbavu muovu. Ingelikuwa wema na uongofu wa wazee unawafaa watoto wao
bila ya wao kushirikiana nao katika wema na uongofu huo. Basi
mwanawe Nabii Nuhu-Amani imshukie-angelinufaika na utume na amali za baba
yake, lakini ilikuwaje, hii hapa Qur-ani Tukufu itegee sikio mwenyewe:
“NA NUHU ALIMUOMBA MOLA WAKE (alipomuona mwanawe anaangamia) AKASEMA:
EWE MOLA WANGU! MWANANGU NI KATIKA WATU WA NYUMBANI KWANGU (mbona
anaangamia)? NA HAKIKA AHADI YAKO NI HAKI, NAWE NI MWENYE HAKI KULIKO
MAHAKIMU (wote). AKASEMA (Allah): EWE NUHU! HUYU SI MIONGONI MWA WATU
WAKO. YEYE NI (mwenye) MWENDO USIOKUWA MZURI. BASI USINIOMBE AMBAYO
HUYAJUI. MIMI NAKUNASIHI USIWE MIONGONI MWA WAJINGA” [11:45-46]
Utaona
kwa mujibu wa aya kwamba wema wa mzazi bila ya wewe mwenyewe kuwa mwema
hautakunufaisha kwa cho chote mbele ya Allah ila kama utamfuata kwenye
wema huo. Hivi ndivyo isemavyo Qur-ani: “NA WALE WALIOAMINI NA
WAKAFUATWA NA VIZAZI VYAO NA WATOTO WAO KATIKA IMANI. TUTAWAKUTANISHA
NAO HAO JAMAA ZAO, WALA HATUTAWAPUNJA KITU KATIKA (thawabu za) VITENDO
VYAO, KILA MTU ATALIPWA KWA KILE ALICHOKICHUMA”. [52:21]
Hii
nayo haiachi kuwa ni aina ya ghururi, mtu kukutana na waja wema,
akawatumikia kwa dhana njema kabisa. Lakini akajiepusha na kujitenga na
mwendo wao mwema na kulazimikiana kwao na twaa ya Allah. Kisha akataraji
kwa kuwatumikia tu mabwana hawa bila ya kuwaiga katika mema yao ataipata
tu pepo ya Allah kwa baraka zao. Hii ni ghururi na wazimu mtupu tu.
Aina
za ghururi ni nyingi mno kuliko tulivyowafikiwa kuzitaja na wala mja
hataokoka na ghururi hizi ila ni kwa kurejea kwa Allah na kutegemea
fadhila na ukarimu wake. Kurejea huko kuwe ni pamoja na kutinda na kupania
katika kumtii na kujitahidi katika kumuabudu. Yote haya yaende sambamba na
kujiepusha pamoja na kujitenga na maasi na kumshukuru kwa kukuwezesha kuwa
katika twaa yake. Huku ukidumisha unyenyekevu, dua na istighfari mchana na
usiku.
|