|
WASIA
WA TANO – USIPENDE CHEO NA MALI.
Ewe
ndugu yangu mpenzi katika imani-Allah akurehemu-ninakuusia bila ya
kuisahau nafsi yangu kwamba usipende mali na cheo. Fahamu na uelewe kwamba
kupenda cheo na mali ni miongoni mwa majanga makubwa ikiwa havikutimiziwa
haki yake. Kwani cheo na mali ni amana na dhima iliyo mabegani mwako.
Kutokana na uzito wa amana hii na ukubwa wa majukumu yake, ndio kukawa
kupenda mno mali na cheo ni jambo lililokaripiwa na kukemewa sana. Allah
Mola Mwenyezi anatuambia: “HIYO NYUMBA YA AKHERA TUTAWAFANYIA WALE
WASIOTAKA KUJITUKUZA (cheo) KATIKA ARDHI WALA (kufanya) UFISADI, NA MWISHO
(mwema) UTAWATHUBUTIKIA WACHA-MUNGU”. [28:23] Mola wetu akazidi
kutuambia: “ENYI MLIOAMINI! YASIKUSAHAULISHENI MALI YENU WALA WATOTO
WENU KUMKUMBUKA ALLAH. NA WAFANYAO HAYO, HAO NDIO WENYE KUKHASIRIKA”.
[63:9]
Akatuambia
tena: “BILA SHAKA MALI ZENU NA WATOTO WENU NI JARIBIO (kwenu, mtihani
kutazama mtakhalifu amri za Allah kwa ajili yao au mtafuata amri zake). NA
KWA ALLAH KUNA UJIRA MKUBWA KABISA”. [64:15]
Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anatuasa juu ya suala zima la kupenda mno
mali na cheo, anasema: “Hawakuwa mbwa mwitu wawili wenye njaa
walioachiwa katika kundi (zizi) la mbuzi na kondoo. Ni wenye kufanya
fisadi (uharibifu) mkubwa zaidi katika kundi hilo kuliko fisadi ya
kupenda mali na utukufu (ukubwa/cheo) katika dini ya mtu muislamu”.
Maana ya kauli hii ya Mtume wa Allah ni kwamba mapenzi ya mali
na cheo. Yanaifisidi na kuiharibu dini ya mwenye vitu hivyo zaidi kuliko
fisadi inayoweza kufanywa na mbwa mwitu wenye njaa kali katika kundi la
wanambuzi na kondoo. Kwa hivyo, elewa na ufahamu ewe ndugu yangu ya kwamba
mtu atakayepupia mno kupenda cheo na kutafuta utukufu na ukubwa katika
nyoyo za watu. Huyu kwa mwenendo na tabia yake hii huwa amejitia mwenyewe
majangani. Hawezi kuyaepa maafa ya jeuri/kibri kitokanacho na mali, ria
(kujiona na kujigamba), kujipamba na sifa asizokuwa nazo na kuacha
kuinyenyekea haki na wenye haki. Na mithili ya haya miongoni mwa mabalaa
mengineyo.
Jua
ewe ndugu yangu kwamba muislamu kama mwanadamu mwingine ye yote hakatazwi
kuwa na mali au cheo au kujijenga kimaisha, dhana hii si sehemu ya
mafundisho sahihi ya Uislamu. Sasa basi, ikiwa hivi ndivyo ni kwa nini
basi mali na cheo vikashtumiwa na kusemwa sana katika Uislamu? Ikiwa hili
ndilo swali linaloweza kuzigubika fikra na mawazo yako, basi ninakuambia
na kukuomba unitegee sikio la usikivu. Ninasema kinachoshtumiwa na
kukaripiwa ni kuipenda mali au cheo kupindukia, kiasi cha kumfanya mtu
kuvitafuta kwa gharama na njia yo yote ile. Iwe ni kwa kumtoa mwanadamu
mwenziwe kafara, kudhulumu au kunyang’anya, yote haya mtu yu tayari
kuyafanya muradi tu apate cheo au mali. Cheo na mali hii vikamuweka mbali
na Allah jambo ambalo ndilo lengo mama la kuumbwa kwake na kuletwa katika
ulimwengu huu. Hawa ndio watu wanaoambiwa na Allah: “KUMEKUGHAFILISHENI
KUTAFUTA WINGI (wa mali, jaha {cheo} na watoto na kujifakharisha kwa
hayo). HATA MUMEINGIA MAKABURINI (mumekufa kabla ya kufanya kheri yo
yote). SIVYO HIVYO! KARIBUNI HIVI MTAJUA (kuwa sivyo hivyo). KISHA
(nasema) SIVYO HIVYO! KARIBUNI HIVI MTAJUA (kuwa sivyo hivyo). SIVYO
HIVYO! LAU KAMA MNAJUA UJUZI WA YAKINI (kuwa sivyo hivyo msingefanya
hivyo). HAKIKA MTAUONA MOTO. KISHA (nasema) MTAUONA KWA YAKINI (moto).
KISHA KWA HAKIKA MTAULIZWA SIKU HIYO JUU YA NEEMA (mlizopewa
mlizitumiaje”. [102:1-8]
Ni
ukweli usiopingika kwamba wengi miongoni mwa wenye mali na vyeo wako mbali
kabisa na Allah Mola Muumba wao, hawana khabari nae hata kidogo. Na kwa
wanadamu wenziwao wamejawa na viburi, dharau na udhalilishaji ila wale
ambao Allah amewafunika na rehema zake. Hii ndio mali na hicho ndicho cheo
kinachosemwa vibaya na kukaripiwa na Uislamu, fahamu na elewa hivi. Ama
mtu atakayetafuta cheo au mali kwa nia njema tu, akaitaka mali ili
imsaidie kuipata akhera kutokana na kuitumia kwake katika mambo ya kheri
na wema. Kwa ajili ya kuilinda dini na nafsi yake dhidi ya uadui wa
madhalimu na kwa ajili ya kuwasaidia watu. Na mali hiyo ikamfanya
asimsahau Mola wake, bali ikazidi kumsogeza karibu nae kwa kumuabudu na
kumshukuru kwa neema alizomneemesha. Mali kama hii si vibaya wala dhambi
mtu kuimiliki huku akitambua kuwa mali hiyo ni mtihani kwake na hesabu
yake kesho mbele ya Mola wake ni nzito na ngumu: “MALI NA WATOTO NI
PAMBO LA MAISHA YA DUNIA. NA VITENDO VIZURI VIBAKIAVYO NDIVYO BORA
MBELE YA MOLA WAKO KWA MALIPO NA TUMAINI BORA (kuliko hayo mali na
watoto”. [18:46]
Huku
akijikumbusha na mtihani wa mali uliompata Qaarun na mwisho wake
ulivyokuwa kama inavyosimulia Qur-ani Tukufu na tuitegee sikio la
kuwaidhika: “HAKIKA QAARUN ALIKUWA KATIKA WATU WA MUSA, LAKINI
ALIWAFANYIA DHULMA. NA TULIMPA KHAZINA AMBAZO FUNGUO ZAKE ZINAWATOPEZA
WATU WENYE NGUVU (kuzichukua). WALIMWAMBIA WATU WAKE: USIJIONE
(usijigambe) HAKIKA ALLAH HAWAPENDI WANAOJIONA. NA UTAFUTE KWA YALE
ALIYOKUPA ALLAH MAKAZI MAZURI YA AKHERA, WALA USISAHAU SEHEMU YAKO YA
DUNIA, NA UFANYE WEMA KAMA ALLAH ALIVYOKUFANYIA, WALA USITAFUTE KUFANYA
UFISADI KATIKA NCHI, BILA SHAKA ALLAH HAWAPENDI MAFISADI. AKASEMA:
HAKIKA NIMEPEWA HAYA KWA SABABU YA ILIMU NILIYONAYO. JE, HAKUJUA KWAMBA
ALLAH AMEWAANGAMIZA KABLA YAKE WATU WALIOKUWA WENYE NGUVU ZAIDI KULIKO
YEYE NA WENYE MKUSANYO MWINGI ZAIDI (wa mali kuliko wake yeye)? NA WABAYA
HAWATAULIZWA MAKOSA YAO (Allah mwenyewe anayajua yote). BASI AKAWATOKEA
WATU WAKE KATIKA PAMBO LAKE. WAKASEMA WALE WANAOTAKA MAISHA YA DUNIA:
LAITI TUNGELIPATA KAMA ALIYOPEWA QAARUN, HAKIKA YEYE NI MWENYE BAHATI
KUBWA. NA WAKASEMA WALE WALIOPEWA ILIMU: OLE WENU! MALIPO YA ALLAH NI
MAZURI KWA YULE ANAYEAMINI NA KUFANYA VITENDO VIZURI (kuliko aliyonayo
huyu Qaarun) WALA HAWATAPEWA HAYO ISIPOKUWA WAFANYAO SUBIRA. BASI
TUKAMDIDIMIZA YEYE (Qaarun) NA NYUMBA YAKE ARDHINI, WALA HAPAKUWA NA KUNDI
LO LOTE LA KUMSAIDIA KINYUME NA ALLAH, WALA HAKUWA MIONGONI MWA WALE
WALIOWEZA KUJISAIDIA. NA WAKAWA WANASEMA WALE WALIOTAMANI CHEO CHAKE
JANA: E-E-E- (kweli) ALLAH HUMZIDISHIA RIZIKI AMTAKAYE MIONGONI MWA WAJA
WAKE (na hali ya kuwa mbaya, hampendi). NA HUDHIKISHA (riziki ya
anayemtaka), ASINGETUFANYIA HISANI ALLAH BILA SHAKA ANGETUDIDIMIZA (kama
alivyomdidimiza kwani sisi tuliitamani hali yake) O! KWELI HAWAFUZU
MAKAFIRI”. [28:76-82]
|