Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Akhlaaq-Tabia  

"Hakika si vingine nimetumwa kuja kutimiza TABIA NJEMA" Hadith Tukufu

WASIA MARIDHAWA KWA KILA MUISLAMU .....I

 

Maana; Wasia ni  neno lenye asili ya lugha ya Kiarabu ni neno ambalo limetumika ndani ya Qur-ani Tukufu, hadithi za mtume na baki ya maandishi mengine ya kiarabu.

Neno hili  kama lilivyotumika ndani ya Qur-ani na Sunah lina maana ya maneno  yenye maadili maonyo yanayolenga :-

Kunasihi/kuamrisha juu ya ama kutenda au  kutokutenda jambo fulani.

Kuadabisha na kutoa muongozo juu ya  suala  zima la maisha.

Kuelekeza, kukosoa na kurekebisha tabia .

 

CHIMBUKO :  Asili na  chimbuko la darsa yetu hii ya wasia ni kauli yake  Allah Mola Mwenyezi ambayo  ni wasia wake kwa walimwengu wote: “...NA KWA YAKINI TULIWAUSIA (amri) WALIOPEWA KITABU KABLA YENU, NA NYINYI (pia) KWAMBA MUMCHE ALLAH (wasia)…” (4:131)

Na inaeleweka wazi kwa kila mmoja wetu kwamba kumcha Allah (Taqwa) ni kujiepusha na makatazo ya Allah na kuyatekeleza maamrisho yake.

LENGO/MADHUMUNI:

     Darsa hizi za wasia zinalenga kumjenga musislamu kiutu na kitabia ili:-

  • Maisha yake yote yatoe taswira ya Uislamu, yaani awe ni Uislamu unaotembea.

  • Awe ni kigezo cha utu na tabia njema katika jamii anayoishi nayo.

  • Afikie daraja ya Ucha–Mungu (Taq-wa) kwa kutenda anayoamrishwa katika wasia na kuacha anayokatazwa.

Mpenzi msomaji wetu, darsa hizi za wasia ambazo ni sehemu ya somo la Akhlaaq zitakujia katika mfululizo utakaokuwa chini ya anuani munasibu.  Ni matarajio yetu makubwa kwamba wasia huu  maridhawa utakunufaisha katika maisha yako binafsi, ya kijamii, ya ulimwengu huu na ule ujao.  Kwa fadhila zake Allah ambaye ndiye aliyetuelekeza katika sula zima la wasia.  Sasa kwa msaada wake Allah tuingie katika darsa zetu hali ya kuwa tunakusudia kujiusia sisi nafsi zetu na wewe msomaji wetu.

 

WASIA WA KWANZA.

a)     KUWA NA HURUMA.

          Muislamu unausiwa na kuhimizwa kujipamba na tabia ya huruma kamili kwa viumbe wote wa Allah; wanadamu wenzio na wasio wanadamu.  Ishi na wanadamu wenzio na changanyika nao kimaisha kwa kuwaonyesha upole na huruma.  Uwe mpole na mwenye huruma hata kwa wale walio maadui zako na wanaokufanyia hasadi katika neema ulizopewa na Mola wako.  Ni wajibu wako kutambua kwamba mwanadamu ikiwa ni pamoja na wewe mwenyewe ni kiumbe dhaifu: “…MWANADAMU AMEUMBWA DHAIFU (hana nguvu kubwa kabisa za kiwiliwili wala nguvu kubwa  za kupigana na moyo na shetani).”  (4:28).  Ukiri udhaifu huu wa mwanadamu ambao ni sehemu ya maumbile yake na umuhurumie. Umuhurumie na umchukulie upole hata adui yako, kwani kwa yakini Allah Mola Mwenye huruma huwaonea huruma waja wake wenye kuwaonea huruma wanadamu wenzao. Hivi ndivyo unavyoambiwa na Mtume wako–Rehema na Amani zimshukie: “Wenye huruma watahurumiwa na Mwingi wa rehema (Allah), wahurumieni walioko ardhini (viumbe wenzenu) atakuoneeni huruma aliyeko  mbinguni (Mola muumba wenu)”. Ahmad, Abuu Daawaud, Tirmidhiy & Al-Haakim

Ni bora na ni kheri kwako ukamuhurumia mwanadamu mwenzio kwa udhaifu wake, kwani kumbuka kwamba asiyehurumia ahurumiwi. Hebu jiulize, je wewe hutaki huruma ya Allah Mola Mwenye huruma? Kama unaitaka, basi itafute huruma hiyo kwa kuwahurumia viumbe wenzio kila unapowapata udhaifu wa kibinadamu. Huruma yako hii isikomelee tu kwa wanadamu wenzio bali iwaenee hata wanyama ambao Allah amewaumba kwa ajili ya manufaa yako.  Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah–Allah amuwiye radhi–kwamba Mtume wa Allah-Rehma na Amani zimshukie amesema: “Wakati ambapo mtu mmoja akienda njiani, kikamshika kiu kikali kabisa akashuka kisimani akanywa maji humo, kisha akatoka (kuendelea na safari yake). Tahamaki huyo mbele yake ni mbwa anahema na kula mchanga kutokana na ukali wa kiu. Akajisemea: Bila ya shaka kimempata (mbwa) huyu kiu kama kilichonipata mimi (hivi punde tu).  Akakijaza maji kiatu chake kisha akakiuma kwa mdomo wake, akapanda (kutoka kisimani mle). Akaja akamnywesha maji mbwa yule, Allah akakishukuru kitendo chake kile cha huruma, akamsamehe dhambi zake kwa sababu hiyo. (Maswahaba) wakauliza: Ewe Mtume wa Allah, hivi sisi tuna ujira kwa (kuwatendea huruma hata) wanyama! Mtume akawajibu: “Katika kila ini bichi (kilicho hai) kuna ujira.”  Bukhaariy

Hebu ndugu muislamu na tuienzi kauli hii ya Mtume wetu–Rehema na Amani zimshukie-kwa kuwaonea huruma wanyama: “Mwenye kukihurumia walau kichinjwa cha ndege, Allah atamuonea huruma siku ya kiyama.” Bukhaariy, Twabaraaniy & Dhwiyaa

Elewa kumuhurumia kiumbe dhaifu mithili ya ndege unayetaka kumchinja kwa ajili ya kitoweo chako si kuacha kumchinja.  Bali ni kutokumtesa au kumchinja kikatili.

 

WASIA WA PILI.

b)     WAEPUSHIE WENGINE SHARI ZAKO:

          Muislamu unausiwa uishi na wanadamu wenzio na ujitahidi upeo wa jitihada zako shari zako zisiwafikie kwa namna yote ile iwayo. Kwani kwa kufanya hivyo, Allah atakukinga na kukulinda na shari na maudhi yao. Tambua kwamba imethibiti kutoka kwa Bwana Mtume– Rehema na Amani zimshukie: “Mwenye kutaka salama, basi na aitafute katika salama ya mwenziwe kutoka kwake.”

Wanuwilie kheri wanadamu wote khususan waislamu na wala usiwadhamirie shari. Wala usimfanyie undani na chuki muislamu mwenzio, bali muislamu mwema ni yule asemaye: “…MOLA WETU! TUSAMEHE SISI NA NDUGU ZETU WALIOTUTANGULIA (kufa) KATIKA USILAMU WALA USIJAALIE KATIKA NYOYO ZETU UNDANI KUWAFANYIA WISLAMU ( wenzetu) MOLA WETU! …”  (59:10)

Ukiwa una sifa hii, huna undani wala mfundo kwa waislamu wenzako utakuwa umejijengea ngome imara dhidi ya shari zao na Allah atakuvika taji la Ucha–Mungu. Kisha ninakuusia tuuzingatie kwa pamoja wasia wa Luqmaan kwa mwanawe kama alivyousajili  Allah ndani ya Qur-ani Tukufu “…EWE MWANANGU! USIMSHIRIKISHE ALLAH, MAANA SHIRKI NDIYO DHULUMA KUBWA.” (31:13) Akaendelea kumuusia: “EWE MWANANGU! KWA HAKIKA JAMBO LO LOTE LIJAPOKUWA NA UZITO WA CHEMBE YA HARDALI, LIKAWA NDANI YA JABALI AU MBINGUNI AU KATIKA ARDHI, ALLAH ATALILETA (amlipe aliyefanya) BILA SHAKA ALLAH NI MJUZI WA MAMBO YALIYOFICHIKANA (na) MJUZI WA MAMBO YALIYO DHAHIRI. EWE MWANANGU! SIMAMISHA SWALA, NA UAMRISHE MEMA NA UKATAZE MABAYA, NA USUBIRI JUU YA YALE YATAYOKUSIBU (kwani mwenye kuamrisha mema na kukataza mabaya lazima zitamfika tu taabu) HAKIKA HAYO NI KATIKA MAMBO YANAYOSTAHIKI KUAZIMIWA (na kila mtu) WALA USIWATAZAME (usiwafanyie watu jeuri) KWA UPANDE MMOJA WA USO, WALA USENDE KATIKA NCHI KWA MARINGO, HAKIKA ALLAH HAMPENDI KILA AJIVUNAE, AJIFAKHIRISHAYE NA USHIKE MWENDO WA KATIKATI, NA UTEREMSHE SAUTI YAKO, BILA SHAKA SAUTI YA PUNDA NI MBAYA KULIKO SAUTI ZOTE (kwa  makelele yake bure)”  (3:16-19)

Ninazidi kukuusia ewe ndugu yangu mpenzi pamoja na kuiusia nafsi yangu ya kwamba tuwe miongoni mwa waja wa Rahmaani–Allah mwingi wa rehema: “….AMBAO WANAOKWENDA (na kurejea) ULIMWENGUNI KWA UNYENYEKEVU, NA WAJINGA WAKISEMA NAO (maneno mabaya) HUWAJIBU (maneno ya) SALAMA NA WALE WANAOPITISHA BAADHI YA SAA ZA USIKU KWA AJILI YA MOLA WAO KWA KUSUJUDU NA KUSIMAMA NA WALE WANOSEMA MOLA WETU! TUONDOLEE ADHABU YA JAHANAMU, BILA SHAKA ADHABU YAKE NI YENYE KUENDELEA NA WALE AMBAO WANAPOTUMIA HAWATIMII KWA FUJO WALA HAWAFANYI UBAKHILI, BALI WANAKUWA KATIKATI BAINA YA HAYO. NA WALE WASIOMUOMBA MUNGU MWINGINE PAMOJA NA ALLAH, WALA HAWAUI NAFSI ALIYOIHARIMISHA ALLHA ISIPOKUWA KWA HAKI, WALA HAWAZINI, NA ATAKAYEFANYA HAYO ATAPATA MADHARA (papa hapa ulimwenguni kabla ya Akhera).” (25:63–68)

Na tuwe katika: “…WALE AMBAO HAWASHUHUDII SHAHADA ZA UWONGO, NA WANAPOPITA PENYE UPUUZI, HUPITA KWA HISHIMA (yao) NA WALE AMBAO WANAPOKUMBUSHWA AYA ZA MOLA WAO HAWAZIANGUKII KWA UZIWI NA UPOFU. NA WALE WANAOSEMA: MAOLA WETU! TUPE KATIKA WAKE ZETU NA WATOTO WETU YABURUDISHAYO MACHO (yetu, nyoyo zetu) NA UTUJAALIE KUWA WAONGOZI KWA WAMCHAO ALLAH”.  (25:72-74)

Ewe ndugu yangu katika imani-Allah akurehemu-elewa na ufahamu kwamba tukiushika wasia huu na tukajipamba na sifa hizi. Basi hapana shaka kwamba tutakuwa ni malaika watembeao katika ardhi na ujira adhimu unatungojea kesho mbele ya Allah: “…HAO (wenye sifa hizo) NDIO WATAKAOLIPWA GHOROFA (za peponi) KWA KUWA WALISUBIRI, NA WATAKUTA HUMO HISHIMA NA AMANI. WAKAE HUMO MILELE, KITUO KIZURI NA MAHALA PAZURI (kabisa) PA KUKAA”. (25:75–76)

Tuusiane na tutambue kuwa gharama na thamani ya kununulia hizo ghorofa za peponi ambazo ni mahala pazuri mno pa kukaa mja ni kuishi katika ulimwengu huu kwa kujipamba na sifa tulizozitaja.  Mola wetu Mtukufu tunamuomba atujaalie kwa fadhila zake kuwa ni miongoni mwa “WAJA WA RAHMAANI” – Aamiyn!

 



Forum | Guestbook | Tuandikie |