Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Akhlaaq-Tabia  

"Hakika si vingine nimetumwa kuja kutimiza TABIA NJEMA" Hadith Tukufu

10. HAKI ZA MAKHADIMU (WATUMISHI WA MAJUMBANI), VIBARUA NA WAAJIRIWA.........Inaendelea

 Faida

3. HAKI YA KUFANYA KAZI KULINGANA NA UWEZO:

Katika jumla ya haki za mtumishi/mfanyakazi ni kuwa kazi anayopewa ilingane na uwezo wake. Kwa maneno mengine mtumishi asikalifishwe kufanya kazi asiyo na uwezo nayo. Hii ni kwa sababu: “ALLAH HAIKALIFISHI NAFSI YO YOTE ILA YALIYO SAWA NA UWEZA WAKE...”. [2:286]

Ikiwa Allah Mola Muumba na Bwana Mlezi mwenye kustahiki kutumikiwa na kuabudiwa na kila kiumbe ukiwemo wewe muajiri, haikalifishi nafsi ila yaliyo katika uweza wake. Ni dhahiri basi, kwamba hakuna mwenye haki ya kumkalifisha mtumishi/muajiriwa kufanya kazi nzito na ngumu asiyoimudu. Au kumkalifisha mtu mmoja kufanya kazi inayohitaji nguvukazi ya zaidi ya mtu mmoja hata kama anamlipa. Huu si Uislamu na wala si ubinadamu kamwe, ni lazima kazi husika iende sambamba na nguvukazi inayohitajika katika kuitekeleza kazi hiyo. Hivi ndivyo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anavyoielezea haki hii: “...Na wala msiwakalifishe (kufanya kazi) wasiyoiweza na iwapo mtawakalifisha basi wasaidieni”. Bukhaariy & Muslim 

Katika kusaidia utekelezaji wa haki hii ni lazima uwepo muda maalumu wa kuanza na kumaliza kazi. Muda huu ni wajibu uheshimiwe na pande zote mbili; mtumishi na mtumikiwa (muajiri) ili kuwepo na ufanisi katika utendaji mzima wa kazi.

 

4. DHAMANA YA MAHITAJI MUHIMU NA HIMAYA DHIDI YA MAJANGA YA KIMAUMBILE:

Uislamu unampa mfanyakazi/mtumishi haki ya dhamana ya mahitaji yake muhimu kiasi ya tosha ya maisha yake. Hivi ndivyo inavyofahamisha kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atakayetawalishwa (atakayetawazwa) kwetu sisi (kufanya) kazi fulani (kwa maslahi ya uma wa kiislamu) na (akawa) hana nyumba, basi na ajifanyie nyumba (kutokana na mali ya waislamu). Au (akawa) hana mnyama (kipando/gari), basi na ajitwalie mnyama (kwa mali hiyo)”. Bukhaariy & wengineo

Kauli hii ya Bwana Mtume kwa lugha ya leo inamaanisha dhamana (guarantee) ya maisha bora kulingana na zama anazoishi mtumishi huyo wa uma. Dhamana hii inahusisha:-

v     maskani (nyumba) bora na salama ya kuishi,

v     mke wa kumliwaza baada ya machovu yatokanayo na utumishi wa uma,

v     usafiri utakaomuwezesha kwenda katika utumishi wa uma na kurudi nyumbani.

 

Ijapokuwa hadithi hii imepokelewa katika kutaja na kubainisha haki za watumishi wa dola/serikali ya kiislamu. Kwa yakini sababu iliyompelekea mtumishi huyu wa dola kuyapata haya, ambayo ni kumuhakikishia na kumdhaminia tosha ya maisha yake ili aweze kuifanya kazi aliyopewa kwa amani, utulivu na ufanisi. Hapana shaka kwamba sababu hii inapelekea kuenea kwa hukumu kwa wafanyakazi na watumishi wengine. Sherehe (ufafanuzi) hii ya kauli ya Mtume haikusudii kusema kwamba kila muajiri analazimika kumpa muajiriwa wake mahitaji yake yote ya lazima zaidi kuliko ujira anaoustahiki. Bali maana yake ni kwamba dola ina wajibu wa kumtimizia mwananchi/raia wake huyu kile asichoweza kukipata kutokana na kazi aifanyayo. Baadhi ya nchi za Kiarabu na baadhi ya madola ya kimagharibi yamejaribu kwa kiwango kikubwa kulitekeleza zoezi hili ambalo ni sehemu ya mfumo sahihi wa maisha (Uislamu). Katika kulitekeleza zoezi hili nchi hizi zimefikia hatua ya kumlipa mtoto mchanga aliyezaliwa, bila ya kumsahau mzee kikongwe asiyejiweza. Huu ndio Uislamu, mfumo wa maisha waliochaguliwa wanadamu na Mola Muumba wao: “...NA NIMEKUPENDELEENI (nimekuridhieni) UISLAMU UWE NI DINI YENU...” [5:3]

Dola ya kiislamu imdhaminie mwanadola haki ya tosha ya maisha yake na himaya ya familia yake kutokana na maradhi, uzee au kifo. Hivi ndivyo ilivyokuja katika hadithi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atakayeacha mali (baada ya kufa), basi mali hiyo ni (haki) ya warithi wake. Na atakayeacha watoto walio dhaifu (hawana mali), basi na wanijie kwani mimi ndio mlinzi/msimamizi wao”. Bukhaariy

Katika hadithi hii, Bwana Mtume anawapa yatima walioachwa bila ya mali haki ya kupata mali ya dola, kwa kiasi kitakachowahakikishia kupata mahitaji yao ya msingi.

5. HAKI YA KUTENDEWA VEMA (KIBINADAMU):

 

Tabia na umbile la Uislamu ni umbile la sawa linalowaweka watu wote katika daraja moja la usawa. Mkubwa na mdogo, tajiri na masikini, mtumishi na mtumikiwa wote hawa ni sawa mbele ya macho ya Uislamu. Dhana hii ya usawa katika Uislamu haikinzani na ukweli wa utukufu na ubora waliopewa baadhi ya watu na Allah kwa hekima na busara azijuazo yeye mwenyewe. Haikanushi kuwaweka watu kulingana na daraja zao mbele ya Allah na mbele ya jamii. Kwa tabia na umbile hili la Uislamu ndio Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alivyoishi na watumishi wake. Tukimchulia Sayyidina Anas-Allah amuwiye radhi-kama kigezo chetu, Bwana Mtume hakupata kumkaripia, wala kumtolea maneno yenye kuumiza hisia zake au kumvunjia heshima. Huyu hapa Anas mwenyewe anaelezea namna ulivyokuwa utumishi wake kwa Mtume wa Allah: “Nilimtumikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa kipindi cha miaka kumi. Basi (katika kipindi chote hicho) hakupata kuniambia japo ‘ah!’ au ‘kwa nini umefanya?’ au ‘kwa nini hukufanya’. Muslim

Chini ya kivuli cha hali hii ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuelekea watumishi wake. Tunagundua kosa baya kabisa linalotendwa na wengi wetu leo. Ni ukweli uonekanao kwamba matajiri au waajiri walio wengi leo hawawatendei vema watumishi/waajiriwa wao, hili li bayana mbele ya macho ya kila mmoja wetu. Watumishi leo wanadharauliwa, wananyanyaswa, wanapuuzwa, wanapunjwa na kudhulumiwa haki zao na pengine hupigwa. Haya yanapingana na misingi ya sheria ya Uislamu. Katika hadithi iliyopokelewa na swahaba Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Inatosha (kabisa) shari mtu kumdharau nduguye muislamu”. Muslim

Imepokelewa kutoka kwa Ibn Masoud-Allah amuwiye radhi-amesema: “Nilikuwa nikimpiga bakora mtumwa wangu, nikasikia sauti nyuma yangu (ikisema): Tambua ewe Ibn Masoud. Sikuweza kuitambua sauti ile kutokana na ghadhabu (niliyokuwa nayo). Alipokurubia (mwenye sauti) tahamaki ni Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-naye akiniambia: “Tambua kwamba ewe Ibn Masoud Allah ana uwezo zaidi juu yako kuliko uwezo ulio nao wewe juu ya mtumwa huyu”. Nikasema sitampiga tena mtumwa ye yote baada ya leo.

Katika riwaya nyingine: “Bakora ile ilinianguka mkononi kutoka na khofu ya (maneno yale ya) Mtume”. Na katika riwaya nyingine: “Nikasema: Ewe Mtume wa Allah, nimemuacha huru kwa ajili ya Allah. Mtume akasema: “Ama lau usingelifanya hivyo, ungeliunguzwa na moto (wa Allah)”. Muslim

 


TUJIFUNZE NA TUKUBALI kuwa: “Atakayempiga mtumwa (mtumishi) wake kwa dhuluma, atalipiwa (mtumwa huyo) kisasi chake siku ya kiyama”.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Riwaya: Twabaraaniy


Forum | Guestbook | Tuandikie |