|
CHAFYA:
Kupiga chafya kunaonekana kuwa ni tendo la kawaida tu, kwa
hivyo wengi wetu huwa hatuizingatii chafya. Bwana Mtume tabibu
aliyefundishwa na Allah ana mtazamo tofauti na wetu kuelekea chafya. Yeye
anaiona chafya kuwa ni miongoni mwa neema za Allah kwa mwanadamu ambazo ni
wajibu wake kumshukuru kwazo Mola wake. Mtazamo huu wa Mtume wa Allah
unatokana na ukweli kwamba mtu anapopiga chafya, huwa anautoa ukungu
uliotanda katika ubongo wake. Ukungu huu hautoki ila kwa njia hiyo ya
kupiga chafya na kama haukutoka huweza kumsababishia mwanadamu madhara
makubwa. Kwa kulizingatia hili ndio chafya inapata hadhi ya kuwa neema
inayohitajisha shukurani na himda kwa Allah aliyetuwekea utaratibu huu wa
kupiga chafya. Kwa hivyo ni haki ya nduguyo muislamu anapopiga chafya na
akamuhimidi Allah, yaani akasema (Al-hamdulillaah), umshemue. Kumshemua
mtu aliyepiga chafya ni kumuombea dua kwa kumwambia:
(Yar-hamukal-laah)-yaani Allah akurehemu. Hivi ndivyo alivyotufundisha
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atapopiga chafya mmoja wenu
na aseme: (Al-hamdulillaah) na nduguye (amsikiaye akisema hivyo) amwambie:
(Yar-hamukal-laah). Atakapomwambia (Yar-hamukal-laah) nae (huyo mpiga
chafya) amwambie: (Yahdiykumul-laahu wayuswlih baalakum)”. Bukhaariy
Mpiga chafya kama hakusema (Al-hamdulillaah) mara tu
anapopiga chafya, huwa amejidhulumu mwenyewe haki ya kushemuliwa.
Utamshemua mpiga chafya mara ya kwanza, ya pili na ya tatu kwa kumwambia:
(Yar-hamukallaah). Akipiga tena chafya mara ya nne utamwambia:
(‘Aafakallaah) yaani Allah akuafu, kwa sababu sasa hiyo itakuwa sio
chafya ya kusafisha na kuuondoa ukungu bali ni ya ugonjwa. Kwa hivyo
unamuombea afya, huu ndio Uislamu ambao kila muumini anapaswa kuufuata.
Lakini kwa masikitiko makubwa tumeyatupilia mbali mafundisho haya na
kuuiga utamaduni wa kimagharibi. Leo sia ajabu bali ni sehemu ya maendeleo
muislamu anapopiga chafya kusema (I am sorry) badala ya kusema
(Al-hamdulillaah) kama alivyoelekezwa na Mtume wake.
KUJULIWA HALI (KUKAGULIWA) MGONJWA:
Mwanadamu anapopatwa na maradhi, humuondoka hali yake ya
kawaida na mahala pake kuchukuliwa na maumivu, machungu, udhaifu na
unyonge. Maradhi yakimzidia hutambaliwa na khofu ya mauti na kukata tamaa
ya kuishi. Katika hali na mazingira haya magumu, mwanadamu humuhitajia
sana mtu wa kumjali, kumuangalia, kumsaidia na kumliwaza. Mtu wa
kumtembelea (kumkagua) na kumuombea Mungu katika katika kipindi hiki
ambacho humkumbuka sana Allah Mola Muumba wake. Huyu humfungulia mlango wa
matumaini ya kupona kwa kushirikiana nae katika machungu yake. Ni kwa
kuyazingatia yote haya ndio Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-akatuagiza: “Akiumwa mkague”. Kwa hivyo basi kumzuru mgonjwa
ni haki yake aliyopewa na Uislamu. Na tendo hili hujenga baina ya waislamu
huruma, mapenzi na mshikamano. Kadhalika humpa nafuu mgonjwa na
kumkumbusha huyu aliyekuja kumuona thamani ya siha (afya njema) akapata
kumshukuru Allah kwa neema ya siha.
Ilivyo suna kwa mwenye kumkagua/kumtembelea mgonjwa
akifika amuulize hali, anajisikiaje, ampe matumaini ya kupona na amuombee
Mungu. Aseme kama alivyotufundisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie: “ALLAAHUMMA RABBAN-NAASI, ADH-HIBIL-BA’ASA, WASHFI
ANTAS-SHAAFIY, LAA SHIFAA ILLAA SHIFAAUKA, SHIFAA LAA YUGHAADIRU
SAQAMAN”. Bukhaariy & Muslim
MAANA: “Ewe Mola wa watu wote! Ondosha ubaya na uponye
kwani wewe ndiye mponyaji. Hakuna ponyo (liwezalo kuponya)ila ponyo lako,
ponyo lisiloacha ugonjwa wo wote (bila ya kuuponya)”.
Hii ndio dua anayoombewa mgonjwa na zipo nyingine kadhaa
kama zilivyopokewa kutoka kwa Mtume wa Allah. Kadhalika kunampasa mwenye
kumuangalia mgonjwa kumkumbusha mgonjwa kutubia kwa njia ya hekima bila ya
kumtisha na kumfanya ahisi kufa kufa. Kwa mfano anaweza kumwambia: Kwa
yakini katika maradhi yako haya unachuma kheri nyingi, kwa sababu maradhi
ni sababu inayomtakasa mja na Allah akamfutia dhambi zake. Kwa hivyo bila
ya shaka kwa kufungika kwako huku kutokana na maradhi ni fursa adhimu.
Fursa itakayokupatia ujira na thawabu nyingi mbele ya Allah kwa
kukithirisha kwako wakati huu kuleta dhikri, istighfaari na dua. Vile vile
kunamlazimu mwenye kwenda kumuangalia mgonjwa, kuchunga wakati wa kwenda
huko ili aende wakati muafaka. Asiende mapema asubuhi kwani inamkinika
mgonjwa akawa kapata usingizi wakati huo, baada ya kukesha kwa maumivu na
machungu wakati wa usiku. Kadhalika isiwe usiku sana wakati ambao mgonjwa
kachoka na anataka kupumzika, lakini anashindwa kukuambia ondoka ninataka
kupumzika. Vile vile asikae muda mrefu sana kwa mgonjwa au kumpa khabari
za huzuni na kutisha. Pia yatakikana kuchunga, kuheshimu na kufuata amri
na maelekezo ya daktari, kama daktari amekataza kuzungumza na mgonjwa,
basi usimsumbue kwa kumzungumzisha. Au amekataza kutoingia watu wengi kwa
mgonjwa kwa wakati mmoja, basi na waingie wale tu wanaoruhusiwa. Ni kheri
pia ikiwa kila unapokwenda kumuona mgonjwa ukamchukulia zawadi ya kile
akipendacho, chakula au matunda yatakayomuongezea nguvu. Na sio vitu kama
sigara na pombe vitakavyochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa maradhi
yake. Mpe msaada wa pesa kiasi cha uwezo wako ili zimsaidie katika
kugharamia matibabu na kuendesha mambo ya nyumbani kwake.
Kwa ujumla kumtembelea mgonjwa na kumsaidia ni jambo lenye
fadhila kubwa. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Kwa
hakika Allah atasema siku ya kiyama: Ewe mwanadamu, niliumwa hukuja
kuniona. (Mwanadamu) aseme: Ewe Bwana Mlezi wangu, vipi ningekuja kukuona
na ilhali wewe ndio Mola wa walimwengu wote? (Allah) atamwambia: Je,
hukujua kwamba mja wangu fulani anaumwa? Je, hukujua kama ungelienda
kumuona ungenikuta mimi kwake?...”. Muslim
KUMZIKA:
Kila kilicho hai hakina njia ya kukwepea mauti: “KWA
YAKINI WEWE UTAKUFA NA WAO PIA WATAKUFA”. [39:30]
Mtu anapokufa, huwa ni pigo na msiba mkubwa kwa familia
husika, kwani huwa limekauka na kuanguka tawi katika mti wa familia. Na
familia huwa imepungukiwa na tofali miongoni mwa matofali yanayoijenga
familia hiyo. Mafungamano na mahusiano baina ya muislamu na nduguye
muislamu, hayakatiki kwa kufa mmoja wao. Bali kamba ya mahusiano haya
huendelea kuungwa na maagano ya mwisho. Haya kwa mujibu wa sheria ni
pamoja na kumkosha, kumkafini (kumvika sanda), kumswalia na kulisindikiza
jeneza lake mpaka makaburini. Ambako mwili wake utatiwa kaburini mwake na
kuzikwa kama alivyosema Allah: “KATIKA HII (ardhi/udongo) TUMEKUUMBENI,
NA HUMO TUTAKURUDISHENI, NA KUTOKA HUMO TUTAKUTOENI MARA NYINGINE (muwe
hai tena)”. [20:55]
Yote haya ndio yanayoifasiri kivitendo kauli ya Bwana
Mtume-Rehema zimshukie-aliposema: “Na akifa lifuate jeneza lake”.
Mambo haya yana mchango mkubwa kabisa katika kuiliwaza familia ya marehemu
katika kipindi hiki kigumu cha msiba. Miongoni mwa maneno ya ta’azia
ambayo muislamu anatakiwa kuwaambia wafiwa ni pamoja na: “FALILLAAHI MAA
A’ATWAA WALILLAAHI MAA AKHADHA, WA KULLU SHAYN ‘INDAU BIAJALIN
MUSAMMAA”.
MAANA: “Ni chake Allah alichokitoa na ni chake Allah
alichokitwaa na kila kitu kina muda maalumu mbele yake”. Bukhaariy &
Muslim.
Katika kuyatenda yote haya kuna fadhila na ujira mkubwa,
hivi ndivyo anavyosema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“Atakayehudhuria jeneza mpaka likaswaliwa, basi yuna yeye
‘Qiyraatw’, na atakayelihudhuria mpaka likazikwa yuna ‘Qiyraatw’
mbili. (Mtume) akaulizwa ni nini hizo Qiyraatw mbili? Akasema: Ni mithili
ya majabali mawili makubwa”. Bukhaariy & Muslim.
Hizi ni sehemu tu ya haki za muislamu kwa nduguye muislamu
kama zilivyoelezwa na Mtume wa Uislamu katika hadithi yake. Kwa hakika
haki za muislamu kwa muislamu mwenziwe ni nyingi mno kathiri, lakini
yamkinika kuzikusanya zote na kauli ya Mtume: “Muislamu ni ndugu ya
muislamu:-
-
Hamdhulumu wala hamsalimishi (kwa maadui).
-
Na atakayekuwa katika haja ya nduguye (akamsaidia),
Allah atakuwa katika haja yake yeye.
-
Na atakayemuondoshea shida muislamu, Allah
atamuondoshea shida miongoni mwa shida za siku ya kiyama.
-
Na atakayemsitiri muislamu, Allah atamsitiri siku ya
kiyama”. Bukhaariy & Muslim
Ikiwa kila mmoja wetu atazichunga na kumtekelezea nduguye
muislamu haki zake ambazo chimbuko lake ni udugu wa imani. Basi hapana
shaka kwamba huruma, mapenzi, umoja na mshikamano vitatawala baina ya
waislamu.
TANBIHI:
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amewakataza
wanawake kulisindikiza jeneza mazikoni. Imekuja katika hadithi
iliyopokelewa na Ummu ‘Atwiyyah: “Tumekatazwa kuyafuata majeneza
(mazikoni)...” Muslim
Si katika mila ya Uislamu kile kinachojulikana leo kama
“last respect” ambacho huhusisha kukashifiwa kwa maiti na watu wakawa
wanapita mbele yake mmoja baada ya mwingine kwa imani ya kutoa heshima ya
mwisho. Huu si Uislamu yaani si sehemu ya mafundisho aliyotuachia nabii
Muhammad-Rehema na Amani zimshukie.
|