|
Tuanze na kujiuliza,
jirani ni nani? Jirani tunayemkusudia hapa ni yule mtu aliye karibu yako
kimakazi, yaani nyumba zenu zinakurubiana. Mtu mwenye wasifu huu ana haki
kubwa juu yako, ewe muislamu. Itakaposadifu kwamba jirani yako ni ndugu
yako wa nasabu na akawa ni muislamu mwenzako. Basi jirani huyu atakuwa ana
haki tatu kwako; haki ya ujirani, haki ya udugu na haki ya Uislamu. Na
akiwa jirani yako ni muislamu lakini si nduguyo wa nasabu, huyu atakuwa
nazo kwako haki mbili; haki ya ujirani na haki ya Uislamu. Na iwapo jirani
yako huyu si muislamu na hapana udugu baina yenu, jirani huyu atamiliki
kwako haki moja tu nayo ni haki ya ujirani. Hivi ndivyo anavyotufundisha
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Majirani ni watatu; jirani
mwenye haki moja naye ndiye mwenye haki ndogo kuliko wote. Na jirani
mwenye haki mbili na jirani mwenye haki tatu. Ama yule ambaye mwenye haki
moja ni jirani mushriki (kafiri), na ama ambaye mwenye haki mbili ni
jirani muislamu (ana) haki ya Uislamu na haki ya ujirani. Na ama yule
mwenye haki tatu ni jirani muislamu aliye ndugu, (ana) haki ya Uislamu,
haki ya ujirani na haki udugu”. Al-Bazzaar & Abuu Nuaim.
Muislamu anakiri,
anaikubali na kuichunga haki ya jirani akiamini kuwa kufanya hivyo ni
kuitekeleza amri ya Mola wake: “MWABUDUNI ALLAH WALA MSIMSHIRIKISHE NA
CHO CHOTE NA WAFANYIENI IHSANI WAZAZI WAWILI NA JAMAA NA MAYATIMA NA
MASKINI NA JIRANI WALIO KARIBU NA JIRANI WALIO MBALI--- [ 4 : 36] Naye
Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-kama mfasiri mkuu wa Qur–ani,
anauelezea uzito wa haki hii ya jirani iliyotajwa ndani ya Qur-ani
anasema: “Hakuacha Jibril kuniusia juu ya jirani mpaka nikadhani kwamba
atampa na haki ya kurithi”. Bukhaariy
& Muslim.
Miongoni mwa haki za
jirani kama zilivyoelezwa na Uislamu ni kumtendea wema kiasi cha uwezo wa
mtu. Mtendee wema jirani yako kwa mali yako, cheo chako na kila chako
chenye kuweza kumnufaisha kwa namna moja au nyingine. Hivi ndivyo anavyo
tufundisha. Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie– kutokana na
kauli yake: “Jirani bora mbele ya Allah ni yule aliye mwema kwa jirani
yake”. Tirmidhiy.
Na akasema tena
Bwana Mtume: “Mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho basi na amtendee
wema jirani yake”. Muslim.
Kauli hii ya Mtume
wa Allah kama inafahamisha jambo, basi jambo hilo si jingine bali ni kuwa
ukitaka kumjua muumini wa kweli basi muangalie anavyoishi na jirani yake.
Imepokelewa kutoka kwa Muawiyah Ibn Jundub-Allah amuwiye radhi–kwamba
alimuuliza Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie: “Ewe Mtume wa
Allah, ni ipi haki ya jirani kwa jirani yake? Mtume akamjibu:-
Akiugua mkague
(mtake hali),
Akifa msindikize
(nenda kamzike),
Akikuomba mkopo,
mkopeshe,
Akienda utupu (hana
nguo), msitiri ( mvike ),
Akipatwa na kheri,
mpongeze,
Akipatwa na msiba,
muizi (mfanyie ta’azia),
Wala usinyanyue
nyumba yako zaidi kuliko nyumba yake ukamzibia hewa/upepo,
Na wala usimuudhi
kwa harufu ya chungu chako ila umchotee kidogo”. Twabaraaniy
Kumtendea wema
jirani alikokueleza Bwana Mtume katika hadithi tulizozitaja ni pamoja na
kumpelekea zawadi katika furaha mbali mbali anazozipata. Mithili ya
kufaulu katika mtihani, kupata cheo, kuzaliwa mtoto, kuoa/kuozesha,
kujenga nyumba na kadhalika. Falsafa na siri ya kupeana zawadi ni kujenga
mapenzi na kuondosha chuki na uadui kama anavyolibainisha hilo Mtume wa
Allah–Rehema na Amani zimshukie: “Peaneni zawadi mtapendana, na
peaneni mikono itakuondokeeni chuki baina yenu”. Ibn Asaakir.
Na katika jumla ya
haki za jirani ni kutokumuudhi kwa kauli au matendo. Siku moja Mtume wa
Allah–Rehema na Amani zimshukie– alisema: “Wallahi hawi muumini,
Wallahi hawi muumini, Wallahi hawi muumini. Maswahaba wakamuuliza: Ni nani
huyo ewe Mtume wa Allah? Akajibu: Huyo ni yule ambaye jirani yakke
hasalimiki na shari/uovu wake”. Bukhaariy
Mtu mmoja alimuendea
Mtume wa Allah na kumuambia: “Hakika mwanamke fulani anatajwa sana kwa
wingi wa swala zake, kutoa kwake sadaka kwa wingi na wingi wa kufunga
kwake. Isipokuwa kwamba yeye anamuudhi jirani yake kwa ulimi wake. Mtume
akasema: “(Pamoja na ibada zake zote hizo, mwanamke) huyo ataingia
motoni”. Ahmad, Al-Bazzaar, Ibn Hibbaan & Al-haakim.
Kauli hii ya Mtume
wa Allah inaonyesha uzito wa dhambi ya kumuudhi jirani na kwamba ibada ya
mtu anayemfanyia maudhi jirani yake haitamsaidia kuingia peponi jirani
huyo mbaya. Na kinyume chake, kutokumuudhi jirani ni sababu tosha
inayoweza kumuingiza mtu peponi, kwani kukaa kwa wema na jirani bila ya
kumuudhi kwa maneno au matendo ni kielelezo cha wema wa mja. Imepokelewa
kwamba mtu mmoja alimwambia Mtume wa Allah– Rehema na Amani
zimshukie–nijulishe amali ambayo nitakapoitenda nitaingia peponi. Mtume
akamjibu: “Kuwa mwema”. Akasema mtu yule: Ewe Mtume wa Allah,
nitajuaje kwamba mimi ni mwema?
Mtume akamwambia:
Waulize jirani zako, wakikuambia kwamba wewe ni mtu mwema basi fahamu
kwamba wewe ni mwema (kweli). Na wakikuambia kwamba wewe ni mtu mbaya
(muovu), basi fahamu kwamba wewe ni mbaya (kweli )”. Al-Baihaqiy
Huyu ndiye jirani na
haki yake katika Uislamu, lakini watu wengi miongoni mwetu hawaijali haki
hii ya ujirani. Kutokuitambua haki hii ya ujirani ndio imekuwa sababu kuu
ya magomvi uadui na mizozo mitaani mwetu. Utawaona majirani daima
wakigombana kwa mambo ya kipuuzi kabisa kiasi cha kuwafanya wasijuliane
hali na kutokushirikiana katika furaha wala huzuni. Huu si Uislamu
aliokuja nao Bwana Mtume kutoka kwa Allah, muislamu wa kweli haishi hivyo
na jirani yake hata kama si muislamu mwenziwe(kafiri )
|