|
2- WAJIBU WA RAIA/HAKI ZA VIONGOZI.
Utakapofungamana uongozi kwa mtu ambaye waislamu
wamemridhia kwa nafsi zao, dini na dunia yao. Atakuwa tayari ana dhima na
wajibu ambao ni haki ya Allah na haki ya uma (raia) wake. Sasa basi ili
aweze kuutekeleza wajibu wake huu ipasavyo na kwa ukamilifu, Uislamu
umempa haki kadhaa juu ya raia wake. Haki hizi zimsaidie katika kumtumikia
Allah na uma wake. Miongoni mwa haki hizi za kiongozi katika Uislamu ni
kama zifuatavyo:-
KUSIKILIZWA NA KUTIIWA:
Miongoni mwa haki za kiongozi ambazo ni wajibu wa uma
(raia) kumtekelezea kama mtumishi wao ni kumsikiliza na kumtii katika hali
zote maadam hakuamrisha maasi. Haki hii anapewa na mwenyewe Allah, hebu na
tuitegee siko Qur-ani Tukufu: “ENYI MLIOAMINI! MTIINI ALLAH NA MTIINI
MTUME NA WENYE MAMLAKA JUU YENU (viongozi) WALIO KATIKA NYIE (waislamu
wenzenu)...” [4:59]
Hii ni nukuu ya Qur-ani inayowafaradhishia waumini kwanza
kumtii Allah Mola Muumba wao na kadhalika kumtii Mtume wake. Na muislamu
anapaswa kutambua kwamba kumtii Mtume ni kumtii Allah aliyemtuma kutuletea
sheria hii: “MWENYE KUMTII MTUME AMEMTII ALLAH (kwani anayoyaamrisha
Mtume yametoka kwa Allah)...” [4:80]
Na suna ya Mtume ni sehemu ya sheria ya Allah (sheria
mama), kazi yake ni kubainisha mujmali (ujumla) wa sheria mama. Kwa
mantiki hii suna ya Mtume inakuwa ni sheria shereheshi. Baada ya aya
kuwaamrisha waumini kumtii Allah daraja la kwanza, kumtii Mtume wa Allah
daraja la pili, ndipo ikawaamrisha kumtii kiongozi daraja la tatu.
Utaratibu huu wa twaa unaonyesha kuwa twaa ya kiongozi inaiandamia twaa ya
Mtume ambayo nayo inaiandamia twaa ya Allah Mola Mwenyezi. Kwa utaratibu
huu ni muhali kumtii Mtume bila ya kumtii kiongozi na hivyo hivyo ni
muhali kumtii Allah bila ya kumtii Mtume wake. Kadhalika utaratibu huu
unafahamisha kuwa raia hawawajibiki kumtii kiongozi wao mpaka kwanza naye
awe anamtii Allah na Mtume wake sambamba na kusimamisha sheria ya Allah.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema kuhusiana na haki hii ya
kiongozi: “Sikilizeni na kumtii hata kama atakutawalieni (mambo yenu)
mtumwa wa kihabeshi mwenye kichwa mithili ya zabibu”. Bukhaariy. Akasema
tena: “Ni juu ya mtu muislamu kusikiza na kumtii (kiongozi) katika
alipendalo na alichukialo maadam hakuamrishwa maasi. Ikiwa ataamrishwa
maasi, basi (hapo) hakuna kusikiliza wala kutii”. Bukhaariy &
Muslim.
Uislamu siku zote unapupia mshikamno na umoja wa uma na
kuepusha njia za migongano na fitna. Kwa kulizingatia na kulichunga hili,
Uislamu umewatahadharisha na kuwaonya waislamu dhidi ya kujitoa katika
twaa ya kiongozi na kumuasi. Eti kwa sababu tu ya maasi na ufasiki
unaotendwa na kiongozi huyo kama binadamu mwingine ye yote. Si haki
kumuasi muda wa kuwa hajatenda ukafiri wa waziwazi kabisa. Isieleweke kuwa
Uislamu unamlea na kumlinda kiongozi fasiki, la hasha. Uislamu unaangalia
uzito na athari ya mambo mawili haya kwa jamii; uasi/ufasiki wa kiongozi
na fitna/shari ya kumuasi kiongozi fasiki. Uislamu ukaona kuwa
fitna/athari ya ufasiki wa kiongozi kwa jamii si kubwa zaidi kuliko athari
ya kumuasi kiongozi huyo. Fitna hii ya kujitoa katika twaa ya kiongozi ni
shari yenye kuendelea, kwani itaugawa uma katika matapo (makundi) mawili.
Tapo la kiongozi fasiki mwenye dola (nguvu) na tapo la hawa raia
waliojitoa wasio na nguvu za kuwahami dhidi ya nguvu za dola
watakazoshushiwa na kiongozi fasiki ili kuwarejesha katika twaa yake na
kukomesha uasi wao kwake. Katika hali hii ya mgawanyiko ni lazima patazuka
vita ya wenyewe kwa wenyewe vitakavyozichukua muhanga roho za watu wengi
wasio na hatia. Kwa kulichelea hili ndio Uislamu ukautaka uma kusubiri na
kustahamili juu ya ufasiki huu wa kiongozi wao huku ukiitumia haki yao ya
kumuelekeza na kumnasihi kwa utaratibu wa kiislamu. Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie-anatuambia: “Atakayeung’oa mkono katika twaa (ya
kiongozi), atakutana na Allah na ilhali hana hoja. Na atakayekufa na
ilhali hana shingoni mwake kiapo cha utii (kwa kiongozi) atakufa mauti ya
kijahilia”. Muslim. Akazidi kutuambia: “Atakayelichukia kwa kiongozi
wake jambo/tabia fulani, basi na asubiri. Kwani atakayejitoa katika twaa
ya kiongozi kwa (kiasi cha) shubiri moja (tu), atakufa mauti ya
kijahilia”. Bukhaariy & Muslim. Mukhtasari wa kauli, hakumuhalalikii
muislamu ye yote kumuasi kiongozi aliye muislamu mwenziwe kwa kisingizio
cha uasi/ufasiki wa kiongozi huyo. Ni wajibu wake kuendelea kumtii pamoja
na uasi wake huo maadam uasi huo haujafikia kiwango cha kufuru ya wazi
isiyo na tafsiri nyingine ila kufru tu.
KUMSAIDIA NA KUSIMAMA NAE KATIKA JIHADI:
Ni wajibu wa raia (uma) kumuunga mkono na kumsaidia
kiongozi wao katika kuwatumikia. Na hii ni haki inayokwenda sambamba na
haki ile ya twaa. Kila atakalolifaradhisha au kuliamrisha kiongozi ndani
ya mipaka ya sheria kwa maslahi ya uma, dini ya Allah na kulinda heshima
ya waislamu na dini yao. Ni wajibu wa kila muislamu (raia) kuitekeleza
amri hiyo ya kiongozi wake hata kama itagharimu uhai wake. Hili linatokana
na ukweli kwamba kiongozi kama binadamu hawezi kubeba dhima hii kuu ya
kuutumikia uma mpaka raia wasimame upande wake na kumsaidia kwa mali na
nafsi zao. Kiongozi akitangaza jihadi dhidi ya maadui wa Uislamu, jihadi
hii haitasimama ila kwa msaada na uungaji mkono wa raia. Kama
tulivyotangulia kueleza kuwa haki ya msaada na kusimama na kiongozi katika
jihadi inaandamana na haki ya twaa. Kadhi Abuu Ya’alaa-Allah
amrehemu-anasema: “Imamu (kiongozi) atapotekeleza haki za uma (raia),
zitamuwajibikia yeye juu yao (raia) haki mbili: (Haki ya) twaa na (haki
ya) msaada (kuungwa mkono), muda wa kuwa halipatikani upande wake jambo
litakalomtoa katika amana/uaminifu”.
TOSHA YA MAISHA YAKE:
Kiongozi wa kiislamu huutumia muda wake mwingi pengine
hata ule wa mapumziko binafsi katika kuhakikisha kuwa anayatekeleza vema
na ipasavyo majukumu yake kama mtumishi wa uma. Huutumia muda wake huu kwa
ajili ya maslahi na manufaa ya uma wake. Kwa kuuzingatia ukweli huu na
kuuthamini mchango huu wa kiongozi, Uislamu unampa haki ya kuchukua tosha
ya maisha yake katika mali ya waislamu. Kiasi anachoruhusiwa kuchukua ni
kile kinachoweza kukidhi mahitaji yake na familia yake kwa wema bila ya
ubadhirifu. Zama alipotawazwa Sayyidna Abuu bakri-Allah amuwiye radhi-kuwa
Amirul-Muuminina kushika nafasi iliyoachwa wazi kwa kufariki kwa Bwana
Mtume, maswahaba wa Mtume wakaambizana: Mkadirieni khalifa wa Mtume
kitakachomkwasia (kitakachomtoshelaza) Wakasema: Naam, nguo mbili
atakapozichakaza atazivua na kuchukua nyingine mithili ya hizo. Kipando
(usafiri) anapotaka kusafiri na matumizi ya nyumbani kwake (outlay) kama
alivyokuwa akitumia kabla ya kutawazwa khalifa. Abuu bakri akasema:
Nimeridhia.
Yatizame haya katika “TWABAQAAT” ya Ibn Sa’ad juzuu
ya tatu, sahifa 184 na 185. Kadhalika amepokea Ibn Sa’ad kutoka kwa Bi.
Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: Alipotawazwa Abuu Bakri alisema: Kaumu
yangu inatambua fika kwamba kazi yangu haikushindwa kuilisha familia
yangu. Na hivi sasa nimeshughulika na mambo ya waislamu na nitachuma
katika mali yao na familia ya Abuu Bakri itakula kutokana na mali hiyo.
(Twabaqaat).
Na wakati alipotawalia ukhalifa Sayyidna Umar Ibn
Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-waliulizana baadhi ya maswahaba waliokuwa
katika baraza ya Umar kuhusiana na kinachomuhalalikia katika mali ya
Allah. Umar akawaambia: Mimi nitakuelezeni kinachonihalalikia katika mali
hiyo. Zinanihalalikia nguo mbili; nguo ya kiangazi (joto) na nguo ya
kipindi cha baridi. Mnyama wa kuendea Hijjah na Umrah, chakula changu na
familia yangu kama chakula cha mtu wa kawaida katika Makurayshi ambaye si
tajiri wala fakiri wao. Kisha mimi nichukuliwe kama ye yote miongoni mwa
waislamu, yananifika yanayowafika.
Riwaya hizi za tarekh na mithili ya hizi zinafahamisha
kuwa kiongozi (Amirul-Muuminina) ana haki katika Baytul-Maali (khazina) ya
waislamu. Achukue/apewe katika mali hiyo kadri ya haja yake na familia
yake ili asishughulike na kazi nyingine itakayomfanya ashindwe kutimiza
majukumu kama kiongozi na mtumishi wa uma.
|