|
WAJIBU WA KIONGOZI/HAKI ZA RAIA.
IV/. KUGAWA MADARAKA KWA KUWATEUA VIONGOZI WA CHINI YAKE.
Kiongozi mkuu ndiye mwenye dhima na jukumu la kuongoza
serikali sambamba na kupanga mipango endelevu ya jamii (raia). Ana wajibu
mkuu wa kuhakikisha kuwa mipango na taratibu hizo zinahamishwa kutoka
maandishini na kutiwa katika ulimwengu wa matendo kwa maslahi na manufaa
ya jamii yake. Ni jukumu lake kuutumikia uma wake kwa uadilifu. Kutokana
na ukubwa, uzito na ugumu wa majukumu haya ya kiongozi kama mtumishi mkuu
wa uma, ni dhahiri kuwa hataweza kulibeba furushi hili la majukumu peke.
Kutokana na ukweli huo usiokanushika ni haki ya msingi ya raia wake na ni
wajibu wake wa lazima kuwateulia watu miongoni mwao watakaomsaidia katika
majukumu ya utawala. Hii ndio njia aliyoitumia Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-wakati wa ustawi (kupanuka) wa dola ya Kiislamu zama za uhai
wake. Ukizifungua kurasa za tarekh (history) hutoshindwa kuona kuwa Bwana
Mtume aliwateua kwa vipindi maalumu mabwana Aliy Ibn Abuu Twaalib na
Muaadh Ibn Jabal-Allah awawiye radhi-kuwa makhalifa wake katika nchi ya
Yemen. Kama alivyomteua Abuu Musa na maswahaba wengine-Allah awawiye
radhi-kuwa makadhi baadhi yao na wengine kuwa magavana na walinganiaji
dini sehemu mbalimbali za ulimwengu ule wa Kiislamu. Bwana Mtume
alipomteua mmojawapo wa maswahaba wake kuwa kiongozi wa uma katika ngazi
fulani, hakumuachia kuongoza kwa maoni na matashi yake binafsi. Bali
alimpa muongozo kamili wa kufuata katika kazi yake hiyo, sambamba na miiko
na mipaka ya kazi. Na zaidi ya yote hayo alimuusia kumcha Allah na kuwa
muadilifu katika kazi yake hiyo. Katika uteuzi huu wa viongozi (makhalifa)
wa chini yake, Bwana Mtume alitumia vigezo maalumu. Aliangalia uaminifu,
uwezo wa kazi (utawala), ucha-Mungu na baki ya sifa nyingine njema.
Hakumteua katu mtu ajizi, dhaifu wala mwenye pupa ya kupata uongozi ili
awe bwana mkubwa (muheshimiwa). Swahaba Abuu Dhari alimuomba Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kumpa nafasi ya uongozi. Mtume akamwambia:
“Wewe ni dhaifu (huuwezi uongozi) nao (huo uongozi) ni amana na siku ya
kiyama ni fedheha na majuto. Ila kwa atakayeutwaa kwa haki yake na
akayatekeleza yanayompasa katika huo uongozi”. Muslim
Utaratibu huu wa uteuzi ulirithiwa pia na makhalifa wa
Mtume baada ya kufa kwake, na inatakikana urithiwe pia na viongozi wetu
wakuu wa leo kwa maslahi ya uma.
V/. JIHADI KATIKA DINI YA ALLAH NA ULINZI (HIMAYA) WA
DOLA.
Allah Mola Mwenyezi amemleta Mtume wake Muhammad-Rehema na
Amani zimshukie-kwa watu wote: “NA HATUKUKUTUMA (hatukukuleta) ILA KWA
WATU WOTE, UWE MTOAJI WA KHABARI NZURI NA MUONYAJI...” [34:28]
Kwa kauli na tangazo hili la Allah, Bwana Mtume akabeba
amana hii ya kuwa mjumbe wa Allah kwa ulimwengu mzima. Akaitekeleza haki
ya amana hii kwa kuufikisha ujumbe wa Allah kwa walimwengu wote kwa
kipindi kisichotindika miaka kumi na tatu. Hapo ndipo akatunukiwa shahada
ya ustahiki iliyopigwa muhuri wa kukamilisha na kukhitimisha kazi kwa
kauli yake Allah: “...LEO NIMEKUKAMILISHIENI DINI YENU NA KUKUTIMIZIENI
NEEMA YANGU NA NIMEKUPENDELEENI UISLAMU UWE DINI YENU...” [5:3] Kutokana
na vikwazo alivyokumbana navyo katika kuitekeleza kazi hii ya Mola wake,
wakati mwingine kulimlazimu Mtume kujitoa muhanga kwa mali na nafsi yake
ili kuipigania dini ya Allah. Akapanga katika uhai wake mikakati ya
kuwaandaa maswahaba wake kuchukua na kuiendeleza kazi aliyoianza. Baada ya
kufa Mtume, maswahaba-Allah awaridhie-wakaibeba mabegani mwao bendera ya
da’awah na kuufikisha Uislamu kule usikofika bado. Wakashika hatamu za
kuwaongoza watu katika mfumo sahihi wa maisha uliofumwa na Mola wao
(Uislamu), mpaka sheria ya Allah ikatawala zaidi ya robo tatu ya dunia.
Elewa na ufahamu ewe ndugu muislamu khususan kiongozi, kuwa jihadi hii ya
kuipigania dini ya Allah iliyoasisiwa na mtume wako na kuendelezwa na
maswahaba wake watukufu. Jihadi hii inaendelea muda wa kuwepo/kupatikana
sababu zinazoiwajibisha mpaka kutoweka kwa mbingu, ardhi na vyote
vilivyomo (kiyama). Jihadi hii ni kwa ajili ya kulinda, kutetea na
kuchunga heshima, uhai, mali na haki ya waislamu kama jamii. Sambamba na
haki yao ya kuabudu kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu na kuutangaza
Uislamu ulimwenguni kote bila ya kizuizi cha aina yo yote ile. Nafasi ya
Mtume katika kuuongoza uma katika jihadi unayo wewe ambaye ndio kiongozi
wa waislamu leo. Hii ni dhima isiyoepukika iliyo shingoni mwako, ni wajibu
wako bali ni sehemu ya dini khasa kuwaongoza raia wako katika jihadi iwapo
hali na mazingira yanalazimisha hivyo. Na kunawawajibikia raia wako wote
wenye kumuamini Allah na siku ya mwisho kukutii katika hilo.
VI/. USIMAMIZI, UENDELEZAJI NA ULINZI WA RASILIMALI YA
DOLA NA KUHAKIKISHA MGAWANYO ADILIFU WA MALI HIZO MIONGONI MWA RAIA.
Mali ndio kano (mshipa) na zana ya maisha haya na pengine
ndio sababu ya mafanikio ya maisha ya ulimwengu huu na ule ujao (akhera).
Mali pia ni mojawapo ya nguzo za nguvu inayoamrishwa katika kauli tukufu
ya Allah: “BASI WAANDALIENI (wawakeeni tayari) NGUVU MZIWEZAZO (silaha)
NA MAFARASI (vifaru, madege, manowari) TAYARI TAYARI (mipakani). ILI KWAZO
(nguvu hizi) MUWAOGOPESHE MAADUI WA ALLAH NA MAADUI WENU...” [8:60]
Kadhalika mali ni uti wa mgongo wa maisha ya uma, kwa ukweli huu ni haki
ya msingi ya raia na ni wajibu wa kiongozi kuwaratibia raia wake mipango
mizuri ya kiuchumi. Mipango itakayowashirikisha katika kuendeleza
rasilimali za dola na kunufaika nazo katika nyanja za maisha yote ya
kijamii. Mipango itakayowahakikishia kupata mahitaji yao ya msingi kwa
njia halali na rahisi. Ni wajibu wa kiongozi kuanzisha
‘Baytul-Maali’-(Public Treasury) itakayokuwa na vyanzo vya mapato ili
iweze kujitegema katika kutoa huduma kwa uma. Kiongozi atakuwa na wajibu
wa kusimamia mapato na matumizi ya Baytul-Maali moja kwa moja au kupitia
kwa atakayemteua kwa kazi hiyo. Miongoni mwa haki za raia kwa kiongozi wao
ni kupata mgawanyo sawa wa rasilimali za dola na huduma sawa za kijamii
bila ya upendeleo wa mahala fulani kwa sababu tu ndiko anakotoka kiongozi
huyo. Ahakikishe kuwa mali ya uma haihujumiwi na na kuibiwa na watu wa
nje. Wanawazuoni wa kale na hawa wa sasa-Allah awarehemu-wameandika mengi
katika ukumbi huu wa kisiasa khususan katika jukwaa hili la uongozi.
Sheikh Al-Maawardiy-Allah amrehemu-ni mmoja wa wanazuoni walioshika kalamu
katika fani hii na kueleza kwa ufafanuzi wa kina. Yeye ameukusanya wajibu
wa kiongozi katika vifungu kumi, kama ifuatavyo:-
KULINDA MISINGI YA DINI:
Ni wajibu wa kiongozi kulinda misingi ya dini na Ijmaa ya
salafu. Akitokeza mzuzi (mzushi) au mpinzani wa misingi hiyo, ni wajibu
wake yeye mwenyewe au kupitia mteule wake kumuwekea wazi mzuzi huyo hoja
na kumbainishia ilivyo ndivyo. Ayafanye yote haya ili kuilinda dini dhidi
ya kombokombo na kuulinda uma na mgawanyiko usio wa lazima.
KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA SHERIA:
Kunamlazimu kiongozi kama mtumishi wa uma kuhakikisha kuwa
sheria ya Allah ndio inayotumika katika kuwahukumu mahasimu wawili na
kukata magomvi baina ya wagombanao. Ni wajibu wake kuhakikisha kuwa sheria
inampa haki kila aistahikie mpaka mwenye nguvu asiweze kumuonea mnyonge
kwa sababu tu ya nguvu zake.
KUIMARISHA NGUVU ZA DOLA:
Ni wajibu wakiongozi kuunda serikali imara na yenye nguvu
itakayowahakikishia raia wake amani, salama na utulivu. Vitu ambavyo
vitawawezesha kuendesha shughuli zao za kimaisha kwa uhuru na bila ya
khofu wala bughudha. Watu waweze kusafiri wakiwa hawana khofu juu ya nafsi
au mali zao.
KUWEKA MIPAKA:
Aweke mipaka itakayochunga maharamisho ya Allah yasitendwe
na kulinda haki za waja wake zisivunjwe.
KUWEKA ULINZI IMARA KATIKA MIPAKA YA NCHI:
Kunampasa kuhakikisha kuwa kuna ulinzi wa kutosha na imara
kuzunguka mipaka yote ya nchi. Ili kuilinda nchi dhidi ya uvamizi wa
ghafla kutoka kwa maadui wa nje.
JIHADI DHIDI YA MPINZANI WA UISLAMU:
Kiongozi ana wajibu wa kumpiga vita mtu uliomfikia ujumbe
wa Uislamu na akaupinga bila ya kuwa na hoja yenye kuzingatiwa. Ampige
vita mpaka ima aukubali Uislamu (asilimu) au awe chini ya dhima ya Uislamu
(awe Dhimiyu).
KUSIMAMIA MATUMIZI YA FEI NA SADAKA/ZAKAH KWA MUJIBU WA
SHERIA:
Fei ni ile mali inayopatikana bila ya vita baada ya maadui
kukimbia, mali hii na ile itokanayo na sadaka/zakah ni dhima na amana
iliyo mikononi mwa kiongozi. Kwa hivyo basi ni jukumu lake kuhakikisha
kuwa mali hiyo inatumika kwa namna ilivyoagizwa na sheria.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI:
Kiongozi anapaswa kukadiria mapato na matumizi ya
Baytul-Maali na kutoa kasimu (fungu) panapostahiki kwa wakati muafaka bila
ya ubadhirifu au kuchelewa.
KUTEUA WATU STAHIKI WAAMINIFU NA WENYE SIFA STAHIKI
KUENDESHA MAMBO:
Kunamuwajikia kiongozi kuwateua watu watakaomsaidia katika
kuendesha shughuli mbalimbali za kiutawala. Vigezo vya uteuzi huo viwe ni
uaminifu na sifa stahiki kwa kazi husika ili huduma za kijamii ziendeshwe
vema na mali ya uma iwe katika udhibiti wa watu waaminifu.
KUONGOZA NA KUSIMAMIA IDARA ZOTE ZA UTAWALA:
Kiongozi anawajibika kutoa muongozo wa uendeshaji wa
shughuli za utawala katika idara/wizara mbalimbali za serikali yake. Na
kusimamia na kufuatilia kwa karibu utendaji wa watendaji aliowateua
kushika nyadhifa hizo.
Ili kuyaona haya na mengi mengineyo yahusuyo mambo ya
utawala na sheria, rejea kitabu “AL-AHKAAMUS-SULTWAANIYYAH” cha
Al-Maawardiy.
|