Uongo au kusema uongo ni
miongoni mwa tabia mbaya ambazo muumini wa kweli anapaswa kujiepusha nazo.
Mwenyenyezi Mungu Mtukufu anatuambia:-
"WANAOZUA UWONGO NI WALE
WASIOZIAMINI AYA ZA MWENYEZI MUNGU; NA HAO NDIO WAONGO" ?[16:105]
Kwa mujibu wa aya tabia ya kuzua
uongo ni sifa waliyopambika nayo watu wasiyo waumini, muumini mkamilifu wa
imani hawi muongo. Mtume wa Mwenyezi Mungu aliulizwa: muumini anaweza kuwa
mwoga? Akajibu "Ndiyo(anaweza)" Akaulizwa(tena): anaweza kuwa
bakhili (Muumini)? Akajibu: "Ndiyo." Akaulizwa (tena Muumini)
anaweza kuwa muongo? Akajibu: Hapana Muumini hawi muongo."
Ikiwa Bwana Mtume anaikanusha
Imani kwa mtu mwenye tabia ya kusema uwongo, huo uwongo basi ni nini?
Wanazuoni wanasema: Uongo ni kueleza jambo au kitu kinyume na vile kilivyo
kwa kujua au kutokujua, kwa makusudi au bila ya kukusudia. Bwana Mtume
anasema: "Atakayemwambia mtoto mdogo njoo uchukue (akaja) na asimpe
(kitu) huo ni uongo." Ahmad
Kwa nini mtu anasema uongo.? Nini
sababu ya kusema uongo.? Tabia hii ni mbaya inatokana na maumbile ya
mwanadamu ya kutaka kujivutia manufaa na kujiondoshea madhara kwa hali na
gharama yoyote ile. Mwanadamu anaweza kuona kusema uongo ndiko
kutakakomvua na kumuepusha na janga linalomkabili kama vile kufungwa jela
au kufukuzwa kazi, hapo husema uwongo ili asalimike, pia hulazimika kusema
uongo anapoona kusema ukweli kutamletea madhara kama vile kutoa ushahidi
dhidi ya mzazi wake, ushahidi utakaopelekea ahukumiwe kifo, hapo husema
uongo bila ya kujali kauli ya Bwana Mtume alipotuambia:
"Jilazimisheni (kusema)
ukweli kwani ukweli humuongoza(mtu) katika wema na bila shaka wema
humuongozea (mtu)katika uovu, na uovu (nao) humuongozea motoni na mtu
huandikwa mbele ya Mwenyezi Mungu muongo." Bukhaariy na Muslim
Tabia hii mbaya ya kusema uongo
ina madhara mengi sana kwa mzuaji uongo na kwa jamii kwa ujumla. Muongo
akibainika kwa kudhihiri ukweli, huaibika na kudharauliwa na jamii, pia
hupoteza uaminifu kwa watu na akhera anangojewa na adhabu kali. Mtu muongo
pia husababisha chuki, uhasama na hata ugomvi baina ya watu. Ni kutokana
na madhara haya na mengineyo ndio sababu Uislamu umeikemea vikali tabia
hii mbaya.
iv) KUKAA NA WATU KWA WEMA
Ukiirejea historia utangudua kuwa
kuishi vema na watu au ujirani mwema aliokuwa nao Bwana Mtume ulikuwa ni
sababu ya kuwavuta watu kuingia katika dini ya Mwenyezi Mungu. Bwana Mtume
atuatuambia.
"Mche Mwenyezi Mungu popote
(pale) ulipo na ulifuatishie baya/ovu (ulilolitenda) jema
litakalolifuata(baya) na kaa/ishi na watu kwa tabia njema." Tirmidhiy
Kuishi na watu kwa wema ni pamoja
na :-
- Kuwa mkweli katika kauli na
mtendo kwa wenzio
- Kuwa na bashasha mbele yao
- Kuwa na shukrani kwa wema
wanaokutendea
- Kuwa wa kwanza kuwatolea
salamu kila mkutanapo
- Waite kwa majina mazuri
wayapendayo
- Wataje kwa wema
- Wasamehe waliokukosea
- Linda hadhi na heshima zzao
- Usizifichue siri zao
walizokueleza
- Usijifakharishe mbele zao kwa
hadhi, cheo au utajiri wako
- Shirikiana nao kwa hali na
mali katika huzuni na furaha
- Usiwaudhi kwa kuwafanyia
usilopenda wao kukufanyia
- Waheshimu wakubwa na wahurumie
wadogo
- Wape nasaha/ushauri kwa maneno
mazuri yaliyo laini unapowaona wamepotea
- Usiwabague watu kwa sababu ya
utajiri au umasikini.
Ukiishi na watu kwa kuzingatia
nasaha hizi, utapendwa na jamii na utaishi katika jamii kwa furaha na
amani ya kweli . Bwana Mtume -Allah anamshushie Rehema na Amani -
anatuambia:-
"Miongoni mwa tabia za
mitume na watu wakweli ni bashasha waonanapo na kupeana mikono
wakutanapo."