|
Hakuna mwanadamu
mwenye akili timamu anayeweza kukanusha fadhila za wazazi kwa watoto wao.
Ni ukweli usiopingika kwamba wazazi wawili; baba na mama ndio sababu ya
kuwepo mtoto katika ulimwengu huu. Wazazi wana haki kubwa kwa watoto wao,
kwani ni wao ndio waliowalea watoto wao wakati walipokuwa wadogo
wasiojiweza kwa lo lote. Wao ndio waliopata taabu na dhiki kwa ajili ya
raha, buraha na furaha ya watoto wao, wakikesha kwa ajili ya usingizi wao.
Mama amembeba mwanawe tumboni mwake, akiishi kwa kutegemea chakula
anachokila mama yake kwa kipindi cha miezi tisa kwa ghalibu. Hiki ni
kipindi mpito cha dhiki na adha kubwa kwa mama: “…MAMA YAKE AMEICHUKUA
MIMBA YAKE KWA UDHAIFU JUU YA UDHAIFU…” [31:14]
Kisha baada ya
kujifungua kwa uchungu mkubwa ambao pengine huyagharimu maisha yake. Baada
ya hapo ndipo hufuatia mzigo mzito wa ulezi na unyonyeshaji kwa muda
usiopungua miaka miwili ya taabu, uchovu na shida. Ni kutokana na
kuutambua fika ugumu wa kipindi hiki ndio tukawa na msemo usemao: (Kuzaa
si kazi, kazi kulea). Baba nae kwa upande wake huhangaika huku na kule kwa
ajili ya kuhakikisha kuwa unapata kila ukihitajiacho kwa ajili ya maisha
yako. Ikiwa ni pamoja na elimu, hukushughulikia kwa bidii zisizochoka
mpaka unapokuwa mtu mzima unayeweza kujiendeshea mambo yako mwenyewe. Na
hapo ndipo wazazi wako huendelea kuwa washauri wema, wenye busara na
wakutakiao mema katika maisha yako. Ni kutokana na dhima hii kuu
wanayoichukua wazazi kwa watoto wao. Ndio Allah Mola Mwenyezi akawaamrisha
watoto kuwashukuru na kuwatendea wema wazazi wao: “NA TUMEMUUSIA
MWANADAMU (kuwafanyia ihsani) WAZAZI WAKE. MAMA YAKE AMEICHUKUA MIMBA YAKE
KWA UDHAIFU JUU YA UDHAIFU NA (kumnyonyesha na kuja) KUMUACHISHA KUNYONYA
KATIKA MIAKA MIWILI, YA KWAMBA UNISHUKURU MIMI NA WAZAZI WAKO, MAREJEO
YENU NI KWANGU”. [31:14]
Na akasema tena:
“NA MOLA WAKO AMEHUKUMU KUWA MSIMUABUDU YE YOTE ILA YEYE TU. NA
(ameagiza) KUWAFANYIA WEMA (mkubwa) WAZAZI. KAMA MMOJA WAO AKIFIKIA UZEE
(naye yuko) PAMOJA NAWE, AU WOTE WAWILI, BASI USIWAAMBIE HATA AH! WALA
USIWAKEMEE, NA USEME NAO KWA MSEMO WA HISHIMA (kabisa). NA UWAINAMISHIE
BAWA LA UNYENYEKEVU KWA (njia ya kuwaonea) HURUMA (kwa kuwaona wamekuwa
wazee). NA USEME: MOLA WANGU! WAREHEMU (wazee wangu) KAMA WALIVYONILEA
KATIKA UTOTO”. [17:23-24]
Ni wajibu wako bali
ni sehemu ya dini wewe kuwatendea wema wazazi wako, huku ukikiri kuwa ni
haki yao. Uwatendee wema kwa kauli na amali kwa kutumia mwili, mali na
kila ukimilikicho huku ukiamini pasi na shaka kwamba wewe na kila
ulichonacho ni mali ya wazazi wako. Utekeleze amri yao muda wa kuwa si
katika kumuasi Allah na katika lile ambalo ndani yake unaweza kufikwa na
madhara: “NA (wazazi wako) WAKIKUSHURUTISHA KUNISHIRIKISHA NA (yale)
AMBAYO HUNA ILIMU NAYO, USIWATII; LAKINI KAA NAO KWA WEMA HAPA DUNIANI (
maadamu ni wazee wako, ila usiwafuate tu mwendo wao mbaya). SHIKA NJIA YA
WALE WANAOELEKEA KWANGU, KISHA MAREJEO YENU NI KWANGU, HAPO NITAWAAMBIENI
MLIYOKUWA MKIYATENDA”. [31:15]
Zungumza na wazazi
wako kwa kauli laini, wakunjulie uso wako unapozungumza nao. Uwatumikie
upeo wa uweza wako kama wanavyostahiki. Usione kero na udhia wanapofikia
hali ya utu uzima, hali ambayo ina mtihani mkuu unaohitajia subira kubwa.
Wauguze wanapougua na wala usione uzito kuwasafisha pale inapobidi. Kwani
kumbuka na wewe umezaa na pengine utafikia hali hiyo ya utu uzima na
kuhitajia msaada wa watoto wako kwa karibu. Msaada uliojaa huruma na
mapenzi kama wanavyohitajia wao kwako hivi sasa. Kwa hivyo watendee wema
wazazi wako leo ili Allah awatume wanao kukutendea wema kesho. Kumbuka
ukiwatupa wazazi wako leo, nawe kesho utatupwa na wanao. Kwani kama
utendavyo ndivyo utakavyotendewa pengine na kuzidi.
Elewa na ufahamu ewe
ndugu yangu kwamba Allah ameipa haki ya wazazi daraja ya juu kabisa. Baada
ya haki yake YEYE na Mtume wake, inayofuatia ni haki ya wazazi:
“MUABUDUNI ALLAH WALA MSIMSHIRIKISHE NA CHO CHOTE NA WAFANYIENI IHSANI
WAZAZI WAWILI…” [4:36]
Na akasema tena:
“…YA KWAMBA UNISHUKURU MIMI NA WAZAZI WAKO…” [31:14]
Amesema Ibn
Abbas-Allah amuwiye radhi: “Aya tatu zimeshuka zikikutana na mambo
matatu, Allah halikubali moja bila ya (kupatikana) mwenziwe;
Ya kwanza ni kauli
yake Allah: “ENYI MLIOAMINI! MTIINI ALLAH NA MTUME WAKE…” [4:59]
Basi atakayemtii
Allah bila ya kumtii Mtume wake, twaa yake hiyo ya kumtii Allah
haitokubaliwa ila amtii na Mtume.
Ya pili ni kauli
yake Allah: “NA SIMAMISHENI SWALA NA TOENI ZAKA…” [2:110]
Basi atakayeswali
bila ya kutoa zaka (na ilhali uwezo anao), swala yake hiyo haitakubaliwa.
Ya tatu ni kauli
yake Allah: “…YA KWAMBA UNISHUKURU MIMI NA WAZAZI WAKO…” [31:14]
Basi atakayemshukuru
Allah na akaacha kuwashukuru wazazi wake, shukurani zake hizo
hazitakubaliwa”.
Hili ndilo
lililomfikisha Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kusema: “Radhi ya
Allah imo ndani ya radhi ya wazazi na ghadhabu ya Allah imo ndani ya
ghadhabu ya wazazi”.
Ikutoshe kuiona
hadhi na daraja ya wazazi wako kwamba Mtume wa Allah ameutanguliza wema wa
wazazi juu ya jihadi katika dini ya Allah. Imekuja katika hadithi ya Ibn
Masoud-Allah amuwiye radhi-amesema: Niliuliza ewe Mtume wa Allah ni amali
gani ipendezayo zaidi kuliko zote mbele ya Allah? Akajibu: Kuswali swala
kwa wakati wake (uliowekwa na sheria). Nikauliza (tena) kisha inafuatia
amali ipi? Akajibu: Kuwatendea wema wazazi wawili. Nikauliza (tena) kisha
ipi? Akasema: Kupigana jihadi katika dini ya Allah”. Bukhaariy &
Muslim
Kauli hii ya Bwana
Mtume katika hadithi yake hii inonyesha umuhimu wa haki ya wazazi. Haki
ambayo leo imetupwa na kuachwa kutekelezwa na watoto wengi ambao
wamewakata pande wazazi wao sambamba na kuwaasi. Leo sio ajabu tena
kumuona mtoto akiwadharau na kuwafedhulikia wazazi wake. Hawajali na
pengine kufikia hata hatua ya kuwatukana huku akijisifu kuwa amewapa
vidonge vyao. Leo haishangazi tena kumuona mtoto akimpiga mzazi wake.
Mwingine huthubutu hata kusema msinibabaishe eti kwa sababu tu ya kunizaa,
kwani hata mimi ningetangulia ningeweza kukuzaeni, kwani kuzaa ni kazi!
Ebo! Allah Mola Mwenyezi anakukataza kuwaambia wazazi wako hata neno (ah!)
achilia mbali kuguna au kuwafokea, seuze kuwaambia maneno mabaya hayo!
“NA AMBAYE ANAWAAMBIA WAZAZI WAKE: KEFULE NYIE! OH! MNANITISHIA KUWA
NITAFUFULIWA; NA HALI KARNE NYINGI (watu wengi) ZIMEKWISHA PITA KABLA
YANGU (wala hazikufufuliwa)? NA HAO (wazee wake) WAWILI HUOMBA MSAADA WA
ALLAH (na humwambia mtoto wao): OLE WAKO! AMINI (haya unayoambiwa), HAKIKA
AHADI YA ALLAH NI KWELI. LAKINI YEYE HUSEMA: HAYAKUWA HAYA (mnayoyasema)
ILA NI VISA VYA WATU WA KALE (tu si maneno ya kweli). HAO NDIO AMBAO
IMELAZIMIKA HUKUMU JUU YAO (ya kutiwa motoni)…” [46:17-18]
Acha ujuvi, kumbuka
kuwatendea wema wazazi wako ni kwa faida na maslahi yako mwenyewe. Na
kuacha kufanya hivyo, haiwi ila ni kwa maangamivu ya nafsi yako. Hebu
tuitegee pamoja kauli hii ya Mtume wetu-Rehema na Amani zimshukie-sikio la
usikivu na mazingatio: “Atakayependa kurefushiwa umri wake na
kuzidishiwa riziki yake, basi na awatende wema wazazi wake na awaunge
ndugu zake”. Ahmad
|