|
I/. HAKI NA WAJIBU…..I
Muislamu kujua haki na wajibu wake kwa Mola Muumba wake na
viumbe wenzake ni tabia isiyopambanuka naye. Ni fardhi isiyo na shaka
muislamu kuzijua haki zake na kuzidai pake anapozikosa. Na kuujua wajibu
wake ili autekeleze kwa kadri ya uweza wake kama inavyompasa.
Neno “haki” ni dhana pana kabisa yenye maana adida
(nyingi) kulingana na itakavyotumika, mahaka itumikapo na mtumiaji wa
dhana hii. Katika somo letu hili tutaliarifisha neno haki kuwa: Ni ile
hali/jambo lililolazimu katika dhima. Ama kwa neno “wajibu”
tunakusudia jambo/tendo linalomlazimu mtu kulitekeleza ili kujitoa katika
dhima ya utekelezaji wake.
Maisha ya muislamu yamesheheni na kutawaliwa na hisia za
majukumu ambazo humpelekea na kumsukuma kutekeleza wajibu ulio katika
dhima yake. Ni kwa kuutekeleza wajibu wake kwanza ndio muislamu hustahiki
kupata/kudai haki yake. Kwani ni vema tukakumbuka na kutia akilini kwamba
hakuna haki bila ya wajibu. Haki ya mwanzo kabisa ambayo muislamu anapaswa
kuijua na kuitekeleza ni haki ya Allah Muumba kwa waja wake; watumwa wake.
Hii ni haki ya Mola Mwenyezi ambaye amekutoa kutoka ambako hukuwa kitu
kinachotajwa. Haki ya Allah Mola Mlezi ambaye amekulea kwa neema zake
ulipokuwa tumboni mwa mama yako. Ambamo hakuna ye yote anayeweza
kukufikishia chakula chako na kila ukihitajiacho kwa ajili ya maisha yako
hayo, yanayopitia katika viza vitatu. Ni haki yake YEYE aliyekufanyia haya
na mengi yasiyodhibitika na akili yako. Akayafanya yote hayo kwa fadhila
na ihsani yake, kwa hivyo ni wajibu wako kuikabili ihsani yake hii
Umpwekeshe katika uungu, ibada na sifa zake (Tauhiyd).
Umtakasiye dini YEYE peke yake (Ikhlaaswi).
Umuabudu YEYE pekee bila ya kumshirikisha na cho chote.
Tusome na tuzingatie: “NA MUNGU WENU NI MUNGU MMOJA TU,
HAKUNA ANAYESTAHIKI KUABUDIWA ILA YEYE AMBAYE NI MWENYE KUNEEMESHA NEEMA
KUBWA KUBWA NA MWENYE KUNEEMESHA NEEMA NDOGO NDOGO”. [2:163]
Ufuate na kuzitii sheria zake zote.
“KISHA TUMEKUWEKA JUU YA SHERIA YA AMRI YETU, BASI
IFUATE, WALA USIFUATE MATAMANIO YA WALE WASIOJUA (kitu)”. [45:18]
“ENYI MLIOAMINI! INGIENI KATIKA HUKUMU ZA UISLAMU ZOTE,
WALA MSIFUATE NYAYO ZA SHETANI, KWA HAKIKA YEYE KWENU NI ADUI DHAHIRI”.
[2:208]
Utekeleze maamrisho yake na ujiepushe na makatazo yake.
Umfuate na kumtii Mtume wake.
“SEMA: IKIWA NYINYI MNAMPENDA ALLAH, BASI
NIFUATENI…” [3:31]
Na kwa ujumla utekeleze yale yote ambayo yatathibitisha
maana ya uja na utumwa wako kwa Allah Mola Muumba wako.
Naye Allah kwa upande wake amejipangia mwenyewe kwa
fadhila na ukarimu wake kuwalipa waja wake watakaoyatekeleza hayo
malipo/jazaa adhimu na kuwaepusha na adhabu yake. “…NA ANAYEMTII ALLAH
NA MTUME WAKE, (Allah) ATAMUINGIZA KATIKA BUSTANI ZIPITAZO MITO MBELE
YAKE, WAKAE HUMO MILELE. NA HUKO NDIKO KUFAULU KUKUBWA.” [4:13]
2- HAKI YA MTUME WA ALLAH.
Haki ya pili ambayo muislamu anatakiwa aijue na
kuitekelezea wajibu wake ni haki ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie. Hii ndio haki kubwa na tukufu katika haki za viumbe. Kwani ni
ukweli usiopingika kwamba hakuna haki kubwa baada ya haki ya Allah, kuliko
haki ya Mtume wake. Allah anatuambia: “HAKIKA TUMEKULETA UWE SHAHIDI NA
MTOAJI WA KHABARI NJEMA NA MUONYAJI. ILI MUMUAMINI ALLAH NA MTUME WAKE, NA
MUMTUKUZE NA MUMUHISHIMU…” [48:8-9]
Ni kwa ajili hii ndio ikawa ni wajibu kwa muumini
kuyatanguliza mbele mapenzi ya Mtume juu ya mapenzi ya watu wote. Ampende
mtume zaidi kuliko mke, mali, mtoto, mzazi na hata nafsi yake. Katika hili
Mtume wa Allah-Rehma na Amani zimshukie-anatuambia: “Haikamiliki imani
ya mmoja wenu mpaka niwe mimi (Mtume) ni kipenzi mno kwake yeye kuliko
mwanawe, mzazi wake na watu wote”. Bukhaariy & Muslim.
Miongoni mwa haki za mtume wa Allah kwako wewe muislamu ni
kumkubali, kumuadhimisha na kumuhishimu hishima inayolingana na daraja
yake tukufu. Bila ya kuvuka mipaka na kumtoa katika uanadamu na kumpa sifa
ya uungu kama walivyofanya manaswara kwa Nabii Isa. Kumkubali mtume katika
uhai wake ni kuukubali na kuufuata mwendo wake (sunah) na khulka zake
(tabia). Na kumuhishimu na kumtukuza baada ya kufa kwake ni kushikamana na
mwenendo na sheria yake aliyotuletea kutoka kwa Mola wake. Mtu
atakayebahatika kusoma jinsi maswahaba-Allah awawiye
radhi-walivyomuhishimu na kumtukuza Mtume wa Allah. Atatambua ni namna
gani mabwana hawa watukufu walivyoutekeleza wajibu wao kwa Mtume wao.
Baada ya kutambua haki zake zinazowapasa wao kumtekelezea.
Alisema Urwah Ibn Masoud kuwaambia Makurayshi wenzake
wakati walipomtuma kuzungumza na Mtume katika suala la suluhu katika kisa
cha Hudaybiyah, akasema: “Nimeingia kwa wafalme (akina) Kisra, Qayswar
na Najaash, sikupata kumuona ye yote akiadhimishwa mithili ya maswahaba wa
Muhammad wanavyomuadhimisha Muhammad. Alikuwa akiwaamrisha jambo
hukimbizana kuitekeleza amri yake hiyo. Na akitawadha hukurubia kuuana kwa
kugombea maji yatokanayo na udhu wake. Na anapozungumza, hushusha sauti
zao mbele yake na hawakupata kumkazia macho kwa kumuangalia kwa ukubwa wa
kumuadhimisha kwao”. Namna hivi ndivyo walivyokuwa maswahaba-Allah
awawiye radhi-wakimuadhimisha na kumtukuza Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie. Walifanya hivyo pamoja na kuwa tayari Allah alishamuumba na
kumfinyanga Mtume wake kwa tabia njema, ulaini na wepesi wa nafsi. Tabia
hizi za Mtume zilitoa msaada mkubwa uliowawezesha maswahaba kumuadhimisha
na kumuhishimu, kwani Mola wake anamwambia: “…NA KAMA UNGEKUWA MKALI
NA MWENYE MOYO MGUMU BILA YA SHAKA WANGALIKUKIMBIA…” [3:159]
Na katika jumla ya haki za mtume kwa muumini ni
kumsadikisha katika mambo yote aliyoyatolea khabari; yaliyopita na yale
yajayo. Na kuyatekeleza aliyoyaamrisha kutendwa na kukatazika na kuyaacha
yote aliyoyakataza na kuyakemea. Na kuamini kwamba uongozi wake ndio
mkamilifu wa miongozo yote na sheria yake ndio timilifu ya sheria zote. Na
isitangulizwe sheria yo yote juu ya sheria yake: “NAAPA KWA (haki ya)
MOLA WAKO, WAO HAWAWI WENYE KUAMINI (kweli kweli) MPAKA WAKUFANYE (wewe
ndiye) HAKIMU (muamuzi) KATIKA YALE WANAYOKHITALIFIANA. KISHA WASIONE
UZITO NYOYONI MWAO JUU YA HUKUMU ULIYOTOA NA WANYENYEKEE KABISA”. [4:65]
Na miongoni mwa kumuhishimu na kumtukuza Bwana mtume ni
kuitetea na kuilinda sheria na muongozo wake. Kwa upeo wa uweza wa mtu kwa
mujibu wa hali na mazingira yalivyo. Ikiwa adui anaishambulia sheria ya
mtume kwa hoja, basi jawabu tosha la mashambulizi ya aina hii ni elimu na
hoja zitakazoziponda hoja za adui. Na kumbainishia ulemavu wa hoja zake,
na wala sio matumizi ya nguvu. Na kama anahujumu kwa silaha, basi nasi
tupambane naye kwa silaha: “BASI WAANDALIENI (wawekeeni tayari) NGUVU
MZIWEZAZO (silaha)…” [8:60]
Haimfalii muumini wa kweli kusikia sheria ya Mtume au
hishima yake ikivunjwa, naye akae kimya tu bila ya kuchukua hatua yo yote
na ilhali ana uwezo wa kurudi: “NAYE AMEKWISHA KUTEREMSHIENI KATIKA
KITABU (hiki) YA KWAMBA MNAPOSIKIA AYA ZA ALLAH ZINAKATALIWA NA KUFANYIWA
STIHZAI, BASI MSIKAE PAMOJA NAO…” [4:140]
|