|
"Riyaa" ni miongoni mwa tabia mbaya ambazo
muislamu anatakiwa bali anawajibika kujiepusha nayo ili aweze kufikia
uhalisi na ukamilifu wa ibada zake. Riyaa ni maradhi hatari ya moyo,
kirusi hiki hatari huishambuliwa ikhlasi na kuiondosha kabisa katika moyo
wa mja. Mja akikosa ikhlasi huwa amekosa bima (kinga) ya ibada zake na
hivyo kutoa mwanya wa kushambuliwa ibada zake hizo na mdudu mbaya "riyaa".
Riyaa ina athari mbaya kwa mja kwani itazifanya ibada zake hizo siku ya
kiama itafanya kama mavumbi yapeperushwayo na upepo. Riyaa itamfanya mtu
awe muflis awe hana malipo yoyote mbele mola wake. Hapa ndipo unajitokeza
umuhimu wa kuibainisha tabia hii mbaya ili Muislamu aijue na akishaijua
aiepuke upeo wa uwezo wake. Hebu sasa na tujiulize "riyaa" ni
nini ili tuweze kufuatana pamoja.
"Riyaa" hii ni isimu (nomino) itakanayo na lugha
ya kiarabu. Isimu hii ya "riyaa" ikatafsiriwa kuwa ni kufanya
abada (amali njema) kwa lengo la kuwaonyesha watu ili :
- uonekane kuwa ni mwema kuliko ulivyo
- upate kupendeza machoni mwao
- upate maslahi fulani kutoka kwao (mali au cheo)
Kwa ibara sahihi tunaruhusika kusema kuwa "riyaa"
ni kufanya ibada kwa ajili tu ya kuwaonyesha watu na si kwa ajili ya
Allah: hiyo ndiyo tabia mbaya ya riyaa tunayokusudia hapa kwa lengo la
kukutanabaisha ili uweze kuiepuka maana hiyo ya riyaa unaweza kuiona kwa
kuipitia kauli ya Allah:" NA AMBAO WANATOA MALI ZAO KWA KUONYESHA
WATU (riyaa) WALA HAWAAYAMINI (aliyoyasema) ALLAH WALA SIKU YA MWISHO......(4:38)
".... NA WANAPOSIMAMA KUSWALI HUSIMAMA KWA UVIVU,
WANAONYESHA WATU (kuwa wanaswali) WALA HAWAMTAJI ALLAH HATA KIDOGO "
(4:142)
Riyaa ni kinyume cha ikhlasii, kwa kweli huu ni dharura
kuwa pasipo na ikhlaswi pana riyaa tu na si vinginevyo na palipo na riyaa
bila shaka hapana ikhlaaswi hapo. Muislamu hafanyi ibada zake kwa riyaa
wala riyaa si sifa yake, bali muislamu hufanya ibada zake zote kwa
ikhlaswi akiiteekeza amri ya mola wake:" WALA HAWAKUAMRISHA ILA KWA
KUMUABUDU ALLAH KWA KUMTAKASIA DINI (ikhlaswi)...." (98:5)
"SEMA MOLA WANGU AMEAMRISHA UADILIFU NA (ameniambia
nikuambieni) ELEKEZENI NYUSO ZENU(kwake) WAKATI WA KILA SWALA NA MWABUDU
YEYE TU KWA UTII HALISI (ikhlaswi)...." (7:29)
Muislamu hujiepusha na riyaa kwa sababu anamini kuwa
kumfanya riyaa ni kumshirikisha Allah kwa mujibu wa kauli ya mtume wa
Allah rehma na amani zimshukie:" uchache wa riyaa ni shirika
...." Ibn Maajah, Al Hakim na Bayhakiy.
Inamtosha Muislamu kuona ubaya ya maradhi haya hatari ya
riyaa na kujiepusha nayo kwa kupata chanjo ya ikhlaswi, kuwa Allah na
mtume wake wanaichukia riyaa na Allah amewaandalia adhabu kali wale wote
wafanyao amali zao kwa riyaa tusome:"BASI ADHABU ITAWATHUBUTIKIWA
WALE WANAOSALI AMBAO WANAPUUZA (maamrisho ya) SWALA ZAO;AMBAO HUFANYA
RIYAA (hufanya amali zao ili watu wawaone tu)" (107:4 - 7)
Mwenye kufanya riyaa katika amali zake huwa hana chembe ya
ujira wa amali hizo mbele ya Allah zaidi ya kuonekana na hao anaowaonyesha
amali zake na kumjazia sifa kwa makilo. Riyaa ni sababu ya kubatilika
amali (ibada) ya mja kama inavyobainisha kaili hii tukufu ndani ya kitabu
kitukufu:" ENYI MLOAMINI MSIBATILISHE (thawabu za) SADAKA ZENU KWA
MASUMBULIZI YA UDHIA KAMA YULE ANAYETOA MALI YAKE KWA KUJIONESHA MBELE YA
WATU (riyaa) WALA HAMUAMINI ALLAH, WALA SIKU YA MWISHO. BASI HALI YAKE NI
KAMA HALI YA JABALI AMBALO JUU YAKE KUNA UDONGO, KISHA IKALIFIKIA (jabali
hili) MVUA KUBWA (ikasukuma udongo wote huo) NA IKALIACHA TUPU. BASI
HAWATAKUWA NA UWEZO (wa kupata) CHOCHOTE KATIKA WALIVYOVICHUMA NA ALLAH
HAWAONGOZI WATU MAKAFIRI" (2:264)
Allah Subhanahu Wata’alah haitaki wala hana haja na
amali yoyote ambayo mja ataofanya kwa kumshirikisha yeye na viumbe. Hivi
ndivyo anatuambia katika hadithi-qudsi :"atakayefanya amali na
akamshirikisha mwingine (asiye mimi) katika amali hiyo. basi amali hiyo ni
yake yote (huyu mwingine) nami hujitenga mbali nayo (amali hiyo), nami
mkwasi kuliko wakwasi wote na shirika." Muslim.
Riyaa ni adui mkubwa wa ibada na amali yako yote, ili
kubainisha ubaya wake, Bwana Mtume rehma na amani zimshukie akiita kuwa ni
"shirki ndogo" akasem: HAKIKA NILICHELELEALO (niliogopeayo)
KWENU KULIKO YOTE NI SHIRKI NDOGO. (maswahaba) WAKAMUULIZA: EWE MTUME WA
ALLAH-NI IPI HIYO SHIRKI DOGO? AKAMJIBU NI RIYAA, Mwenyezi Mungu mtukufu
atasema siku ya kiama atakapokuwa anawalipa waja (wake) kwa mujibu wa
amali zao: waendeni wale mliokuwa mkiwaonyesha amali zenu ulimwenguni,
muone kama mtapata malipo (jazaa) kwao".
SURA (MAENEO) ZA RIYAA:
Riyaa hujidhihirisha katika sura kadhaa, tutazibainisha
baadhi ya surah hizo ili mtu asije akatumbukia ndani ya janga hili bila ya
kujijua.
1) Mja kuzidisha twaa, pale anaposifiwa mfano anaposoma
quran watu wakamsifia kama anasoma vizuri hapo hupata kichwa na kuzidisha
kusoma kwa juhudi, za makusudi ili kuwaonyesha watu kuwa yeye ndiye
mwenyewe kwa usomaji wala kama yeye hapana. Hufanya hivyo akilenga kuzidi
kusifiwa. Hii ni riyaa jitahidi kuiepuka kwani haina faida hata kidogo
nawe.
2)mtu kuwacha kufanya ibada au amali yoyte ya kheri kwa
sababu amekosolewa katika utendaji wake au hakusifiwa. Kuacha kuendelea na
amali ya twaa, eti kwa sababu hakusifiwa hiyo ni ushahidi dhahiri kuwa
hamkumsudia Allah-mlipaji bali viumbe wasio na cha kukulipa. Hii ni sehemu
ya maradhi ya riyaa jikinge nayo.
3)kufanya ibada kwa nguvu bidii, furaha na nyeyekevu
mkubwa anapokuwa mbele ya watu lakini anapokua pekee ibada ile ile
huifanya kwa uvivu na haraku haraka kama mtu amelazimishwa. Hii pia ni
riyaa inaonyesha dhahiri kwamba amali yako hiyo huwa unaifanya ili upate
kuambiwa kwamba wewe ni mcha Mungu na hao wanaokuzunguka wakati huo lakini
unapokua faraghani wewe na mola wako pekee hufanyi ibada kama vile
unavyofanya mbele ya watu
4)mtu kutoa sadaka katika mazingira ambayo lao
asingekuwepo mtu fulani watakao muona akitoa, basi asingelitoa hiyo nayo
riyaa kwa sababu hutoi kwa ajili ya mola wako bali unatoa ili uonekane na
akina fulani. Watakusaidia nini hao kina fulani mbele ya Allah? “KWA
YAKINI HAO HAWATAKUFAA LOLOTE MBELE YA ALLAH……” (45:19)
5)mtu kusema maneno ya haki au ya kheri au kutenda matendo
mema ambayo dhahiri yake ni kuwa anafanya kwa ajili ya Allah, na hivo
ndivyo watu wanavyomuona kwa sababu anajitokeza mbele ya watu lakini
batini yake sivyo hivyo yeye anayafanya yote haya kama ngazi tu ya kupatia
haja zake kwa watu. Hii pia ni riyaa tahadhari nayo.
Hii ndiyo riyaa, adui wako atakayekufanya wewe uwe muflis
siku ya kiama kama hujamkana na kumuepuka leo. Imepokelewa kutoka kwa Abu
Hurayrah- Allah amiwiye radhi. Amesema : nilimsikia Mtume wa Allah rehma
na amani zimshukie amesema “mtu wa mwanzo atakayehukumiwa siku ya kiama
ni mtu aliyeuwawa shahidi. (ataletwa mbele ya Allah) na atamtambulisha
neema zake alizomneemesha nazo duniani nae azitambue (neeme hizo) kisha
amuambie umefanya nini kwa neema hizo nilizokupa? Atajibu: nilipigania
dini yako mpaka nikafa shahidi. (Allah) atamuambia umeogopa wewe ulipigana
ili uambiwe wewe ni jasiri, na ulikwishaambiwa (ulishalipata hilo). Kisha
ataamrishwa akokotwe kiusouso mpaka motoni.(na atakayehukumiwa mwanzoni ni)
mtu aliyejfunza elimu na akaifundsha na akasoma Quran atamleta na
atamtambulisha neema zake nae atazitambua. Kisha amuambie: umefanyia nini
neema hizo?akajibu: nilijifunza elimu na nikaifundisha elimu na nukasoma
Quran kwa ajili yako. (Allah) atamuambia: umeogopa, wewe ulijifunza elimu
ili uambiwe mwanachuoni (una elimu) na ulisoma Quran ili uambiwe msomaji
na yote hayo ulishaambiwa kisha ataamrishwa akokotwe kiusouso mpaka motoni,
na mtu ambaye Allah amemkunjulia namna kwa namna za mali ataletwa na
atamtambulisha neema zake naye azitambue, atamuuliza; umefanya nini kwa
neema hizi atajibu: sikuiacha njia yoyoyte unayopenda mtu atoe katika (njia)
hiyo ila nilitoa. Atamuambia: umeongopa, wewe ulifanya yote hayo ili
uambiwe kuwa ni karimu na tayari ulishaambiwa. Kisha atamuamrisha aburuzwe
kiusouso mpaka motoni” muslim.
|