|
Ghushi ni nini
?
Ifahamu ghushi
kupitia hadithi hii :
Imepokelewa
kwamba Mtume -Rehema na Amani zimshukie-alilipitia rundo la chakula
(sokoni), akaingiza mkono wake ndani yake (rundo hilo) vidole vyake
vikapata ubichi ubichi. (Mtume) akauliza : Nini hiki ewe muuza chakula ?
Akajibu : Kimepatwa na mvua, ewe Mtume wa Allah. (Mtume) akasema : Kwa
nini basi usikiweke kilicholowa juu ili watu wakione ? Atakayetughushi si
katika sisi" Muslim na Tirmidhiy.
Hii ndiyo
ghushi tunayokusudia, kwa mujibu wa hadithi tunaweza kuieleza ghushi kuwa
ni aina fulani ya udanganyifu unaofanywa katika biashara au katika jambo
jingine. Udanganyifu huu unalenga kuficha aibu/kasoro iliyomo ndani ya
bidhaa au kuchanganya bidhaa safi na ile mbovu na kuiuza kwa thamani ya
bidhaa safi. Ghushi pia inahusisha uchanganyaji wa makusudi nafaka kama
mchele na mchanga kwa lengo la kuongeza uzito au uchanganyaji wa maziwa na
maji ili kuongeza ujazo. Aina hii ya ghushi inabainishwa na hadithi
ifuatayo :
Imepokelewa
kwamba swahaba wa Mtume, Abuu Hurayrah - Allah amuwie radhi - alipita
katika kitongoji kimoja, akamuona mtu mmoja amebeba maziwa akiyauza. (Abuu
Hurayrah) akayachunguza na kugundua amechanganya na maji. Abuu Hurayrah
akamwambia : Utakuwaje utakapoambiwa siku ya Kiyama yatoe maji katika
maziwa (utaweza) ? Al-Baihaqiy.
Muislamu ni mtu
mwenye kuishi kwa kufuata sheria za Allah, hambughudhi mtu wala yeye
hayuko tayari kubughudiwa. Kama huyu ndiye muislamu basi haimpitii akilini
na haimuelei kabisa kuwa na tabia ya ghushi, akipita huku na huko
akiwadanganya watu na kula mali zao kwa njia za dhulma. Hii ni tabia
mbaya, Allah haipendi na anaikemea vikali kabisa : "WALA MSILIANE
MALI ZENU KWA BATILI ... [2:188]
Ukijikuta
umepambika na mojawapo wa mambo yafuatayo, basi jihesabu tayari
umeshaathiriwa na tabia mbaya ya ghushi. Tabia hii ya ghushi inakupelekea
kukanwa na Mtume na kukutoa katika kundi lake : "Atakayechukua silaha
dhidi yetu, si katika sisi, na atakayetughushi, basi si miongoni
mwetu" Muslim. Sasa hebu jikague wewe mwenyewe kupita mambo
yafuatayo, utapata jibu je, ni katika sisi au si miongoni mwetu ?
1. Je, una
tabia ya uhodari wa kumpambia mtu kitu kibaya mpaka akakiona kuwa ni
kizuri, au shari akaiona kuwa ni wema na akatumbukia humo ? Hii ni ghushi
inayokufanya uwe mtu mbaya kiasi cha kutengwa na Bwana Mtume.
2. Je, una
tabia na ustadi wa kuficha aibu/kasoro ya bidhaa unayoiuza kwa mteja hali
ya kuwa unajua dhahiri kuwa lau angeliiona aibu hiyo, asingenunua bidhaa
hiyo kabisa au angeinunua kwa kuwa ana haja lakini si kwa bei hiyo
unayomuuzia sasa. Hii nayo ni ghushi, inakuondoshea baraka katika biashara
na maisha yako kwa ujumla. Jiepushe nayo.
3. Je, una
tabia na mbinu za kujidhihirisha mbele za watu kinyume na ulivyo, kiasi
cha kwafanya watu wakuamini kuwa ndivyo ulivyo ? Hii pia ni aina fulani ya
ghushi itakayokufanya uchukiwe na kutengwa na jamii pindi ukweli
utakapobainika bayana na uongo kujitenga mtengano.
4. Je, una
tabia na ufundi wa kumfurahisha mtu kiasi cha kumuaminisha kuwa wewe ni
mtu mwema, halafu ukaitumia fursa hiyo uliyoitengeneza kumghuri kwa lengo
la kufikia maslahi yako ? Hii kama sio ghushi ni nini basi ? Hebu achana
na tabia mbaya hii kwani mwisho wake ni kuumbuka na kupoteza hadhi machoni
kwa jamii.
5. Je,
umeaminiwa na mtu kwa mkewe au wanawe na mali yake na akakueleza siri zake
? Halafu wewe ukamzunguka na kumfanyia khiyana kwa mkewe huyo ambaye ni
shemeji yako, au wanawe hao ambao wewe daraja yako mbele yao ni baba ? Au
ukamkhini katika mali yake na ukafichua siri zake ? Kama uko hivyo, fahamu
kwamba hiyo ni sehemu ya tabia mbaya ya ghushi, je, wewe ukitendewa hivyo
kwa mkeo, wanao, mali au siri zako, utafurahi ? Kama hufurahi, basi na
mwenzio naye hafurahi kama ambavyo Allah na Mtume wake wasivyolifurahia
hilo.
6. Je, una
maarifa ya kutengeneza fedha bandia au madini bandia na kisha kuzitumia
fedha hizo au kuwauzia madini hayo wenzio ? Huko ni kula mali ya watu kwa
batili na ni ghushi.
Hii ni sehemu
tu ya sura pana ya tabia na maradhi mabaya ya ghushi. Haya ni maradhi
mabaya kabisa, kwa sababu yatakufanya :
i) Upoteze
hadhi na heshima yako.
ii) Udharauliwe
na kupuuzwa.
iii) Usiaminiwe
hata kidogo na hivyo kukosa msaada wa jamii hata katika shida.
iv) Uchukiwe na
uonekane kuwa ni mtu mbaya usiyefaa kuwa karibu na jamii.
v) Upoteze
baraka katika shuguli zako kutokana na manung'uniko ya watu juu yako.
vi) Ujitoe
mwenyewe kwa khiyari yako katika kundi la Mtume.
vii) Ustahiki
kutendewa kama unavyotendewa wenzio.
viii) Utengwe
na jamii na kusababisha kukosa ushirikiano wao wa karibu.
Ili ujikinge na
maradhi haya mabaya na ujiepushe kufikwa na mambo tuliyotaja hapo juu, ni
wajibu wako :
a) Kama ni
mfanyabiashara, kubainisha aibu/kasoro ya bidhaa yako kwa mnunuzi/mteja
wako ili awe na khiyari ya kununua pamoja na aibu hiyo au kuacha kununua.
Kama hukufanya hivyo, Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie - anakuambia
: "Yeyote atakayeuza kitu hali ya kuwa kina aibu (kasoro) bila ya
kuibainisha (kasoro hiyo kwa mteja), ataendelea kuwa katika chuki ya Allah
na malaika wataendelea kumlaani (mpaka aache)" Ibn Maajah.
b) Kama mtu
kando kumfahamisha mtu anayetaka kuuziwa kitu kibaya; chenye kasoro kuwa
kitu hicho kina kasoro kadha wa kadha. Kwa kufanya hivyo utajiepushia
dhima mbele ya Allah ya kumuona mtu anadhulumiwa na ukaacha kumsaidia kwa
kuogopa watu. Tambua : ".... ALLAH NDIYE MWENYE HAKI ZAIDI YA
KUOGOPWA ...." 33:38.
c) Utakapomuona
mtu amekuja kuposa na ukawa unajua wazi si kwa chuki binafsi kwamba mtu
huyo ana kasoro katika mwenendo, tabia na dini yake. Si majungu wala
fitina kuwaendea wazazi wa binti na kuwaeleza kwa nia njema juu ya huyo
mposaye binti yao. Ili waamue ama kumuoza pamoja na uchafu wake wa tabia
kwa tamaa ya anachomiliki au waache kumuoza kwa ajili ya kuheshimu
muongozo wa Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie - Atakapokujieni
(kuposa) mnayemridhia dini na tabia zake, basi muozeni ..."
d) Utakapomuona
mtu anataka kushirikiana na mtu katika biashara au jambo lolote lile na
ukajua kwamba huyo anayetaka
kushirikiana naye si mtu muaminifu. Ni vema ukamueleza kwa njia ya hekima
na ushauri kwani kama hukufanya hivyo nawe utahesabika kuwa ni mshirika
katika madhara yote yatakayomkumba kutokana na ushirika huo wa mtu mbaya.
Kumbuka Mwenyezi Mungu anatuagiza : "... NA SAIDIANENI KATIKA WEMA NA
TAQ-WA, WALA MSISAIDIANE KATIKA DHAMBI NA UADUI NA MCHENI ALLAH, HAKIKA
ALLAH NI MKALI WA KUADHIBU" [5:2]
|