|
Muislamu
hadhulumu na wala hadhulumiwi. Yeye hamdhulumu mtu kwa kigezo cho chote kile,
hata kama anatofautiana nae katika imani. Wala hakubali kudhulumiwa na ye
yote awaye. Hii ni kwa sababu dhulma kwa aina zake zote imeharamishwa na kukaripiwa
vikali kabisa ndani ya Qur-ani tukufu na suna ya mtume (hadithi) Tusome
pamoja kwa mazingatio:-
“---
MSIDHULUMU WALA MSIDHULUMIWE.” [ 2 : 279]
“---
NA ATAKAYEDHULUMU MIONGONI MWENU TUTAMUONJESHA ADHABU KUBWA.” [25 : 19]
“---
NA ALLAH HAWAPENDI MADHALIMU.” [3 : 57]
Na
Allah amesema tena katika hadithi Qudsi. “Enyi waja wangu, hakika mimi
nimejiharamishia dhulma na nimeifanya (dhulma) kuwa ni yenye kuharamishwa
baina yenu, basi msidhulumiane.” Muslim.
Mtume
wa Allah Rehema na Amani zimshukie anatahadharisha juu ya dhulma, anasema:
Iogopeni/jiepusheni na dhulma, kwani hakika dhulma ni viza siku ya kiyama
---“ Muslim
Eeh!
Utukufu ulioje wa dini hii ya uislamu; dini ya haki, uadilifu na usawa.
Hakika hii nidini ambayo inayochukia dhulma na madhalimu na inaamrisha
uadilifu, kufanya hisani na kuwapa jamaa na inakataza uchafu na uovu na
dhulma. Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie anatubanishia katika hadithi
hii upeo wa dhulma na mwisho mbaya wa madhalimu. Kweli huo ni mwisho mbaya
kabisa kwani dhalimu atagubikwa na kiza totoro siku ya kiyama asiweze kuiona
njia. Asijue aendeje na aende wapi: --- “NA KARIBUNI (hivi) WAFANYAO DHULUMA
WATAJUA NI MGEUKO (mpinduko) WA NAMNA GANI WATAKAOGEUKA (watakaopinduka)” [26
: 227]
Akasema
tena Bwana mtume Rehema na Amani zimshukie: “Hakika Allah anampururia (anampa
muda) dhalimu, akimtwaa hamponyoki, kasha akasoma: “NA NAMNA HIVI NDIVYO
INAVYOKUWA KUTESA KWA MOLA WAKO ANAPOWATESA (watu wa) MIJI WANAPOKUWA
WAMEACHA MWENDO WALIOAMBIWA HAKIKA TESO LAKE (Allah) LINAUMIZA (na) KALI
KABISA.” [11 : 102]. Bukhaariy na Muslim.
Hebu
kabla ya kuziangalia na kuzichambua aina za dhuluma, tujiulize kwanza hii
dhulma inayokemewa vikali na uislamu ni nini?
Tunaweza
tukaiarifisha na kuianisha dhuluma kuwa ni (kuitumia/kuikalia haki ya mtu
bila uhalali au (ni kuchupa/kuvuka mipaka ya Allah) Hii nidio maana ya dhulma
tunayoikusudia hapa. Na dhuluma mara nyingi hufanyiwa mnyonge/dhaifu
asiyeweza kujinusuru nayo. Dhuluma hutokana na kiza kilichoko moyoni mwa mtu,
ni kiza hiki ndicho kinachomzuia kuiona haki na kuheshimu haki ya mwenziwe.
Lau moyo wa dhalimu ungelikuwa na nuru basi angezingatia haki ya mwenziwe na
kuiheshimu na asingelijasiri kumdhulumu.
Aina
za dhuluma:
Kuna
aina kuu tatu za dhuluma ambazo zinajumuisha:-
1. Dhuluma ya mja kwa Mola wake.
Aina
hii ya dhuluma hupatikana kwa mja kumkufuru/kumkanusha Mwenyezi Mungu
Mtukufu, kuhusiana na hili tunasoma: “--- NA WALIOKUFURU NDIO WALIOJIDHULUMUI
(kweli kweli)” [2 : 254] Kadhalika hupatikana kwa kumshriikisha Mwenyezi
Mungu na kitu kingine katika ibada na hii ndiyo dhuluma kubwa isiyo na
msamaha mbele ya Allah. Tusome na tutafakari kama tuendelee kumshirikisha
Allah au tuache na kutubu: “--- USIMSHIRIKISHE ALLAH, MAANA SHIRIKI NDIYO DHULUMA KUBWA.” [31 :
13]
“HAKIKA
ALLAH HASAMEHI KUSHRIKISHWA NA HUSAMEHE YASIYOKUWA HAYA KWA AMTAKAYE. NA
ANAYEMSHIRIKISHA ALLAH BILA SHAKA AMEBUNI DHAMBI KUBWA [4 : 48]
2. Dhuluma ya mja kwa mja mwenziwe au kwa viumbe vingine vya
Mwenyezi Mungu.
Aina
hii ya pili ya dhuluma hupatikana pale ambapo mtu atakapowafanyia maudhi
wenziwe kwa kuwavunjia heshima. Au kwa kuwadhuru katika miili au hisia zao,
au kwa kutwaa mali zao akayatenda yote hayo pasina uhalali au haki. Bwana
mtume Rehema na Amani zimshukie anatutahadharisha na kutuonya juu ya dhuluma
hii pale aliposema: “Ye yote atakayeimega haki ya muislamu kwa kiapo chake
(alichoapa ili imuhalalikie), basi (kwa kufanya hivyo) Allah amekwisha
muwajibishia moto na kumuharamishia pepo.” Mtu mmoja akauliza: Hata kama
ikiwa ni kitu kidogo tu, ewe Mtume wa Allah? (Mtume) akajibu: “Hata kama ni
ujiti wa mpilipili tawa (aina ya mti unaotumika kama mswaki).” Kila musilamu
kwa muislamu (mwenziwe) ni haramu: (kumwaga) damu yake, (kutwaa) mali yake na
(kuvunja) heshima yake” Muslim
Maneno
haya ya Bwana Mtume ni tafsiri sahihi ya kauli ya Allah ndani ya Qur-ani
Tukufu,tusome: “ENYI MLIOAMINI! MSILIANE MALI ZENU KWA (njia za) BATILI.
ISIP0KUWA IWE BIASHARA KWA KURIDHIANA BAINA YENU (hiyo inajuzu) WALA MSIJIUE
(wala msiue wenzenu). HAKIKA ALLAH NI MWENYE KUKUHURUMIENI NA ATAKAYEFANYA
HAYA KWA UADUI NA DHULUMA, BASI HUYO TUTAMUINGIZA MOTONI NA HAYO NI RAHISI
KWA ALLAH.” [4 : 29-30]
3. Dhuluma ya mja kwa nafsi yake.
Mja
anapoiboronga na kuichafua kwa kutenda aina mbalimbali za maasi. Hili
hufanyika pale ambapo mja anapojasiri kutenda aliyokatazwa na kuharamishiwa
na Mola wake na kuacha kutenda aliyoamrishwa kuyatenda: “--- NAO
HAWAKUTUDHULUMU SISI (walipokhalifu amri yetu) LAKINI WALIKUWA WAMEJIDHULUMU
NAFSI ZAO (kwa huko kuacha kututii).” [2 : 57]
Kama
ambavyo ni haramu kudhulumu, kadhalika ni haramu kuisaidia dhuluma na
madhalimu japo kwa upande wa neno. Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie
anatuambia: “Madhalimu na wasaidizi wao (wote kwa pamoja wataingizwa)
motoni.”
Dailamiy
Ikiwa
utakuwa umeisoma darasa hii kwa moyo uliosalimika na kwa insafu (uadilifu)
hutoshindwa kuona ni jinsi gani uislamu kama dini na mfumo sahihi wa maisha
ulivyolishughulikia suala la kulinda na kuhifadhi haki za jamii ya wanadamu.
Umetoa umuhimu wa pekee katika kulinda haki ya mtu ya kuishi, kumiliki na
kuheshimu wa utu wake
|