|
i/ KUTEKELEZA AHADI
Kutekeleza ahadi ni miongoni mwa tabia njema/tukufu anazotakiwa ajipambe nazo
muislamu wa kweli. Muislamu anapotoa ahadi, basi atambue kwamba amelazimishwa na sheria
kuitekeleza ahadi muda wa kuwa si katika kumuasi Mola Mtukufu. Mwenyezi Mungu
atuambia:-"NA TIMIZENI AHADI. KWA HAKIKA AHADI ITAULIZWA (siku ya kiama) (17:34)
Kukhalifu au kutokutimiza ahadi ni katika jumla ya alama za unafiki wa mtu kama
anavyotubainishia hilo Bwana mtume: "Alama za mnafiki ni tatu:anapozungumza husema
uwongo, na akiahidi hukhalifu (hatekelezi ahadi) na akiaminiwa hufanya khiyana".
Bukhaariy na muslimu.
Tabia ya kutekeleza ahadi humfanya mtu aaminiwe na watu, atajwe vema katika uhai
na baada ya kufa kwake kama Qur-ani inavyotuambia:
"NA MTAJE KATIKA KITABU (hiki) ISMAIL. BILA SHAKA YEYE ALIKUWA MKWELI WA AHADI,
NA ALIKUWA MTUME, NABII". (19:54)
Mwenyezi Mungu amuambia Nabii Muhammad amtaje na kumkumbuka Mtume wake Ismail
ndani ya Qur-ani baada ya kupita chungu ya miaka kwa sababu ya kupambika kwake na tabia
tukufu ya kutekeleza ahadi. Anayetoa ahadi na kutimiza basi atambue kwamba amepambika na
sifa miongoni mwa sifa za mitume. Sifa hii kutekeleza ahadi huambatana na sifa mbili kuu;
kusema ukweli na kutokukhini amana. Basi ukimuona mtu atekeleza ahadi basi mshuhudie pia
kuwa ni mkweli asiye na khiyana.
ii/ UKWELI
Ukweli ni mtu kulieleza jambo kama kilivyo bila yakupunguza au kuzidisha chochote.
Muislamu huwa ni mkweli apendaye kusema ukweli na kujitazamisha na tabia ya ukweli
hii ni kwa sababu anatambua ukweli humuongezea katika wema, wema ambao humuongoza
(kumpeleka) peponi na pepo ndio lengo kuu la muislamu. Muislamu hauangalii ukweli kama ni
tabia njema anayopaswa kujipamba nayo tu bali huenda mbali zaidi ya hapo. Huuona ukweli
kuwa ni miongoni mwa mambo yanayoikamilisha imani na uislamu wake: Mwenyezi Mungu
anatuagiza:-
"ENYI MLIOAMINI: MCHENI ALLAH NA KUWENI PAMOJA NA WAKWELI" (9:119)
Ukweli umejengeka juu ya sababu tatu, ambazo ni:-
- Akili akili timamu ndio humfanya mtu anayetambua manufaa ya ukweli na
madhara ya uwongo.
- Murua mtu mwenye murua, murua wake haumruhusu na kumuachia kusema uwongo
bali humlazimisha ajipambe na tabia ya ukweli
- Dini Dini pia humfinyanga mtu ksema ukweli kwa kuamini kuwa dini
inamuamrisha kusema ukweli na inamkataza kusema uwongo.
Ukweli pia ni miongoni mwa sifa njema walizopambika nazo Mitume wa Mwenyezi Mungu.
Qur-ani yatuambia:- "NA MTAJE IDRIS KATIKA KITABU (hiki). BILA SHAKA YEYE ALIKUWA
MKWELI SANA NA NABII". (19:56)
Tabia ya ukweli huzaa matunda mema na mazuri ambayo huvunwa na watu wakweli.
Miongoni mwa matunda hayo ni:-
- Utulivu wa nafsi Mwenye kupambika na tabia ya ukweli huwa na utulivu wa
nafsi kwa mujibu wa kauli ya Mtume: "Ukweli ni utulivu" At-tirmidhiy
- Baraka katika chumo na ziada ya kheri Bwana Mtume amesema:
"Wauzianaji(Muuzaji na mnunuzi) wana khiyari (ya kupitisha au kuvunja biashara) muda
wa kuwa hawajatengana, wakiwa wakweli na wakabainisha (aibu za kinachouzwa) watabarikiwa
katika biashara yao, na wakificha (aibu) na wakasema uongo itafutwa baraka ya biashara
yao" Al-bukhaariy
- Kufuzu kwa kupata daraja ya mashahidi, hili linathibitishwa na kauli ya Mtume
aliposema: "Mtu atakayemuomba Mwenyezi Mungu kufa shahidi kwa ukweli, Mwenyezi Mungu
atamfikisha daraja ya mashahidi hata akifia kitandani". Muslim
- Kuepuka balaa, inasimuliwa kwamba mtu mmoja aliyekuwa anakimbizwa alikimbilia kwa
mtu mwema mmoja akamuomba amfiche hasikamatwe. Yule mtu mwema akamwambia; "Lala
hapa", akamfunika na rundo la makuti. Wale waliokuwa wanamkimbiza wakapita pale kwa
yule mtu mwema wakamuuliza :"Umemuona mtu akipita hapa anakimbia?" Akawajibu:
"Huyo hapo chini ya makuti". Wale watu wakamuona nawafanyia maskhara wakampuuza
wakaenda zao. Yule mtu aliyekuwa akikimbizwa akaokoka kwa bababu ya ukweli wa mtu mwema
yule.
- Kuchuma mapenzi ya Mola na watu. Mtu mkweli hupendeza mbele ya Mwenyezi Mungu na
watu na watu wema humpenda.
|