|
Ikutoshe
kuona na kutambua ubaya wa hasadi kwamba Allah alimuarisha Mtume wake
Rehema na Amani zimshukie kujilinda na kujikinga na shari ya mtu hasidi
sambamba na shari ya shetani. “NA SHARI YA HASIDI ANAPOHUSUDU”
(113:5). Maana ya hasadi ni mtu kuwa na dhiki, uzito na chuki moyoni mwake
kwa sababu ya neema yua Allah aliyomneemesha mja wake katika dini au
ulimwengu wake.
Muislamu
hamuhusudi mtu na hasadi si sifa wala tabia yake. Hili linatokana na tabia
yake ya kuwapendea kheri watu wote na kuwatanguliza kuliko nafsiyake, yeye
mwenyewe. Kwa mantiki hii basi, muislamu anaichukia hasadi, kwa sababu
hasadi ni kupinga na kuingilia kati mgawanyo wa neema na fadhila za Allah
baina ya waja wake. Hasidi huungua moyoni mwake kwa kujiuliza, kwanini
apate yeye, kwa nini nisipate mimi yeye akakosa. Eeh mtu mbaya hasidi,
huko ni kujipa kazi isiyo yake ugawaji wa neema katika milki yake Allah.
Tusome na tuwaidhike “ (basi Allah anasema). JE, WAO NDIO WANAIGAWA
REHEMA YA MOLA WAKO (wakampa wampendaye wao na wakamnyima wamtakaye?) SISI
TUMEWAGAWANYIA MAISHA YAO KATIKA UHAI WA DUNIA NA TUMEWAINUA BAADHI YAO
DARAJA KUBWA JUU YA WENGINE, KWA HIVYO BAADHI YAO WANAWAFANYA WENGINE KUWA
WATUMISHI WAO……………….”. (43: 32).
Hasidi hana
fungu/sehemu katika miliki na ufalme wa Allah, sasa hadhi ya kugawa nema
za Allah anaipata wapi? Allah anawauliza mahasidi: “AU WANAYO SEHEMU YA
UFALME (wa Allah, basi wanahamaki kwa nini kupewa mtu kitu pasina amri
yao? ). BASI HAPO WASINGALIWAPA WATU HATA TUNDU YA KOKWA YA TENDE. AU
WANAWAFANYA WATU HUSUDA KWA YALE ALIYOWAPA ALLAH KWA UKARIMU
WAKE?……………” (4: 53-54)
Hasadi kama
tabia mbaya inayochukiwa na kupigwa vita na Uislamu inagawanyika katika
matapo (makundi) mawili yafuatayo:-
i.
Mtu kutamani neema aliyokuwa nayo mwenziwe kama
mali, elimu, cheo au madaraka imuondokee na aipate yeye.
ii.
Kutamani kuondoka kwa neema aliyoneemeshwa mja na
Mola wake hata kama hakuipata yeye.
Hasidi yuko
tayari kutoa mali, muda na kila kilicho chake ili kuhakikisha kuwa lengo
lake hilo linafanikiwa hata ikibidi kwa kutoa uhai wa mtu Rejea kisa cha
watoto wa Nabii Adamu, Haabil na Qaabil ni ushahidi mzuri wa hili (5:
27-30) hapo tena ndipo hupumzika, akafurahi na kuona raha.
Hasadi ni
maasi kama maasi mengine, ni dhambi kama dhambi nyingine, na ni haramu. Si
halali kwa yeyote kumuhusudu yeyote kwa lolote. Mtume wa Allah Rehema na
Amani zimshukie anatuasa akisema: “Msibughudhiane, wala msihusudiane,
wala msifanyiane uadui na wala msikatane
na kuweni ndugu enyi waja wa Allah. Si halali kwa Muislamu
kumuhajiri nduguye zaidi ya siku tatu Bukhaariy na Muslim.
Mtume wa
Allah anazidi kutuasa na kutuonya juu ya tabia hii mbaya ya hasadi,
tumsikilize “Jiepusheni/tahadharini na hasadi, kwani hasadi hula mema
(ya mja) kama moto ulavyo kuni au majani:” Abuu Daawoud.
Muislamu
akipitiwa/akijiwa na mawazo ya hasadi kutokana na ubinadamu wake na
kutokuwa kwake na kinga dhidi ya madhambi hupambana nayo. Akijikuta
anamfanyia hasadi mtu yeyote, basi ni juuyake aichukie na aifiche moyoni
mwake, asiidhihirishe kupitia kauli au matendo yake. Atenda matendo
yatakayokwenda kinyume na hasadi iliyomo moyoni mwake, amsifie na kumtaja
kwa wema mtu anaymuhusudi, ajishughulishe na kumtukuza na kumsaidia. Na
akiona lolote au chochote kinachompelekea kufanya hasadi aseme: MA
SHAA-ALLAH, LAA HAWLA WALAA QUWWATA ILLA BILLAH
Hii ndiyo
dawa pekee inayofaa kuitibu na kuiondosha
hasadi au kuidhoofisha, kwani kwa kufanya hivyo hasadi
haitamuathiri na atasalimika nayo. imepokewa: “Utendaji wema huepusha
mianguko miovu/mibaya” Al-baihaqiy.
Si hasadi kufanya
“ghibtwah”’ ambalo ni kutamani kupata neema mithili ya neema
aliyoneemeshwa nayo mtu mwingine bila ya kutamani imuondokee na uipate
wewe. Tena ikiwa ni
neema inayofungamana na dini kama vile elimu na ibada, basi
kutamani huko kuwa katika daraja yenye kusifiwa. Ama ikiwa ni neema
ianyofungamana na dunia kama mali na cheo, kutamani huku huwa katika
daraja ya jaizi na mubaaha. “Ghibtwah” inahalalishwa kupitia kauli yua
Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie :”Hapana (si halili kufanya)
hasadi ila katika mambo mawili. Mtu aliyepewa mali na Allah na akampa
mamlaka/nguvu ya kuitumia (mali hiyo) katika haki. Na mtu aliyepewa hekima
na Allah naye akawa anatoa hukumu kwa kuitumia (hekima hiyo) na
akaifundisha (kwa wenzake):” Bukhaariy. Hekima iliyokusudiwa hapa katika
hadithi ni Qur-ani tukufu na suna ya Mtume (hadithi) tunasihike na
tuwaidhike na ushauri nasaha huu alioutoa Imamu mmoja kwa kiongozi wa
wakati wake, alimwambia.
·
“ Jiepushe na kibri kwani hiyo ndiyo dhambi
awali aliyoasiwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kisha akasoma: “NA (wakumbushe
watu khabari hii) TULIPOWAAMBIA MALAIKA MSUJUDIENI ADAM (yaani
mwadhimisheni kwa ile ilimu yake aliyopewa) WAKAMSUJUDIA WOTE ISIPOKUWA
IBLISI, AKAKATAA NA AKAJIVUNA…………….” (2: 34)
·
Jiepushe na pupa kwani hiyo ndiyo iliyomtoa Adamu
katika pepo aliyomuweka Mwenyezi Mungu, na akamwambia kula humo ila mti
mmoja akamkataza. Kutokana na pupa yake akaula (mti ule) ndipo Mwenyezi
Mungu Mtukufu akamtoa peponi. Kisha akasoma (Allah) AKASEMA ONDOKENI HUMU
NYOTE HALI YA KUWA NI MAADUI NYINYI KWA NYINYI (vizazi vyenu vitakuwa
maadui wenyewe kwa wenyewe) NA UKIKUFIKIENI KUTOKA KWANGU UWONGOFU, BASI
ATAKAYEUFUATA UWONGOFU WANGU HUO HATAPOTEA WALA HATATAABIKA” (20: 123)
·
Na jiepushe na hasadi kwani hiyo ndiyo
iliyompelekea mwana wa Adamu kumua nduguye alipomuhusudi, kisha akasoma,
NA WASOMEE KHABARI ZA WATOTO WAWILI WA ADAMU KWA KWELI. WALIPOTOA SADAKA,
IKAKUBALIWA YA MMOJA WAO NA YA MWINGINE HAIKUKUBALIWA. AKASEMA, (yule
isiyokubaliwa sadaka yake) NITAKUUA, AKASEMA (yule aliyehadidiwa kuuawa)
ALLAH HUWAPOKELEA WAMCHAO TU……………BASI NAFSI YAKE IKAMUWEZESHA
KUMUUA NDUGUYE AKAMUUA NA AKAWA MIONGONI MWA WENYE KUKHASIRIKA” (5:
27-30)
Inasemekana
sababu ya kumuua nduguye ni kwamba mke wa haabil aliyeuwawa alikuwa mzuri
kuliko mke wa Qaabil muuaji. Akamfanyia hasadi nduguye na kamuua ili pate
kumchukua mkewe aliye mzuri.
|