Kazi ni sehemu isiyotengeka ya maisha ya mwanadamu.
Allah Mtukufu ameifanya kazi kuwa ndio wasila wa mwanadamu katika kupata
maisha (riziki) yake ulimwenguni hapa. Tusome huku tukitafakari. “YEYE NDIYE
ALIYEFANYA ARDHI IWE INAWEZA KUTUMIKA (Kwa kila myatakayo) KWA AJILI YENU.
BASI NENDENI KATIKA PANDE ZAKE ZOTE NA KULENI KATIKA RIZIKI YAKE, NA KWAKE YEYE NDIO MAREJEO (yenu nyote)”
(67: 65)
Kwenda katika pande (sehemu/nchi) za ardhi hili ni
suala la kushughulika na kuhangaika kwa ajili ya kutafuta maisha. Mitume wa
Allah-Rehema na Amani ya Allah iwashukie – ambao ndio Waalimu wateule wa
Allah kwa waja wake, pia nao walishiriki katika kufanya kazi. Hawa Allah
asingeshindwa kuwaruzuku bila ya kufanya kazi. Lakini aliwataka wafanye kazi ili
wawe ni mfano mwema wa kuigwa na sisi wafuasi wao. Pia ili kuonyesha kwamba
kila mmoja. Hana budi kula kupitia jasho lake.
Huyu hjapa Nabii Daudi mfanyakazi:”….NA
TUKAMLAINISHA CHUMA. (Tukamwambia). TENGENEZA (nguo za chuma) PANA NA UPIME
VIZURI KATIKA KIUNGANISHA, NA FANYENI VITENDO VIZURI…….” (34:10-12)
Aya inatubainishia kwamba Nabiii Daudi – Amani ya
Allah imshukie – alikuwa ni fundi muhunzi akitengeneza na kuuza mavazi ya
chuma ambayo yalikuwa yakitumika vitani. Tena Allah, anamuagiza aifanya kazi
yake hiyo kwa ufanisi mkubwa. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie
analisisitiza suala hili la ufanisi kazini katika kauli yake: Hakika Allah
anapenda mmoja wenu afanyapo kazi, basi aifanya kwa ukamilifu/uzuri (ufanisi)
Al-baihaqiy). Ione nafasi ya kazi katika uislamu kupitia aya hii, tusome na
tutafakari pamoja. NA ITAKAPOKWISHA SWALA (kuswaliwa) TAWANYIKENI KATIKA
ARDHI MTAFUTE FADHILA ZA ALLAH……….” (62:10).
Nae Bwana Mtume Rehema na Amani zimminikie –
anasema katika hadithi – Qudsi: “ Hakika Allah anasema: Ewe mja wangu wee!
Utikise mkono wako nikuteremshie riziki.
Tutafahamikiwa kutokana na rukuu hizi za aya na
hadithi kwamba ni wajibu tufanye kazi ili iwe ni sababu ya kupatia riziki na
baki ya mahitaji yetu mengine katika maisha haya. Ni lazima tujishughulishe
na kuhangaika kufanya kila shughuli halali tuiwezayo ili tuweze kujipatia
riziki zetu huku tukiamini kuwa bado tumo ndani ya ibada tuliyoumbwa kwa
ajili yake. Tufahamu na tuelewe kwamba Allah Mtukufu hakutuumba na kutuleta
hapa duniani bure bure tu “JE MLIDHANI YA KWAMBA TUMEKUUMBENI BURE NA YA
KWAMBA NYINYI KWETU HAMTARUDISHWA?” (23: 115).
Hapana tena hapana Allah hakutuumba bure, bali
ametuumba kwa hekima na busara nyingi. Ametuumba tufanye kazi tupate riziki
zetu, tumuabudu bila ya kumshirikisha na chochote, tumtukuze na tumshukuru
kwa neema zake zisizodhibitika na akili zetu. “KULENI KATIKA VILE
ALIVYOKUPENI ALLAH, VILIVYO HALALI NA VIZURI. NA SHUKURUNI NEEMA ZA ALLAH,
IKIWA KWELI MNAMUABUDU YEYE.” (16: 114).
Tufanye kazi ili iwe ndio sababu ya mafanikio yetu
hapa duniani tulipo hivi sasa na huko akhera tuelekeako. Tufanye kazi huku
tukiamini kuwa hiyo ni amri ya Mola wetu na ndio utaratibu aliotupangia
katika kupata riziki zetu: ……..”BASI NENDENI KATIKA PANDE ZAKE ZOTE NA KULENI
KATIKA RIZIKI ZAKE……” (67:15).
Katika aya hii Allah Mtukufu anatuagiza na
kutuamrisha waja wake tuziendee pande za ardhi, tujishughulishe/tufanye kazi.
Tusome elimu mbalimbali zitakazotuwezesha kuitumia kwa manufaa yetu rasimali
aliyoijaza tele angani, ardhini, na
majini. Kutokana na rasimali hizo tufanye uhunzi, biashara, kilimo, ufugaji
na ……na……ili tuweze kupata raha na mafanikio katika maisha haya ya majaribio
na iwe pia ndio sababu ya fanaka katika maisha hayo ya milele yajayo.
Pia tutakuwa tumelitekeleza agizo na amri ya Mola
wetu ya kufanya kazi na hivyo kujihakikishia fursa ya kupata radhi zake
ambazo hazitamaanisha kingine zaidi ya raha na amani ya milele duniani,
kaburini na kule peponi.
Ni muhimu tukaelewa na kufahamu kwamba Allah
Mtukufu kwa hekima zake zilizotukuka ameviumba vitu vyote na kuviwekea faida
yake. Tukiangalia mathalani faida ya mimea ni nafaka na makapi yake, nafaka
tunazitumia kama chakula chetu na wanyama na makapi/pumba kama chakula cha
wanyama tu. “NA ALAMA (ya kuonyesha moja ya rehema za Allah) JUU YAO NI ARDHI
ILIYOKUFA. TUNAIFUFUA NA TUKATOA NDANI YAKE NAFAKA. WAKAWA WANAZILA” (36;
33).
Faida ya miti ni yale matunda, vivuli na mazao
yake mengine kama vile mbao ambazo tunazitumia katika manufaa/maslahi yetu mbalimbali. “NA TUKAFANYA NDANI
YAKE MABUSTANI YA MITENDE NA MIZABIBU NA KUPITISHA CHEM CHEM NDANI YAKE. ILI
WALE KATIKA MATUNDA YAKE, NA
HAIKUYAFANYA (matunda) HAYO MIKONO YAO, JE, HAWASHUKURU”.(36: 34-35).
Faida ya wanyama ni pamoja na maziwa, suti,
manyoa, nyama, mifupa yake na mazao yake mengine kama vile ngozi na pembe
zake. Pia tunawatumia wanyama kama
chombo cha usafiri wetu na mizigo yetu, kadhalika tunawatumia katika shughuli
zetu za kilimo. “ NA (pia) AMEWAUMBA WANYAMA. KATIKA HAO MNAPATA (vifaa
vitiavyo) JOTO NA MANUFAA (mengine) NA WENGINE MNAWALA NA MNAONA RAHA
MNAPOWARUDISHA JIONI NA MNAPOWAPELEKA MALISHONI ASUBUHI. NA (wanyama hao pia)
HUBEBA MIZIGO YENU KUPELEKA KATIKA MIJI MSIYOWEZA KUIFIKA ISIPOKUWA KWA
MASHAKA NA TAABU. HAKIKA MOLA WENU NI MPOLE SANA (na) MWENYE REHEMA NYINGI.
NA (amewaumba) FARASI NA NYUMBU NA PUNDA ILI MUWAPANDE NA (wawe) MAPAMBO……”
(16: 5-8)
Ndugu yangu muislamu hatuwezi kutaja faida ya
neema za Allah zilizo juu yetu tukasesha bali hata hizo neema zenyewe ……….NA
KAMA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH, HAMTAWEZA KUZIHISABU………” (14: 34)
Na faida ya mwanadamu ni kujishughulisha na
kufanya kazi ili aweze kuzitumia neema hizi alizopewa bure na Mola wake kwa
ajili ya ustawi wake katika ardhi hii na akhera. Kisha amuabudu na kumshukuru Mola wake juu ya neema zake hizo ili ampe ziada ya neema. (NA
(kumbukeni) ALIPOTANGAZA MOLA WENU (kuwa) “ KAMA MKISHUKURU, NITAKUZIDISHIENI
NA KAMA MKIKUFURU (jueni) KUWA ADHABU YANGU NI KALI SANA” (14:7)
Ewe ndugu
muislamu, Allah Mtukufu ametuelekeza na
kutuongoza tufanye kazi na tusifanye uvivu pale alipomuamrisha mdudu mdogo
nyuki kufanya kazi na kujijenga
nyumba majabalini na mitini. Ale katika anuwai za matunda ili aweze
kuutekeleza wajibu alioumbiwa ambao ni kutengeneza asali, chakula na dawa kwa
binadamu. Tusome na tuchukue mfano mzuri wa mdudu nyuki katika kufanya kazi.
(NA MOLA WAKO AKAMFAHAMISHA NYUKI YA KWAMA “ JITENGENEZEE MAJUMBA (yako)
KATIKA MILIMA NA KATIKA MITI NA KATIKA YAKE (majumba) WANAYOJENGA (watu)”
KISHA “KULA KATIKA KILA MATUNDA, NA
UPITE KATIKA NJIA ZA MOLA WAKO ZILIZOFANYWA NYEPESI (kuzipita).” KINATOKA KATIKA MATUMBO YAKO KINYWAJI (asali)
CHENYE RANGI MBALIMBALI, NDANI YAKE KINA PONYO (pozo) KWA WANADAMU. HAKIKA
KATIKA HAYO MUNA MAZINGATIO KWA WATU WENYE FIKRA”. (16: 68-69).
Ni vema ukafahamu na kuelewa kwamba kazi ndio
kipimo cha utu. Fakhri na utukufu wa mtu hujidhihirisha kupitia kazi, huoni
kuwa ombaomba ni mtu duni asiye na
thamani machoni mwa jamii? Huoni kuwa wale waliochukua taabu katika
kusoma na kufanya kazi ndio watu maarufu na wenye maisha mazuri katika jamii” Hawa wana nafasi
kubwa zaidi ya kuirithi pepo ya Allah kupitia neema zake alizowapa kutokana
na juhudi yao katika kufanya kazi. “
NA UTAFUTE KWA YALE ALIYOKUPA ALLAH- MAKAZI MAZURI YA AKHERA. WALA USISAHAU
SEHEMU YAKO YA DUNIA NA UFANYE WEMA KAMA ALLAH ALIVYOKUFANYIA…….” (28:77).
Hao matajiri, wavumbuzi, wataalamu na mabingwa.
Katika fani mbalimbali tuwaonao leo, hawakuzifikia daraja/nafasi hizo kwa
kubahatika tu. La hasha!. Bali
imewagharimu taabu, muda na juhudi kubwa za makusudi mpaka kufika hapo walipo
leo na kuanza kufaidi matunda ya
taabu na juhudi zao za jana. Mafanikio na fanaka yako wewe leo
hapa duniani na kesho kule akhera
yatategemea kwa kiasi kikubwa.
i)
Juhudi na bidii yako katika
kufanya kazi.
ii)
Kufanya kazi kwa ufanisi.
iii)
Kuifanya kila kazi ikupasayo katika wakati wake muafaka bila ya
kuichelewesha .
KUMBUKA
Kufanya kazi ni agizo na amri ya Allah.
Kufanya kazi na kula kutokana na kazi hiyo ni
ibada kama ibada nyingine.
Kuacha kufanya kazi bila ya udhuru ni dhambi.