Kumpenda
jirani, hii ni tabia ambayo Muislamu anatakiwa aijenge, aizoee na
kujipamba nayo. Muislamu anapaswa kujua kuwa kumpenda jirani yake ni
sehemu ya mafundisho ya dini yake ambayo Uislamu wake haukamiliki ila kwa
kuyaitakidi, kuyafuata na kuyatia vitendoni. Kumpenda jirani ni pamoja na
kuzijua haki zake zikupasazo na kumtekelezea.
Mafanikio,
raha na furaha ya maisha ya mwadamu hutegemea kwa kiasi kikubwa sana mambo
yafuatayo:-
1.Utulivu wa moyo na akili.
2.Amani na usalama wa maisha (uhai), mali na heshima (hadhi)
3.Thamani ya utu wake.
4.Mapenzi na ushirikiano wa jamii inayomzunguka.
Maeneo
yote haya na mengine ambayo hatujayataja ni mazingira yanayohitaji
kuandaliwa, kutayarishwa na kujengea ili mwanadamu aishi kwa amani na
utulivu na kuyaonea raha na furaha maisha yake katika ulimwengu huu.
Mtu
aliye karibu zaidi nawe, ukiachilia mbali wazazi wako, ndugu na jamaa na
nasabu ni jirani yako. Jirani ni mtu unayeishi naye mtaani kwako au
kitongojini mwako kwa kawaida huyu ndiye mtu wa kwanza kusikia na kisha
kushirikiana nawe katika machungu yaliyokusibu au furaha iliyokushukia.
Uislamu
katika kulizingatia hili, umempa mtu huyu muhimu (jirani) heshima na haki
za pekee bila ya kujali ni ndugu wa nasabu au la. Tulisome agizo na amri
ya Mola juu ya jirani "MWABUDUNI ALLAH WALA MSIMSHIRIKISHE NA
CHOCHOTE NA WAFANYIENI IHSANI WAZAZI WAWILI NA JAMAA NA MAYATIMA NA
MASIKINI NA JIRANI YAKO KARIBU NA JIRANI WALIO MBALI NA RAFIKI WALIO
UBAVUNI (Mwenu) NA MSAFIRI ALIYEHARIBIKIWA NA WALE ILIYOWAMILIKI MIKONO
YENU YA KULIA????" (4:36).
Ufafanuzi
mdogo aya:
JIRANI
WALIO KARIBU: Huyu ni yle anayeishi karibu kabisa na wewe hata kama si
Muislamu au ni yule ambaye mna udugu wa nasaba baina yenu.
JIRANI
WALIO MBALI: Huyu ni yule aishiye mbali na wewe au si ndugu yako wa nasabu.
RAFIKI
WALIO UBAVUNI: Huyu ni mwenzio katika kusoma (elimu) kazi, safari yaani ni
mtu mnayeshirikiana au kuambatana katika jambo/suala Fulani.
Ili
kuonyesha umuhimu wa jirani na haki zake Malaika Jibril - Amani imshukie -
alimuusia sana Bwana Mtume juu ya jirani na kuukariri wasia wake huo mpaka
Mtume akadhania ataamrishwa kumrithisha kwa kupewa fungu la mirathi kama
wanavyopewa ndugu wa nasabu "Jibril aliendelea kuniusia juu ya jirani
mapaka nikadhania kuwa atamrithisha." Bukhaariy na Muslim.
Uislamu
umeifanya haki ya jirani kuwa ni haki ya kijamii inayomuhusu jirani
muislamu na asiye muislamu.
Uislamu haukulitazama hili kwa mtazamo wa itikadi bali umelitazama kwa
mtazamo wa amani na usalama ili watu wote waishi katika mazingira yenye
amani na usalama, na jami
yenye utulivu. Taji hili la ujirani ikiwa ni pamoja haki zinazoambatana
nalo anavishwa kila mtu, bila ya kujali kuwa ni muislamu au kafiri, mwema
au muovu, rafiki au adui, ndugu au si ndugu, anaishi jirani kabisa na
mbali na kadhalika. Pamoja na uislamu kuwapa wote hao haki na heshima ya
ujirani, umewagawa na kuwapanga katika daraja na mafungu yafuatayo.
Tuisome sote kwa pamoja hadithi hii ya Bwana Mtume- Rehema na Amani
zimshukie: " Majirani ni watatu, Jirani mwenye haki moja nae ni
Mushrikina (kafri/asiye muislamu), huyu ana haki ya ujirani (tu). Na
jirani mwenye haki mbili nae ni Muislamu (mwenzio), huyu ana haki ya
ujirani na haki ya Uislamu. Na jirani mwenye haki tatu, huyu ni Muislamu
aliye ndugu wa nasabu, ana haki ya ujirani, haki ya Uislamu na haki ya
udugu" Twabaraariy.
Hebu
angalia ni namna gani Uislamu unavyomthamini hata jirani asiye muislamu
kupitia mfano hai aliotupigia
swahabu wa Mtume - Rehema na Amani zimshukie. Imepokelewa kutoka kwa
Abdillah Ibn Amri - Allah awawiye radhi- kwamba yeye alichinja mbuzi,
akauliza, mmempelekea yule jirani Myhahudi? Kwani mimi nimemsikia Mtume wa
Allah - Rehema na Amani zimshukie - akisema, "Hakuacha Jibril
kuniusia juu ya jirani mpaka nikadhani atamrithisha" Bukhaariy na Abu
Daawaoud. Katika uislamu, ujirani una haki zake za pekee na haki hizi
uzidi itakaposadifu kuwa na uislamu ndani yake. Haki hizi huongezeka zaidi
na zaidi iwapo ujirani huu utachangaya uislamu na udugu wa nasabu pamoja.
Mwanadamu yeyote hupitia katika
mkondo wa matatizo na shida mbalimbali shida hizi huweza kutokea mchana au
usiku na bila taarifa au kufanya maandalizi yoyote ya kukabiliana nayo.
Maradhi ya ghafla, msiba, moto, kuingiliwa na wezi, yote haya huweza
kumtokea mtu na kuhitaji msaada wa haraka. Hakuna anayeweza kutoa msaada
huu wa haraka na katika wakati muafaka ila ni jirani. Sasa kama hukuishi
naye vizuri, kwa masikilizano na ushirikiano, utapataje msaada wake? Kweli
atakuwa na moyo na mapenzi ya kusaidia, ikiwa hukuyajenga mazingira mazuri
mapema.?
Haki
hizi za kijamii katika Uislamu zinalenga kujenga mahusiano mema baina ya
jamii, kupanda moyo wa huruma, upendo na kusaidiana ili jamii ya wanadamu
iishi chini ya anga la amani, utulivu, furaha na salama.
Haki
hizi zikichungwa na kutekelezwa ipasavyo, natija yake ni kuwafanya watu wa
mji mmoja kuwa kama mfano wa mwili mmoja, kama kwamba ni watu wa familia
moja. Mipaka ya ujirani kisheria imedhibitiwa na riwaya zifuatazo:-
1.
Imepokelewa kutoka kwa Imam Ally Allha amuwiye radhi amesema: Atakayesikia
adhana basi huyo ni jirani yako. Yaani mtu mnayesikia pamoja adhana ya
msikiti ulio jirani yeu, yeye akiwa nyumbani kwake na wewe nyumbani kwako,
basi fahamu huyo ni jirani yake.
2.
Riwaya nyingine inasema:- Atakayeswali swala ya sub-hi msikitini pamoja
nawe, basi huyo ni jirani yako.
3.
Imepokelewa kutoka kwa Bi Aysha Allah amuwiye radhi "Mpaka wa ujirani
ni nyumba arobaini kwa kila upande."
4.
Imepokelewa kutoka Al-Hassan Al-Biswriy kwamba yeye aliulizwa kuhusiana na
jirani, akajibu"Ni nyuma, yake arubaini kuliani mwake na arubaini
kushotoni mwake (mtu)" Bukhaariy katika kitabu "AL-ADABUL MUFRAD".
Miongoni mwa haki jumla za jirani ni kumfanyia ihsani. Ihsani, hili ni
neno lenye maana pana sana, linahusisha kumtendea kila ambalo ni jema/zuri
lenye kumpa faraja, furaha na matumaini, ihsani hii inakusanya vyote
viwili; kauli (maneno) na amali (matendo) na hii ni amri ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu, tusome na tuamrike. "--- NA WAFANYIENI IHSANI WAZAZI WAWILI
NA JAMAA NA MAYATIMA NA MASIKINI NA JIRANI WALIO KARIBU NA JIRANI WALIO
MBALI NA RAFIKI WALIO UBAVUNI (Mwenu)---." [4:36]
Amri
hii pia imekuja katika sunah ya Bwana Mtume (hadithi) kwa tamko la IKRAAMU
na mara nyingine kwa tamko la IHSAANI kama ilivyokuja katika aya. Amesema
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie : " Mwenye kumuamini Allah na
siku ya mwisho, basi na amkirimu jirani yake." Bukhaariy na akasema
tena:" Mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi na amfanyie
Ihsaani jirani yake." Muslim.
Tafsiri
na ufafanuzi wa matamko haya mawili; ikraamu na ihsaani, umekuja katika
hadithi kadhaa. Miongoni mwa hizo: "(maswahaba) waliuliza ewe Mjumbe
wa Allah ni ipi haki ya jirani kwa jirani yake? Akajibu: Akikuomba mkopo
mkopeshe, akikuomba msaada msaidie, akiumwa mkague, akiwa na haja mpe (mtekelezea),
akipatwa na kheri (jambo zuri) mpongeze, akipatwa na msiba umuizi (mfanyie
taazia) na akifa lifuate jeneza lake (mazikoni)." Twabaraaniy
Haki
nyingine za jirani, mbali na hizo ni pamoja na:-
1·Uhifadhi/utunze
siri zake unazozijua.
2·Uchunge
heshima na hadhi yake.
3·Ujipendekeze
kwake kwa kumpa zawadi
4·Uyapupie
maslahi yake kama unavyoyapupia maslahi yako.
5·Umkabili
kwa bashasha na uso mkunjufu.
Amesema
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie "Ewe Abu Dhari, ukipika mchuzi
basi ongeza maji yake na umuangalie jirani yako (mpelekee)" Muslim.
Mwanamke
kimaumbile na kiuzoefu ndiye hugongana na kukwaruzana na jirani yake mara
kwa mara. Jambo hili huathiri kwa kiasi kubwa ujirani na kupandikiza mbegu
ya chuki na uhasama na kusababisha kuvunjika kwa hali ya amani na utulivu.
Njia munasibu ya kuliepusha janga hili ni kutumia njia hii ya kupeana
zawadi hata zile ambazo ni duni na ndogo machoni. Kitendo hiki cha
kuzawadiana hujenga moyo wa huruma na upendo na kuifukuzilia mbali chuki.
Hebu na tuuzingatie wito huu wa Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie:-
Enyi wanawake waislamu, jirani asimdharau asimdharau jirani yake walau kwa
(kumpa) makongoro (miguu) ya mbuzi" Bukhaariy na Muslim.
Kitendo
cha kumpa zawadi/hadiya jirani yako humjengea hisia za kuwa unamjali,
unamthamini, unampenda na kumuheshimu. Ni hisia hizi ndizo ambazo
humuondoshea chuki, husda, mafundo na fitna juu yako na mahala pake
kutawaliwa na upendo, huruma na moyo wa kusaidia.
Ikiwa
kumfanyia Ihsaani jirani ni jambo linalotakiwa na sheria, basi
kutokumuudhi pia ni amri ya lazima. Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie
anatuasa juu ya hilo. "Mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi
asimfanyie maudhi jirani yake." Bukhaariy na Muslim.
Kuna
matendo mengi ambayo ukiyafanya huwa ni maudhi na kero kwa jirani yako kwa
mtazamo wa sheria, hayo ni pamoja na
1·kuegesha
gari lako mbele ya nyumba yake na kumzibia mlango wake.
2·Kutupa
takataka zako uwanjani kwake.
3·Kufungua
radio yako kwa sauti kubwa
4·Kuwaacha
wanao kuchezacheza na kupiga kele mbele ya nyumba yake.
Kupanga
njama za kumdhuru au kumvunjia heshima yake.
Angalia
namna Uislamu ulivyoyachunga hata mambo ambayo yanaweza kuleta athari
mbaya kwa wakubwa na watoto. Mtegee sikio la usikivu wa kufuata na
kuzingatia Mtume wako Rehema na Amani zimshukie:"--- na wala
usimuudhi kwa harufu ya chungu chako ila umchotee humo, na ukinunua
matunda mpe na yeye, kama hukumpa basi yaingize kwa uficho (asiyaone) na
wala mwanao asitoke nalo nje na kuwakasirisha wanawe (kuwafanya waanze
kulilia)". Twabaraariy