|
Muislamu wa kweli ni mtu mwenye huruma. Huruma ni miongoni mwa tabia za muislamu.
Chimbuko la huruma ni usafi na utakasifu wa nafsi na roho, hivyo ndiyo kusema kuwa na
huruma ni nembo na alama ya kuonyesha usafi wa nafsi ya mja na utakasifu wa roho yake.
Huruma ya kweli inatokana na ulaini wa moyo ambao humpelekea mja kumsamehe aliyemkosea na
kumfanyia wema aliyemtendea uovu. Huruma ikijizatiti na kuthibiti moyoni ndipo hujitokeza
nje athari yake. Hapo ndipo utamuona mtu aliyepambika na tabia hii ya huruma anaitumia
mali yake kumsaidia mwenye shida, hutumia cheo/hadhi yake kumnusuru/kumsaidia mdhulumiwa,
humsamehe aliyemkosea, humpa chakula mwenye njaa na humsaidia mgonjwa. Zote hizi ni baadhi
tu ya athari za tabia ya huruma.
Huruma ni miongoni mwa sifa za watu wa peponi, Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia
"KISHA AWE MIONGONI MWA WALIOAMINI NA WAKAUSIANA KUSUBIRI NA WAKAUSIANA KUHURUMIANA.
HAO NDIO WATU WA UPANDE WA KHERI (peponi)" [90:17-18] kuwahurumia watu ni sababu ya
kupata huruma ya Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume isemayo: "Hakika
si vinginevyo Mwenyezi Mungu huwaonea huruma waja wake wenye huruma"
Al-Bukhaariy.
Hapana shaka mtu mwenye sifa na tabia hii ya huruma hupendwa na jamii. Tabia hii ya
kuoneana huruma pia ndio siri kubwa ya ushindi na mafanikio ya waislamu wa mwanzo, kwani
kuhurumiana kwao ndiko kulikowapelekea kupendana mapenzi ya kweli, na mapenzi haya
yakawapeleka katika mshikamano wa dhati ambao ukawafanya kuwa wamoja na nguvu. Tunasoma
ndani ya Qur-ani: "MUHAMMAD NI MTUME WA ALLAH NA WALIYO PAMOJA NAYE NI WENYE NYOYO
THABITI MBELE YA MAKAFIRI NA WENYE KUHURUMIANA WAO KWA WAO" (48:29)
iv/ KUWAHURUMIA WANYAMA
Wanyama ni miongoni mwa viumbe hai ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa fadhila zake
ametuambia tuwahurumie ili watusaidie na kututumikia katika maisha yetu hapa duniani. Kwa
hivyo ni wajibu wetu kuwanea huruma. Mwenyezi Mungu atuambia: "NA (pia) AMEWAUMBA
WANYAMA KATIKA HAO MNAPATA (vifaa vitiavyo) JOTO NA MANUFAA (mengine); NA WENGINE MNAWALA:
NA MNAONA RAHA MNAPOWARUDISHA JIONI NA MNAPOWAPELEKA MALISHONI ASUBUHI. NA (wanyama hao
pia) HUBEBA MIZIGO YENU KUPELEKA KATIKA MIJI MSIYOWEZA KUFIKA ISIPOKUWA KWA MASHAKA NA
TAABU. HAKIKA MOLA WENU NI MPOLE SANA (na) MWENYE REHEMA NYINGI NA (amewaumba) FARASI NA
NYUMBU NA PUNDA ILI MUWAPANDIE NA (wawe) MAPAMBO
" (16:5-8)
Utafahamikiwa kutokana na aya hizi kwamba wanyama manufaa mengi sana kwa wanadamu.
Wanyama wana sifa nyingi za kimaumbile zinazoshabihiana na zile za binadamu. Miongoni mwa
sifa hizo ni kushikwa na kiu na njaa, kuugua, kuona baridi au joto, kuhitajia mahala pa
kulala, kuchoshwa na kazi ngumu na kadhalika. Kwasababu hizi imemlazimu mwanadamu
kumuhurumia mnyama kwa kumpa chakula na maji ya kutosha, kumpa malazi mazuri, kumtibu
anapoumwa, kutomkalifisha kufanya kazi asizoziweza na kutomuadhibisha wakati wa kumchinja.
Amesema Bwana Mtume katika hadithi aliyoipokea Abu Hurayrah: "Wakati mtu mmoja
alipokuwa akienda (njiani) akashikwa na kiu kikali sana. Akashuka kisimani akanywa maji
kisha akatoka, kutahamaki akamuona mbwa akihema na kula mchanga kutokana na kiu.
Akajisemea (nafsini mwake): kimempata huyu kiu kama kilichonipata mimi. Akakijaza maji
kiatu chake, kisha akakishika kwa mdomo wake akapanda (kutoka kisimani kuja juu).
(Akanywa) mbwa akakata kiu, akamshukuru Mwenyezi Mungu, akasamehewa yule mtu madhambi
yake. Wakauliza (maswahaba): Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sisi tunapata ujira kwa
(kuwafanyia wema) wanyama? (Mtume) akajibu: "kuna ujira katika kila ini bichi (mnyama
hai)" Al-Bukhaariy.
Katika hadithi hii tunamuona mwanadamu huyu anachukua taabu anaingia kisimani kuchotea
mbwa maji na kumnywesha. Yote haya yanatokana na huruma iliyomo moyoni mwa mtu yule,
isingelikuwa huruma asingeweza kufanya aliyoyafanya. Tabia na kitendo chake hiki cha
huruma kimekuwa ni sababu ya kusamehewa dhambi zake.
|