|
Upole ni dhana ambayo huweza kutofautiana baina ya mtu na mtu, jamii na
jamii nyingine, dini na dini kulingana na mtazamo wa mtu/jamii au dini husika juu ya dhana
nzima ya upole. Tunamaanisha na kukusudia nini tunapozungumza dhana ya upole? Makala haya
yamekusudia kuiangalia na kuieleza dhana hii ya upole chini ya kivuli cha uislamu kupitia
Qur-ani Tukufu na Sunnah ya Bwana Mtume Rehema na Amani zimshuke. Tusome kwa
mazingatio:- KWA YAKINI IBRAHIMU ALIKUWA MPOLE MWENYE KUMTUKUZA ALLAH NA MWEPESI WA
KUREJEA (kwake).[11:75]
Qur-ani Tukufu inatufahamisha kupitia aya hiyo hapo juu kwamba:-
- Kumbe upole ni sifa njema waliyopambika nayo mitume wa mwenyezi mungu japokuwa hapa
ametajwa Nabii Ibrahimu- Rehema na Amani ziwashukie wote.
- Upole ni sifa muhimu ya kiutendaji ambayo Mjumbe/Mtume/Mtumishi yeyote wa ummah hana
budi kuwa nayo ili imsogeze karibu na watu wake. Huku kuwa karibu na watu wake
kutamrahisishia mawasiliano yake nao jambo ambalo litamwepesishia kazi yake.
- Pole wa kweli na halisi ni ule uambatanao na sifa mbili muhimu ambazo ni :-
- Kumtukuza Mwenyezi Mungu Mtukufu.
- Wepesi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu kuomba msamaha mara tu kosa litendekapo.
Kupitia aya hii tunaweza sasa tukaieleza dhana ya upole kuwa ni kudhibiti
nafsi wakati wa mafuriko ya ghazabu au kuacha kulipa kisasi dhidi ya adui/mbaya wakati wa
kuweza kulitekeleza hilo na kuendelea kuwa karibu na mtu huyo.
Kuna mambo kadhaa ambayo kwa kiasi kikubwa kuchangia kumfanya mtu awe na
sifa hii njema na tukufu ya upole ambayo inatakiwa iwe ni pambo na vazi la kila muislamu.
Tukubaliane na tuyaite mambo hayo kuwa sababu/msingi ya upole. Miongoni mwa sababu hizo
ni:-
- Kuwa na huruma. :
Ni muhali kabisa mtu kuwa mpole ikiwa hamna ndani ya moyo wake chembe ya
huruma, kwani ni hisia za huruma ndizo ambazo humfanya mtu kuwa mpole kiasa cha kuacha
kumuangamiza mbaya wake il-hali ana uwezo na nguvu za kulitekeleza hilo. Bwana Mtume
Rehema na Amani zimshukie- anutuambia :- Asiyehurumia (hastahiki)kuonewa
huruma.
- Kujiepusha na kuwashutumu na kuwatukana watu.
Kitendo cha kushutumiana na kutukanana hupeleka kujenga chuki na moyo wa
kulipiza kisasi baina ya watu. Ni bayana kwamba palipotawaliwa na chuki na visasi hapana
huruma na pasipo na huruma hapana upole. Hii ndio sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu
akatukataza kuwatukana washirikina/makafiri ili tusisababishe kutukanwa Mwenyezi Mwenyezi
Mungu, jambo ambalo waumini wa kweli hawatalivumilia na watataka kuliondosha kwa nguvu zao
zote hapo ndipo hasira, chuki na visasi vitatawala pande zote mbili na kuzifukuzilia mbali
huruma na upole na kusababisha umwagikaji wa damu usio wa lazima. Tusome na
tuzingatie:-WALA MSIWATUKANE WALE AMBAO WANAABUDU KINYUME CHA ALLAH, WASIJE
WAKAMTUKANA ALLAH KWA JEURI ZAO BILA KUJUA
.[6:108]
- Kuwa na haya
Kuwa na haya ni kuhifadhi na kuichunga nafsi na kila ambalo kwa namna moja
ama nyingine linaweza kuwa ni sababu ya kuvunja heshima na hadhi ya mtu mbele ya jamii.
Pia kuwa na haya huonyesha kukamilika kwa murua wa mtu. Mtu anapojivika joho la haya, haya
itamsukuma kujichunga sana katika utendaji wake katika kuchanganyika kimaisha na wenziwe.
Hatofanya la kuwaudhi au kuwakera wenziwe ili naye asije kufanyiwa, hatakuwa ni
chanzo/sababu ya kuvunja heshima ya wengine ili kuhifadhi heshima yake isivunjwe. Huyu
atakuwa akiuzingatia na kuishi na msingi wa busara usemao: utendavyo ndivyo
utakavyotendewa. Mtu anapokosa haya, huwa hana huruma na hivyo kutokuchunga wala
kujali heshima na hadhi za watu wengine. Ni kutokana na umuhimu na nafasi ya sifa hii
inayompamba na kumfanya mtu kuwa mpole ndio Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie
akatuambia : haya ni sehemu ya imani
.Ahmad.
- Kuacha kuzungumza maneno ya ufedhuli ya upuzi yasiyo na maana
Katika kusema maneno ya ufadhuli kutapelekea kuhimiza hisia za watu na
pengine kuzusha hali ya kutokuelewana na kusababisha kuvunjika kwa amani baina ya pande
mbili husika. Ni kwa kulizingatia hilo ndipo Bwana Mtume-Rehema na amni zimshukie-akatuasa
:-Mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, basi na aseme la kheri {ikiwa
hana}na anyamaze
Kwa mantiki hii kuacha kwako kusema maneno ya ufedhuli huonyesha kuwajali
kwako wenzio, na hili haliji hivi hivi tu bali husababishwa na huruma iliyomo ndani ya
nafsi ambayo humfinyanga mtu kuwa mpole.
Mambo haya ni baadhi tu ya msingi, sababu na vyanzo vya sifa njema ya
upole ambayo ni rasilimali kubwa ya mtu.Tujipambe na sifa hii ili nasi tuipate daraja
kubwa iliyoandaliwa maalumu kwa ajili ya watu wapole tuisome na kuuamini kauli ya Bwana
Mtume Rehema na Amani zimshukie:- Hakika mtu huridhika/ hupata kwa sababu ya
upole daraja ya mfungaji {mchana} asimamaye{usiku kufanya ibada}
|