|
AKHLAAQ NI
NINI?
Elimu ya akhlaaq ni elimu ya malezi ya tabia ambayo
hujihusisha na kutengenea kwa moyo kwa kuupamba na tabia njema na kuuepusha na tabia
mbaya.
CHIMBUKO LA ELIMU YA AKHLAAQ:
Elimu hii msingi wake ni Qur-ani Tukufu
na Hadithi. Amesema Mwenyezi Mungu katika kusifia Mtume wake juu ya tabia njema: "NA
BILA SHAKA UNA TABIA NJEMA KABISA"(68:4) Bwana Mtume naye anaukiri na kuuthibitisha
ukweli huu pale aliposema: "Hakika si vingine nimetumwa kuja kutimiza TABIA
NJEMA" Al-Bukhaariy
FAIDA ZA ELIMU YA AKHLAAQ:
Elimu hii husaidia kuutengeneza moyo wa mwanadamu
ikamtoa katika unyama, ikamfinyanga na kumfanya kuwa mtu mwema, aliyepambika na sifa na
tabia njema na kumuepusha na tabia mbaya, na ikawa ndiyo sababu ya kufaulu duniani na
akhera. "Aliulizwa Mtume wa Mwenyezi Mungu juu ya mambo yanayoingiza watu peponi kwa
wingi,akasema: (Kumcha Mungu na tabia njema)" At-twabraaniy
Elimu hii pia humsaidia mtu kuzijua tabia njema akazifuate na tabia mbaya
akaziepuka.
SOMO LA KWANZA
i) UBORA WA ELIMU
Elimu ndio pambo tukufu na lenye thamani
kushinda/kuliko mapambo yote anayojipamba nayo mwanadamu. Elimu ndio mwangaza na taa pekee
inayomuangazia mwanadamu katika maisha ya ulimwengu huu. Elimu ndio chombo pekee
anachoweza kukitumia mwanadamu katika kumtii Mola wake, kwani kutokana na elimu ndipo
mwanadamu huweza kujua halali na haramu na akapambanua baina ya lenye kunufaisha na lenye
kudhuru. Elimu ndio wasila na sababu ya msingi ya mtu kuweza kupata utukufu. Lau si elimu
mataifa yasingeweza kupata maendeleo yaliyonayo leo, maendeleo ambayo hukua siku hata siku
kwa sababu ya elimu. Lakini lazima tutambue kwamba elimu pekee bila ya amali/vitendo haina
maana, haisaidii chochote, kwani elimu haiwi elimu ila kwa kutumiwa kama walivyosema
wanazuoni wema: {Elimu bila ya matendo ni kama mti usiotoa matunda}.
Mwenye kutaka kupata elimu ya ziada, pamoja na
kufanya juhudi ya kusoma basi ajilazimishe sana kumcha Mwenyezi Mungu katika dhahiri na
siri. Amesema Mwenyezi Mungu: "NA MCHENI MWENYEZI MUNGU NA MWENYEZI MUNGU
ATAKUELIMISHENI; NA MWENYEZI MUNGU NI MJUZI WA KILA KITU"(2:282)
Katika kuonyesha ubora na utukufu wa elimu Mwenyezi Mungu anatuambia: "SEMA,
JE WANAWEZA KUWA SAWA WALE WANAOJUA NA WALE WASIOJUA?.."(39:09)
Ili kusisitiza na kuonyesha ubora wa elimu ndipo Bwana Mtume akatuambia:{Kutafuta
elimu ni faradhi ya lazima kwa kila muislamu: mwanamume na mwanamke}
UBORA/FAIDA ZA KUSOMA
Kusoma kuna faida nyingi sana. Bila ya shaka, elimu
ndio huzisafisha na kuzitakasa nafsi za wanadamu, ikazirekebisha tabia zao mbaya na
kuwaongoza katika njia ya kheri. Kusoma ni miongoni mwa amali tukufu ambazo mja anaweza
kujikurubisha nazo kwa Mola wake, kwani bila ya elimu watu wasingeliyajua mambo ya dini
wala ulimwengu wao, bali wangeliyafuata matashi na matamanio ya nafsi zao. Kutokana na
sababu hizi na nyinginezo ndio Mwenyezi Mungu akawaletea wanadamu mitume ili waje
wawafundishe yaliyo na manufaa kwao katika dini yao na ulimwengu wao. Mwenyezi Mungu
hakuwaacha mitume waitekeleze kazi aliyowapa ya kuwaelimisha waja wake bila ya muongozo,
bali aliwapa muongozo akawaagiza:"WAITE(watu) KATIKA NJIA YA MOLA WAKO KWA HIKIMA NA
MAWAIDHA MEMA NA UJADILIANE NAO KWA NAMNA ILIYO BORA
"(16:125) katika jumla ya
faida za kusoma ni kufuzu kwa kupata daraja kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu ulimwenguni.
Amesema Mola Mtukufu: "MWENYEZI MUNGU ATAWAINUA WALE WALIOAMINI MIONGONI MWENU; NA
WALIOPEWA ELIMU WATAPATA DARAJA ZAIDI" (58:11)
ii) TWAA
Moyo na nafsi ya mwanadamu imeumbwa katika maumbile na tabia ya kufuata au
kutofuata inayoelekezwa na kuamrishwa kutenda au kutotenda. Nafsi inapojijengea utamaduni
wa kufuata na kutekeleza iliyoamrishwa na kujiepusha na kuyaacha iliyokatazwa, hiyo ndiyo
twaa (utii) na mtu mwenye nafsi yenye sifa hizo huitwa mtiifu. Imempasa na kumlazimu
mwanadamu kumtii Mola Muumba wake, kumtii mtume wa Mwenye Mungu na watawala wanaotawala
kwa kufuata muongozo wa Mwenyezi Mungu, haya ni kwa mujibu wa kauli ya Mola isemayo:-
"ENYI MLIOAMINI! MTIINI MWENYEZI MUNGU NA MTIINI MTUME NA WENYE MAMLAKA JUU YENU,
WALIO KATIKA NYIE(Waislamu wenzenu)"(4:59)
Hii ni twaa ya kwanza kabisa, twaa ya pili ielekezwe kwa wazazi. Wazazi wako ndio
sababu ya kuwepo kwa leo katika maisha haya,
Na wamepata taabu, mashaka na shida chungu nzima katika kukuzaa, kukulea na
kukuelimisha mpaka ukawa mtu mzimajunayeweza kuyasimamia mambo yako mwenyewe. Kwa
kuyazingatia yote haya Mwenyezi Mungu anatuamrisha:
"MOLA WAKO AMEHUKUMU KUWA MSIMUABUDU YOYOTE ILA YEYE TU NA (ameagiza)
KUWAFANYIA WEMA(mkubwa) WAZAZI KAMA MMOJA WAOAKIFIKIA UZEE, (naye yuko) PAMOJA NAWE, AU
WOTE WAWILI, BASI USIWAAMBIE HATA AH! WALA USIWAKEMEE NA USEME NAO KWA MSEMO WA
HISHIMA(kubwa). (17:23))
Twaa ya tatu ni kuwatii
wanawazuoni na walimu. Wakati ambapo mzazi humlea mwanawe kimwili kwa kumpa chakula,
mavazi na mahala pa kulala mwalimu humlea mtoto kiroho na kiakili, vitu viwili hivi roho
na akili ndivyo humfanya mtu kuwa mwanadamu kamili aliyetofautiana na viumbe hai vingine.
Mwalimu ndiye sababu ya mtoto kumjua mola wake, kuijua daraja ya wazazi wake, kuijua dini
yake na ulimwengu wake. Kwa sababu hizi na nyingine tusizozitaja imempasa mtoto/mwanafunzi
kumtii, kumuheshimu na kumpenda mwalimu wake na kutokasirika anapomtia adabu.
|